Tuwarudishe wabunge wote wa CCM?


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 21 April 2010

Printer-friendly version
Tafakuri
Samwel Sitta

UCHAGUZI ni njia ya kawaida katika nchi ya kidemokrasia ya kuondoa madarakani viongozi wazembe, wasio na maono, wasio na uwezo na ambao ni mzigo kwa taifa. Njia isiyo ya kawaida ni kuwashikia viboko, kuandamana na kuwatimua kama ilivyotokea huko Kyrgyzstan majuzi na kama inavyoonekana nchini Thailand.

Pale njia ya kawaida ya kidemokrasia ya kufanya mabadiliko inaposhindikana, basi wananchi wanayo haki na wajibu wa kutumia njia zisizo za kawaida. Hata hivyo, naamini katika taifa letu hatujafikia mahali pa kukiri kuwa njia za kawaida zimeshindikana.

Mambo kadhaa ambayo yametoka katika Bunge la Jamhuri kwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa miaka hii yote na hasa baada ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi yanatufanya tujiulize kama uchaguzi huu wa 2010 unaweza kutumika kama njia ya kawaida ya kuwakataa viongozi wasiofaa na kuwatimua madarakani bila kujisikia hatia, hisia ya usaliti, unyonge au kwa namna yoyote kujiona kuwa hatuwatendei haki.

Wiki iliyopita niligusia kidogo tu swali la kuchangia au kutochangia kampeni za CCM kama zilivyozinduliwa na mwenyekiti wake Rais Jakaya Kikwete. Nimepokea barua pepe za kutosha kutoka kwa watu ambao baada ya kusoma makala ile waliweza kufikia uamuzi ambao waliona unawafaa kwa dhamira zao.

Katika makala ya leo nataka twende mbele kidogo wakati bado tunafikiria kuchangia au kutochangia CCM hasa ukizingatia kuwa muda si mrefu ujao Rais Kikwete na viongozi wengine wa juu wa CCM watashiriki katika hafla za harambee za kuchangia “CCM ishinde.”

Nina uhakika wafanyabiashara na watu mbalimbali wenye uwezo wataalikwa kwenye hafla hiyo ambayo siyo jambo geni katika medani za kisiasa kwenye nchi zinazojaribu kujenga utawala wa kidemokrasia. Bila ya shaka hata wabunge na wagombea wengine nao wanaweza kuandaa vitu kama hivi (siamini kama wanaweza kwa mujibu wa sheria waliyoipitisha wenyewe).

Kwa upande wa wabunge wa CCM wanaotaka kugombea tena swali la muhimu ambalo wananchi wanatakiwa kujiuliza na kulipatia jibu lake ni kama wako tayari kuwarudisha wabunge hawa hawa Bungeni kwa kipindi kingine tena. Ni lazima tutambue kuwa kuchangia CCM ishinde maana yake ni pamoja na kuwarudisha wabunge kadha wa kadha ambao tungependa wasirudi tena.

Mimi ni miongoni mwa watu ambao naamini kama taifa tutafanya makosa makubwa kama tutaamua kuchagua wabunge mwaka huu kwa kigezo cha kipuuzi cha “ujana”. Tutakuwa tunakosa hekima na busara kama tutaangalia sura za watu na kuamua kama ni vijana au kuangalia kama wanamvi na kwa kutumia vigezo hivyo kuamua kuwaondoa waliopo. Ninawakebehi na kuwadharau wale wenye kuhubiri siasa za “ujana” dhidi ya zile za “uzee” kana kwamba tukichagua vijana basi mabadiliko yatatokea nchini.

Ninaamini kigezo pekee ambacho Watanzania wanatakiwa kukitumia ni kile cha Uwezo. Kinyume na wale wenye kutukuza vigezo vya “elimu na ujana” mimi ninaamini kabisa tatizo letu kama taifa haliko kwenye vitu hivyo bali kwenye uwezo tu. Kama tutaamua kuwatimua wabunge kwenye uchaguzi huu unaokuja na kuwaingiza wengine ni lazima tufanye hivyo kwa kipimo cha uwezo tu si kitu kingine.

Uwezo huu haupimwi kwa ahadi ya nini mgombea atafanya akichaguliwa; wale haupimwi kwa kuangalia mgombea anaahidi kuwa anawafahamu kina nani. Kwa mfano, mgombea anayekuja na kutuambia kuwa akichaguliwa atatutafutia “wafadhili” au “misaada” ili kutusaidia kujenga shule zetu, vyoo, na madarasa ni mgombea mwenye mawazo ya mgando; hatufai.

Mgombea anayekuja na kutoa ahadi kuwa kwa vile yuko karibu na Rais au viongozi wa juu basi ataweza kuwashawishi wafanye hili au lile naye ni kiongozi wa kuogopwa kwani hana maono yake binafsi.

Viongozi ambao taifa linawahitaji ni viongozi ambao wana uwezo wa kuangalia jamii wanazotaka kuziongoza na kutoka humo kuweka kuwa na maono ya jinsi gain ataiongoza jamii hiyo katika kujitegemea kutengeneza maisha yao yakawa bora zaidi.

Kwa mfano, akija mgombea ambaye anatuambia kuwa akichaguliwa tutakuwa na kampeni ya usafi mtaani kila Jumamosi ili kuweka mazingira yetu yawe ya kiafya na kampeni ya kupaka rangi mashule na hospitali zetu kwa namna ya kujitolea huyo ni bora zaidi na wa kuungwa mkono kuliko mgombea anayesema ataenda Ulaya kututafutia rangi, na mafagio!

Tunahitaji wagombea ambao wana mawazo ya kutufanya tujiletee maendeleo sisi wenyewe na kuyadumisha; maendeleo ambayo vyanzo vya nje ya jimbo ni nyongeza tu na si msingi kamwe.

Ni kutokana na hilo basi watanzania wanaitwa kuamua kama wabunge wa CCM walio nao sasa ni wenye mawazo tegemezi au ni wenye mawazo ya kujitegemeaz? Je ni watu ambao wanatuamsha tutumie raslimali zetu kujiletea maendeleo yetu au wanataka tutumie raslimali zetu kuendeleza maendeleo ya nchi za kigeni?

Je, ni wagombea ambao wanaamini Watanzania wanauwezo wa kujiletea maendeleo wao wenyewe wakiunganisha nguvu zao za mwili, kiakili na mali? Kama jibu la swali lolote kati ya hayo hapo juu ni “hapana” mgombea huyo ni wa kutimuliwa!

Tutawajuaje? Wapiga kura wa mwaka huu wameamka. Mapambano ya kifikra ambayo tumeyachochea miaka hii minne yamewafanya kuwa na uwezo wa kuuliza maswali sahihi. Naamini, wagombea watakaokuja na kutaka kugombea au wanaojipitisha pitisha wanapaswa kujibu maswali yafuatayo:

Kwanza, unataka kufanya nini kwenye jimbo letu? Pili, utapata wapi fedha za kufanya hicho unachotaka kukifanya ukiondoa wahisani na wawekezaji kutoka nje na serikali kuu?

Tatu, utafanya nini ili kuhakikisha jimbo letu linajitegemea katika masuala ya elimu, afya, na miundombinu?

Nne, kwenye masuala ya kitaifa una msimamo gani matumizi mabaya ya fedha za umma na mabadiliko gani ya sheria utayapigania ili kuleta nidhamu ya fedha?

Tano, una msimamo gani kuhusu watumishi wa ngazi za juu wanaotajwa kuhusika na vitendo vya ufisadi wakiwa madarakani, waliokuwa na kinga wavuliwe ili washitakiwe?

Sita, kabla ya wakati huu umefanya nini kutuonesha uongozi na kutupa uwezo wa sisi kujitegemea na kuinua hali ya maisha yetu? Kwa mgombea aneyerudia – unadhani maisha yetu ni bora kuliko miaka mitano iliyopita hadi wewe umeamua kugombea?

Hayo ni baadhi ya maswali ya msingi tu kuwauliza wanaotaka kugombea. Yeyote atakayejiuma uma kuyajibu huyo ni wa kutimuliwa kwenye kura za maoni kwanza na akinusurika kukataliwa kwenye uchaguzi mkuu.

Kumbuka, nchaguzi ni njia ya kawaida katika nchi ya kidemokrasia ya kuwafukuza madarakani viongozi wazembe, wasio na maono, wasio na uwezo na ambao ni mzigo kwa taifa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: