Tuzindue akili za serikali


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 04 July 2012

Printer-friendly version

HESABU ngumu. Kila hatua au ngazi fulani ya utoaji elimu huwa kuna hesabu ngumu kulingana na uwezo wa wanafunzi husika.

Walimu wakitoa maswali darasani, kama ni rahisi, wengi watanyosha juu mikono kujibu, lakini kama maswali ni magumu, utaona wakijipiga kwenye paji la uso kuzindua akili zao wapate majibu sahihi.

Hesabu nyingine ni chemsha bongo. Waulize wanafunzi wa darasa la tatu, “kipi kizito kati ya kilo 20 za pamba na kilo 20 za mawe,” haraka watajibu kilo 20 za mawe. Kwanini?

Waulize wanafunzi wa darasa la saba kwamba wako Morogoro na wanataka kununua baiskeli moja. Mjini Morogoro inauzwa Sh. 100,000 lakini Dar es Salaam ni Sh. 90,000. Je, ni busara kwenda kununua Dar es Salaam au Morogoro?

Chemsha bongo nyingine si ngumu ila majibu yake. Jibu la chemsha bongo nani ana elimu bora zaidi na inayostahiki malipo yaliyonona kuliko mwingine kati ya mwalimu, ofisa kilimo, daktari na mwanasheria ni gumu.

Rafiki yangu, ofisa katika Idara ya Ukaguzi Kanda ya Ziwa amenitumia ‘kaujumbe kenye namba,’ kujibu swali hilo.

Mshahara wa wenye cheti: Mwalimu Sh. 244,400; afya Sh. 472,000; kilimo Sh. 959,400; Sheria Sh. 630,000. Wenye diploma: Mwalimu Sh. 325,700; afya Sh.682,000; kilimo Sh. 1,133,600; Sheria Sh.871,500.

Wasomi wenye digrii: Mwalimu Sh. 469,200; afya Sh. 802,200; kilimo Sh. 1,354,000; Sheria Sh. 1,166,000.

Majibu magumu. Mawaziri wa serikali ya Awamu ya Nne, wametoa majibu magumu ya hesabu ngumu za kumaliza mgomo wa madaktari.

Walipokutana kutafakari wafanye nini; wawafute kazi madaktari wote au wawaongezee minoti na kuboresha huduma za afya hospitalini kama wanavyodai madaktari, mawaziri wakatoka na jibu gumu.

Eti mawaziri woooooote 30 wakakubaliana wawafute kazi kuliko kuwaongezea hata Sh. 100,000 kisha watafute mabilioni ya shilingi ya kulipa madaktari kutoka nje – ma TX.

Wakapiga makofi kujipongeza kwa jibu hilo la busara kujibu hesabu ya matakwa ya madaktari, halafu mkubwa wa mawaziri akaenda Mjengoni kusema “…liwalo na liwe” na kwamba kesho yake angetangaza msimamo.

Eti atangaze kuwa wamekosa vijisenti vya nyongeza kwa madaktari ila wamepata Sh. 200 bilioni kwa ajili ya kuwalipa madaktari ma TX. Aibu! Sh. 200 bilioni kwa ajili ya maboresho ya huduma hazipo lakini zilizopo ni za kulipa madaktari wa kigeni?

Akili hii ya serikali haina tofauti na Dogo Aslay wa kundi la Wanaume Family alivyoimba kumsema baba yake katika kibao cha Naenda Kusema kwa Mama. Aliimba

Nyumbani mama umemwachia buku...
Kishtobe umemnunulia kuku...
Kurudi kwako ni usiku...
Naenda kusema kwa mama...
Nasema, nasema...

Serikali inawapa ‘buku’ tu madaktari wazalendo lakini inaandaa mabilioni kwa wageni. Heri hata madaktari, walimu je?

Akili hii sawa na ya polisi wetu. Nenda polisi kawape taarifa ya kufanya mkutano pale Jangwani; utaambiwa hakuna polisi wa kutosha kwa ajili ya kulinda usalama.

Lakini ukifanya mkutano kwa nguvu, bila kibali chao, polisi lukuki  waliosheheni silaha na wenye kiu ya kuua utaona wamejaa wakitangaza mkutano uvunjwe. Wametoka wapi hawa?

Vyama vya siasa vikisema vinaandamana, waziri wa polisi atasema taarifa za kiintelejensia zinaonyesha kuwa Al Shabab watashambulia. Lakini intelejensia ya polisi imeshindwa kujua mipango ya kutekwa na kuteswa kwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka. Ipo haja ya kuzindua akili ya serikali.

0
No votes yet