Twendako giza


editor's picture

Na editor - Imechapwa 02 February 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

IWAPO kiwango cha kufaulu watoto wanaotarajiwa kuingia kidato cha kwanza kinazidi kushuka kwa miaka mitatu mfululizo, na kile cha wanaotarajiwa kuingia ngazi ya juu ya sekondari nacho pia kinashuka, serikali imeshindwa.

Takwimu za Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) zilizotolewa wiki iliyopita kuhusu matokeo ya mitihani ya kidato cha nne zinahuzunisha.

Tafsiri yake, ni kwamba katika watoto kumi waliofanya mtihani huo, watano wameanguka au katika watoto wawili, mmoja amefeli. Hawataingia kidato cha tano.

Maana yake uwezo wa Taifa letu kuzalisha wataalamu wa fani mbalimbali unapungua siku hadi siku. Uwezo wa Taifa kujenga vijana wake kitaaluma unakufa.

Haitafika siku miaka 15 au 20 ijayo tukapata uwezo wa kushindana kwa jambo lolote ambalo ushiriki wake unahitaji watu waliowiva kitaaluma.

Zipo fursa za kimaendeleo kanda ya Afrika Mashariki, lakini kwa sababu hiyo, uwezo wetu wa kushiriki kiushindani na nchi jirani kama Kenya na Rwanda unaporomoka. Wenzetu wanakimbia, Tanzania tunasota.

Sera za serikali ya CCM zinaangusha taifa. Hazina tija wala matumaini. Ni rahisi kusema CCM kama chama cha siasa imeshindwa kujibu changamoto zinazokabili taifa.

Elimu ndio ufunguo wa maisha na chimbuko hasa la maendeleo yoyote duniani. Lakini kwa Tanzania, kwa inavyosimamiwa, inatuchongea. Elimu tunayoiona inadhoofisha nuru ya maendeleo.

Mtu ungetarajia kwa kuwa Tanzania imeongozwa kwa miaka yote ya uhuru karibu miaka 50 na chama kimoja cha siasa, ingeshuhudia maendeleo makubwa.

Serikali iliyopo inaitizama elimu kisiasa zaidi kuliko kitaaluma. Sera zake ni butu na zilizo nzuri, zinasimamiwa kisiasa zaidi kuliko kitaalamu.

Siasa ni jambo jema lakini inapotumika kuleta mabadiliko katika maendeleo. Ikiendeshwa kishabiki badala ya kisayansi inaleta matokeo hasi. Serikali ya CCM inaendesha siasa kishabiki na matokeo yanaonekana. Hakuna tija.

Matokeo ya kuanguka kila mwaka kwa viwango vya kufaulu vijana wa Tanzania ni ushahidi mzuri wa hatari iliyopo kwa maendeleo kuzidi kuwa ndoto.

Rais Jakaya Kikwete alikuta sera na mpango wa kuimarisha elimu ya msingi (MMEM) ulioanza kutekelezwa na awamu iliyomtangulia. Serikali yake ilibadilisha, ikaja na yake. Ikajenga shule za kata. Ikasahau walimu bora, nyumba zao, vifaa vya kufundishia, maabara kwa ajili ya masomo ya sayansi.

Ikazalisha walimu wa chap-chap – waliitwa walimu Vodafasta. Wiki nne una mwalimu wa kufundisha sekondari. Tangu lini haya?

Wale walioingizwa kidato katika mazingira hayo ndio hawa waliofeli leo. Ni janga. Tunaendekeza “bora elimu” badala ya “elimu bora.”

Watanzania wanaingizwa gizani. Huko siko. Kama Umoja wa Vijana wa CCM wanasema Bodi ya Mikopo ipinduliwe; sisi tunasema CCM ipinduliwe; tupate elimu bora.

0
No votes yet