Uamsho hai, Dola kandamizi na Muungano


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 20 June 2012

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

SASA tunalo tatizo sugu na la msingi Zanzibar – utawala mbaya. Chembechembe za utawala wa aina hii zinapoachwa na kukua, matokeo yake ni kupandikiza chuki kati ya dola na wananchi.

Pale utawala na wananchi wanapochukiana, watategana, wataviziana, watatunishiana misuli. Kila upande utataka kujithibitisha ulivyo na nguvu.

Ni kawaida kwa dola kuwa na nguvu nyingi. Hizi huchangiwa na ile asili ya dola kuwa ni chombo cha mabavu; lakini pia kwa sababu utawala utataka kuthibitishia wananchi kuwa chombo hicho kweli ni cha mabavu.

Zanzibar sasa inashuhudia utawala kutaka kuthibitisha unazo nguvu kubwa kuliko raia. Lakini, laiti kiongozi mkuu, rais, angefikiri vizuri na kutanabahi, wala asingehitaji kuthibitisha nguvu za dola – zinajulikana.

Hakuna hata chembe ya haja kwa serikali kuonyesha nguvu zake kwa wananchi. Nguvu za serikali zipo tu hata iweje; zinajulikana vema, zinatajwa mpaka kwenye katiba ya nchi.

Katiba ya Zanzibar, 1984, iliyorekebishwa mara ya mwisho 2010 na kuruhusu kura ya maoni, inazitaja nguvu hizi. Inasema kutakuwa na rais, ambaye atachaguliwa na wananchi.

Utaratibu umesema atachaguliwa kila baada ya miaka mitano na atakaa kwa kipindi kingine cha miaka mitano, iwapo atachaguliwa tena, ambapo atalazimika kustaafu.

Katiba hiyohiyo inabainisha majukumu na wajibu wa rais. Basi inaelezwa atakuwa hivi; atakuwa vile; atafanya hili; atafanya lile.

Jinsi alivyo “mtu mkubwa mwenye nguvu kubwa” imeelezwa kuwa rais atakuwa mwenyekiti wa baraza la mapinduzi, ataapisha watendaji wote aliowateua, na yeye pia ni sehemu ya baraza la wawakilishi, chombo cha kutunga sheria.

Hayo ni mamlaka makubwa, ya kutosha kabisa kwa binadamu wa kawaida. Lakini je, madaraka hayo yanatumika vizuri, rais anayatumia vizuri, kwa manufaa ya wananchi? Hili ndio swali muhimu hapa.

Sasa, ni muhimu sana kwa utawala, Rais Dk. Shein, kujua kuwa kadiri unavyojitutumua na kutaka kuthibitisha nguvu zake kwa raia ndivyo anavyojiruhusu kuchukiwa na wananchi.

Hakuna mwananchi atakayekubali kuuvaa ujinga na kuridhia kuiunga mkono serikali iliyoanza kutunisha misuli – kutumia askari wake wenye silaha – dhidi ya raia haohao.

Tarehe 26-27 mwezi uliopita, mji wa Zanzibar ulikumbwa na fadhaa kutokana na machafuko yaliyozushwa na utendaji usio wa “Polisi Jamii” wa Jeshi la Polisi.

Walimkamata mmoja wa wahadhiri wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI) Zanzibar, Ustadh Mussa Juma Issa, magharibi akiwa msikitini Kwa Biziredi.

Mwalimu huyu alikamatwa kishenzi-shenzi maana aliyetumwa kumfuata, alikosa busara na hata hekima pamoja na kujua fika wanayemtaka hana silaha yoyote. Uthibitisho ni kilichotokea baada ya wadai haki kubaini mwalimu wao alikamatwa kishenzi-shenzi.

Wakatimkia kituo kikuu cha polisi cha mkoa wa Mjini Magharibi, Muembemadema. Wakamdai mwalimu wao. Polisi wakaendelea kuzika busara na hekima, wakaamua ni bora watu wengi wakusanyike hapo lakini siyo kumuachia kwa dhamana mkamatwaji.

Basi usiku huo, kucha yake na kutwa ya siku ya pili, Jumapili, mitaa ya mji ikahanikiza sauti na mivumo ya risasi za mipira na mabomu ya kutoa machozi dhidi ya raia.

Silaha hizo zikatumika kuharibu afya za raia wazima na pia wagonjwa waliokuwa majumbani. Zikaharibu mali za watu ikiwemo ofisi ya mawakili. Tafrani kubwa ikatokea mitaani.

Hayo ndo matokeo ya matumizi mabaya ya nguvu za dola. Harufu ya kemikali mtindo mmoja, watu, hadi vitoto na vikongwe, kukohoa ovyo.

Niliposema Dk. Shein asisikilize fitna za baadhi ya wasaidizi wake, nililenga kutoa nasaha kwamba fitna huzaa maafa. Ndio haya yanayotokea.

Kumbe Polisi na washirika wao hawajaelewa somo. Labda wameelewa lakini wameelekezwa kwa hayo wanayoyafanya.

Bado nasema, hakujapatikana sababu ya maana inayojali maslahi ya umma na hata nchi, ya Polisi kupiga raia kipindi hichi. Haipo.

Uamsho wanafanya kazi yao. Wanafuata sheria. Laa kama hawafuati, mbona tukiwauliza huwa wanasema hawajazuiwa kwa namna yoyote ile rasmi na serikali, isipokuwa kukurupushwa na Polisi wenye silaha?

Sasa Jumamosi na Jumapili zinakuwa siku za giza Zanzibar. Siku ambazo akili za Polisi huelekezwa katika kutumia risasi dhidi ya raia.

Ile iliyopita ilikuwa Jumamosi na Jumapili; basi Jumapili wiki hii Polisi wakajipanga tena. Kwa bahati mbaya, mkuu wao Zanzibar akawa tayari kwa lolote.

Kweli, akaamuru askari wawapige wananchi  waliokuwa wanakwenda kushiriki mhadhara kwenye msikiti wa Donge, kaskazini Unguja.

Msafara wa wana-Uamsho ulipofika Mahonda, karibu na kituo cha polisi, ukazuiwa. Kisa? Eti Polisi wamepokea barua ya Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini, ya kuzuia msafara huo kwenda Donge. Yote hayo ni kuzuia Muungano kuguswa!

Ni hoja dhaifu sana tukizingatia dhana ya utawala bora. Kwamba bosi wa mkoa ameamuru polisi wazuie msafara wa wananchi kwenda Donge, yeye amepata wapi mamlaka hayo?

Kwani yeye na sheria afatwe nani? Mtendaji yeyote mwenye kufikiri vizuri atafuata sheria si mtu anayeitwa mkuu wa mkoa.

Tatizo ni kwamba hawa wakuu wa mikoa, kama walivyo wa wilaya, hawatii sheria, bali mabavu.

Ndio maana haishangazi leo kukuta hata masheha, viongozi wa hadhi ndogo mno katika mtiririko wa uongozi wa serikali, wanahalifu sheria na hawaulizwi kitu.

Penye utawala bora, utawala mzuri, mkuu wa mkoa alitakiwa aite viongozi wa Uamsho. Akae nao ofisini huku akionyesha uchangamfu. Yeye si ni mtumishi wa watu?

Labda aseme anamtumikia rais. Mbona rais mwenyewe anatumikia watu, au Dk. Shein amepa kutumikia Chama Cha Mapinduzi (CCM)? Mamlaka ni ya wananchi siyo chama.

Mkuu wa mkoa angewaeleza Uamsho rai yake. Angewasikiliza nao wanasemaje. Rai yake ingejadiliwa. Wangejadiliana. Mwisho, wangeafikiana au kutofautiana. Amani ingedumu. Mkubwa huyu hakufanya hivyo.

Aliamuru Polisi. Hawa ni watumishi wa kupokea amri tu. Kweli, historia ya Zanzibar inaonyesha polisi hupokea hata amri za Masheha na maskani za CCM.

Polisi wangekuwa wanafanya kazi vizuri, wangekuwa wamefuta mapema maandishi ya uchochezi yaliyoandikwa kwenye ubao wa maskani ya CCM Kachorora. Siyaandiki hapa maana yanatapisha.

Polisi wamelazimisha msafara usipite Mahonda. Wenye haki ya kutembea nchi yao na kushiriki mijadala hai siyo hoi, wakahoji sababu ni nini? Ati nini? Mkuu wa Mkoa ameagiza tuwazuie msiende Donge, anasema mkuu wa polisi. Lahaula.

Mbinu za watawala wabaya. Dola inayotumia polisi kuogopesha raia, kukandamiza haki zao na kuwazuia watu kufikiri na kuamua, haina jina tamu isipokuwa “dola kandamizi.”

Haya twendeni. Dola sakama Uamsho, wakandamize kisawasawa, bali waachie wanamaskani watambe. Tutaona mwisho wa safari hii ya ovyo ambayo serikali ya Dk. Shein imeanzisha. Kweli tutaona.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: