Uamsho wamenena


editor's picture

Na editor - Imechapwa 27 June 2012

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KAMA kilichotangazwa na Uamsho – kuelekeza wananchi Visiwani kujitokeza kutoa maoni yao kuhusu katiba mpya ni kweli, basi jumuiya hiyo imechukua mkondo sahihi.

Tangu Desemba mwaka jana, Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI) imekuwa ikihamasisha Wazanzibari kukataa kutoa maoni juu ya katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Badala yake, imekuwa ikiwahimiza wananchi hao kuukataa Muungano na sambamba na hilo, ikichukua hatua zinazoelekea katika kuishinikiza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar iitishe kura ya maoni.

Katika kushinikiza kura hiyo, Uamsho wanataka kwanza Wazanzibari wapewe fursa ya kutoa kauli kama wanautaka Muungano na kwa mfumo gani.

Baada ya kutafakari kwa makini, huku kukiwa na taarifa za mafungamano na serikali, viongozi wakuu wa Uamsho wameamua kulegeza kamba.

Sasa Uamsho wanazungumzia kwamba kitendo cha kushajiisha watu kugomea kutoa maoni yao kuhusu katiba mpya, kutawapa mwanya wale inaowaita “watu wasioitakia mema” nchi ya Zanzibar wa kuwasemea wananchi isivyostahiki.

Ni matumaini yetu kuwa tamko lao, lililotolewa na kiongozi wao mkuu, Sheikh Farid Hadi Ahmed, litashusha joto lililokuwa likizidi kupanda Zanzibar hata kufikia kusababisha mapambano kati ya Polisi na wananchi.

Harakati zilizoanzishwa na Uamsho mara baada ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza nia ya serikali yake kuanzisha mchakato wa kupatikana kwa katiba mpya yenye ridhaa ya Watanzania, zilishaanza kuleta athari na mpasuko katika jamii.

Watu kadhaa wameumia na mali nyingi za watu binafsi na zile za taasisi za dini zimeharibiwa huku katika nchi kukitanda wingu la fadhaa kutokana na hatari ya amani kuvunjika.

Ingawa madai ya Uamsho yalikuwa na yangali ya haki kwa mujibu wa sheria, yalitumiwa vibaya na watu wasioitakia mema nchi au kuiona Zanzibar ya maridhiano ikizidi kustawi.

Kwa kuwa Uamsho wameshatoa tamko la kutaka watu wanaowatii waende kutoa maoni yao kuhusu katiba mpya pale tume itakapofika kwao, na kwa kuwa wametangaza wazi kuunga mkono serikali ya Rais Dk. Ali Mohamed Shein, kilichobaki ni kwa serikali nayo kutimiza wajibu wake.

Wajibu tunaousema ni ule wa kuweka mazingira mazuri yatakayowezesha wananchi kutoa maoni yao kwa uhuru wa kutosha huku ikihakikisha hakutatokea tena vitendo vya kihalifu kama vilivyotokea.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: