UAMSHO Zanzibar waibana serikali


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 16 May 2012

Printer-friendly version
Zanzibar

TAASISI za Kiislamu Zanzibar zinakusanya saini 450,000 za wananchi ili kushinikiza serikali kuitisha kura ya maoni ya kuamua hatima ya Muungano, MwanaHALISI imebaini.

Kazi hiyo inaratibiwa na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI) au Uamsho, kama inavyojulikana kwa ufupi.

Naibu Amir wa Uamsho, Sheikh Azzan Khalid Hamdan ameliambia gazeti hili kwamba wamechapisha fomu 25,000 na kuzisambaza nchi nzima kwa matarajio ya watu kuzijaza.

“Kama fomu zote 25,000 tulizosambaza zitajazwa na kutufikia, tutakuwa tumepata saini 450,000… yatakuwa mafanikio kwa asilimia 100. Lakini hata tukipata saini 250,000 tu, itakuwa hatua nzuri,” alisema.

Kila fomu imeandaliwa kwa ajili ya watu 20.

Alipoulizwa iwapo wanapata upinzani katika kutekeleza azma yao, alisema vitisho vipo lakini vinazimwa kutokana na hamasa kubwa waliyonayo wananchi.

“Tulifanya jambo zuri kutangulia kutoa elimu kwa raia kujua haki zao. Kazi ya miezi mitatu ile imetusaidia sana kuamsha watu na sasa wanatafuta fomu bila ya woga maana wanajua hawavunji sheria.

“Huu umekuwa msisitizo wetu kila tunapokwenda. Tunasoma vifungu vya katiba vinavyotulinda na katika suala hili hatutaki masihara kabisa; kwani hapa tunapigania maslahi ya nchi na watu wake,” alisema.

Alipoulizwa iwapo wamesimamisha mihadhara iliyokuwa ikihamasisha watu kuhusu mustakabali wa Muungano, alisema mihadhara inaendelea “licha ya vitimbi vya baadhi ya viongozi” binafsi wa serikali.

“Hata jana (Jumapili) tulikuwa na mhadhara Pemba; na kwa Unguja tulikuwa Fujoni, mkoa wa Kaskazini, ambako tulizishinda mbinu za polisi kuvuruga mhadhara wetu,” alieleza.

Naibu Amir Azzan alisema walimwambia kamanda wa polisi mkoani, kwamba hakuna amri yoyote ya kusimamisha mihadhara.

Alisema kamanda huyo aliwaambia ana barua ya serikali inayozuia mihadhara hiyo, lakini wao walimjibu kwamba kama kuna amri, wangeandikiwa wao ambao ndio wanaendesha mihadhara.

“Tulimwambia wazi kuwa sisi hatuvunji sheria yoyote ya nchi, na hakika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 inalinda haki yetu.

“Hakuna mtu mwenye haki ya kuzuia wananchi kushiriki shughuli za umma; na kwa kweli, yule anayezuia wananchi kutumia haki yao hiyo ndiye mvunjaji sheria,” alifafanua.

Amesema kwa fikra zake, serikali haipendi lakini “haiwezi kuzuia kwa sababu viongozi wanajua wananchi wana haki ya kikatiba kushiriki katika mambo yenye maslahi na umma.”

Amesema walieleza msimamo huo walipoitwa na kamati ya mawaziri na wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama na kutakiwa kueleza maoni yao kuhusu mihadhara yao.

0
No votes yet