Uasi wa wabunge kwa mawaziri ni halali


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version

KUNA burudani ya aina yake bungeni. Baadhi ya wabunge wameshika makoo ya mawaziri kama vile uchaguzi mkuu unafanyika mwaka huu, si mwaka kesho.

Mfano hai, ni hatua ya mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, kukataa kufuta kauli yake bungeni, kwamba Naibu Waziri wa Fedha, Jeremiah Sumari, alitoa majibu ya “ovyo ovyo” kwa mbunge wa Karatu (Chadema) Dk. Wilbrod Slaa.

Zitto, mbunge wa Kigoma Kaskazini aliamua kumtolea uvivu waziri Sumari baada ya waziri huyo majibu ya “ovyo kuhusu ukwapuaji wa mabilioni ya shilingi uliofanywa na kampuni ya Meremeta.”

Kampuni ya Melemeta iliyokuwa inamiki mgodi wa dhahabu wa Buhemba, mkoani Mara ulichotewa na serikali mabilioni ya fedha za umma kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kinyume cha taratibu.

Akijibu swali hilo, Sumari alisema suala hilo haliwezi kuzungumzwa hadharani, kwa kuwa linagusa masuala ya usalama wa taifa, kwa maelezo kwamba kampuni hiyo iko chini ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Baada ya Zitto kutakiwa kufuta usemi wake na Mwenyekiti wa Bunge, Zubeir Ali Maulid, alisema yu radhi kukabiliwa na lolote, na kwa hali hiyo aliendelea kuchangia mjadala wa hoja ya makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Mbali na Zitto kuelekeza hoja kali kwa Sumari, pia wapo wabunge wengine kama Lucas Selelii (Nzega-CCM), ambaye aliwashambulia vikali mawaziri wote, kiasi cha kuwatakia laana.

Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama, naye hakufanya ajizi. Alimsulubu vilivyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia.

Mhagama alimtaka waziri huyo kutoa maelezo kuhusu zaidi ya watumishi 10 wa Halmashauri ya Songea, ambao hawajaingizwa kwenye orodha ya malipo, licha ya kuitumikia serikali kwa zaidi ya miaka 20. Ilibidi Spika wa Bunge, Samwel Sitta, kuingilia kati kwa kumtaka waziri huyo asijibu kutokana na ukosefu mawasiliano.

Orodha ni ndefu. Kuna Mudhihir Mohamed Mudhihir (Nchinga-CCM) ambaye alimfananisha waziri mmoja na nyoka wa kwenye mdimu.

Mashambulizi haya makali kwa mawaziri, na kauli nyingine nyingi za wabunge zinaonyesha wabunge hawana imani na utendaji wa baadhi ya mawaziri, vilimfanya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa kauli kwamba tabia ya kuwashambulia mawaziri kwa kauli za ukali na kukunja uso si nzuri.

Pinda alikwenda mbali zaidi na kuwataka wabunge kuwa na staha wanapowajadili hoja za serikali.

Aliasa wabunge kuwa na ushahidi wa kile wanachotuhumu, kwa sababu wanaweza kuaibika kama mawaziri wakipewa fursa kujibu, kiasi cha kuonekana kwamba wanachosema hakina ukweli wowote.

Lakini Pinda anapaswa kufahamu kwamba wabunge wamefikishwa kwenye hali hiyo ya kukosa uvumilivu na staha kwa mawaziri, kwa sababu ya tabia ya mawaziri husika.

Ni kawaida kwa mawaziri kujiona wako juu zaidi kuliko wabunge, kiasi cha kutoa majibu ya ovyo pale wabunge wanapozungumza bungeni.

Kwa mfano, hakuna wabunge wanaojibiwa ovyo, na hata wakati mwingine kupuuzwa, kama ilivyo kwa wabunge wa upinzani.

Nani asiyekumbuka kwamba Dk. Slaa, kwa mfano, alitaka kuwasilisha hoja binafsi kuhusu EPA mwaka juzi, lakini alifanywa nini? Nani asiyejua kwamba Zitto alipowasilishwa hoja binafsi kuhusu mgodi wa Buzwagi, aliandamwa hadi akasimamishwa kuhudhuria mikutano ya Bunge?

Lakini ukiacha hao wawili, hivi nani asiyejua kwamba chimbuko la hasira ya wabunge dhidi ya mawaziri, ni tabia ya mawaziri ya kutumia nafasi zao kujijenga kisiasa, lakini wakiwaumiza wabunge wasiokuwa na nafasi serikalini.

Je, kisa cha Waziri Sumari kumjibu ovyo Dk. Slaa ni nini? Ni kielelezo kwamba serikali haiko tayari kujisafisha dhidi ya uchafu unaoizunguka.

Serikali imesema uongo juu ya kampuni ya Meremeta, kiasi kwamba inapozidi kubanwa inakosa uvumilivu na kuanza kusema ovyo.

Jaribu kujiuliza; kauli ya Sumari kwa Dk. Slaa. Hii ni kauli ya kuonyesha kukosa uvumilivu.

Serikali kupitia kwa mawaziri wake, inapokosa uvumlivu kwa sababu wameshindwa kutimiza wajibu wao na kuishia kuwajibu ovyo wabunge, hivi Pinda anataka wabunge wajikunyate na kulia?

Hivi mawaziri wanaposhindwa kuwapa wabunge majibu ya maswali yao kwa wakati, maswali ambayo wanatumwa na wapiga kura wao, Pinda anataka wabunge wajione wanyonge, wasiokuwa na haki wala nguvu ya kujibu mapigo?

Kwa muda mrefu, ambao nimekuwa nikifuatilia mijadala ya Bunge pamoja na maswali, nimejipatia jibu moja; kwamba kwa kiwango kikubwa mno, mawaziri wanajaribu kuremba mambo, lakini kwa bahati mbaya, wabunge, kwa sababu ya itifaki za kibunge, wanayakubali majibu yaliyojaa maneno matamu ya mawaziri, lakini shida za wananchi zikiwa pale pale, mwaka hadi mwaka.

Ndiyo maana watu wanapopoteza uvumilivu kama alivyofanya Zitto, msimamo wa kukataa kuburuzwa unakuwa ni njia pekee ya kukabiliana na kejeli na unafiki wa kuheshimu watu wasiotaka kufanya kazi.

Kwa hali hii basi, Pinda kabla ya kuwaasa wabunge kuacha ‘uasi’ wao dhidi ya mawaziri, alipaswa kwanza kuhakikisha kwamba wanajibu hoja za wabunge kwa ufasaha na heshima. Kwamba ni marufuku waziri kujibu ovyo.

Kama waziri anakosa heshima kwa mbunge, kuna haja gani kwa mbunge kumheshimu? Kwani waziri ni mpiga kura hata mbunge aseme atanyimwa kura?

Wakati umefika kama mbunge atauliza swali kwa waziri katika mkutano wa Bunge na baada ya kipindi cha mwaka mmoja ahadi iliyotolewa ikawa haijatekelezwa, si vibaya kwa mbunge husika kumtaja waziri kama mwongo.

Ni vema wananchi wakakataa kutoa kura kwa wagombea wa serikali hiyo kwenye uchaguzi unaofuata kwa sababu bila maendeleo kwa wananchi hakuna uhalali wa serikali kurejeshwa madarakani.

Wananchi wakifuata fomula hii watajijengea nguvu na uwezo wa kukataa watawala wanaowahadaa mwaka hadi mwaka, uchaguzi hadi uchaguzi, bila kuleta mabadiliko yoyote ya maana kwa maisha ya wapiga kura wao.

Uasi wa wabunge dhidi ya mawaziri ni halali; ikibidi jeuri ya Zitto iwe kigezo. Kwa wananchi uasi ninaoutetea ni kwa mgombea yeyote ambaye atarejea kuomba kura ilihali miaka mitano iliyopita alipiga domo tu, huyo anyimwe kura.

Hasira, hamaki na kukunja uso kwa wabunge ni matokeo ya kukatishwa tamaa na mawaziri na serikali kwa ujumla.

Ili mawaziri waepuke uasi huu, wawe wakweli, watoe majibu ya dhati na kuonyesha unyenyekevu wa kweli, vinginevyo umma utakaa nyuma ya akina Selelii, Mhagama na Zitto wakati wanajibu mapigo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: