Ubunge wa Mwakyembe shakani


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 23 December 2009

Printer-friendly version
Lowassa, Rostam, Karamagi watajwa
Mwenyewe apambana mpaka mwisho
Dk. Harrison Mwakyembe

NGUVU kubwa na za kifedha na mikakati ya kisiasa, zinatumika kuhakikisha John Mwakipesile, mkuu wa mkoa wa Mbeya, anaingia katika kinyang’anyiro cha ubunge mwaka kesho katika Jimbo la Kyela.

Lengo ni kutaka kumtokomeza kisiasa mbunge wa sasa wa jimbo hilo, Dk. Harrison Mwakyembe, imefahamika.

Taarifa zinasema Mwakapisile anajengwa kisiasa na kiuchumi na mtandao mpana wa wanasiasa na wafanyabiashara wakubwa nchini.

Miongoni mwa waliotajwa kumsimika Mwakipisile, aliyewahi kuwa mbunge wa jimbo hilo ni mfanyabiashara na mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, mbunge wa Bukoba Vijijini, Nazir Karamagi na mfanyabiashara Shubash Patel.

Rostam, Lowassa na Karamagi ni baadhi ya majeruhi wakuu wa kashfa ya mkataba wa kufua umeme kati ya serikali na kampuni ya Richmond Development Company (LLC) iliyoibuliwa na Kamati Teule ya Bunge, chini ya Mwakyembe.

Ni kamati ya Mwakyembe iliyozamisha kisiasa Lowassa na Kamaragi, Februari 2008, huku ikimuacha Rostam katika majeraha makubwa ya kisiasa na kuchumi.

Wengine wanaotajwa kuwa nyuma ya Mwakipesile ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya, Nawab Mullah na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba.

Baadhi ya vijana waliohojiwa mjini Kyela wamemtaja pia mkurugenzi mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Cornel Apson Mwang’onda.

Matokeo haya ya uchunguzi wa muda mrefu yamesaidia kubaini uteuzi wa Mwakipesile kuwa mkuu wa mkoa uleule aliopotezea ubunge 2005, kuwa kiini cha harakati zake nyingi wilayani Kyela, ambazo zimeibua malalamiko kutoka kwa mbunge wa sasa, Dk. Mwakyembe kuwa anahujumiwa kisiasa.

Alipoulizwa juu ya juhudi hizi za kumg’oa, Mwakyembe alisema kwa ufupi, “Nimekuwa nikifanya kazi za umma ulionituma. Sitishiki na yeyote anayetaka nafasi hii. Wananchi ndio waamuzi.”

Harakati za Mwakipesile kuingia kwenye kinyang’anyiro cha ubunge mwakani zimechochea mawazo hasi mkoani Mbeya dhidi ya Rais Kikwete.

Kwa kumwacha Mwakipesile mkoani Mbeya muda wote huu, kuna wanaomwona Kikwete kuwa ni “mtu wa visasi” na asiyependa kuzungukwa na wenye mawazo tofauti.

“Rais Kikwete ameonyesha hampendi mbunge wetu na sababu tunazijua. Mbunge wetu alimuunga mkono Profesa Mwandosya (Mark) kwenye kura za maoni za urais mwaka 2005. Hivyo, alimteua Mwakipesile na kumbakiza Mbeya ili awakwamishe Mwakyembe na Mwandosya,” anasema mfanyabiashara katika soko kuu la Kyela, Jailo Mwangego.

Madai ya Mwangego yaliungwa mkono na wafanyabiashara wengine katika soko hilo, hasa wanawake, ambao walipandisha sauti zao wakidai kuwa Rais Kikwete “anamwonea” mbunge wao na kukemea kwa kusema juhudi za kumwangusha kwa kura mwakani “zitashindwa.”

Baadhi ya wananchi waliohojiwa mjini Kyela, wanawataja madiwani wanane kuwa ni mawakala wa Mwakipesile, ambao kazi yao kubwa ni kuzunguka wilaya nzima wakigawa magazeti bure yanayochapishwa kwa lengo la kumchafua Mwakyembe na kumnadi Mwakipesile na “vijana” wake.

Vijana wanaotajwa kuwa wanafaa kuchukua ubunge wa Kyela ni George Mwakalinga, Hunter Mwakifuna na Elias Mwanjala. Hata hivyo, inadaiwa kuwa Mwakipesile yuko nyuma ya vijana hao.

George Mwakalinga ni mwanafunzi na mjasiriamali anayeishi Uingereza. Inadaiwa alifuatwa London na Mwakipesile na Mwang’onda kuombwa agombee ubunge Kyela. Mwakalinga alifika Kyela Agosti mwaka huu na kuendesha kampeni ya kujinadi kwa mwezi mzima.

“Alifanya karamu kubwa kijijini kwao Katumba, Songwe, kwa kuchinja ng’ombe, kuwatangazia wananchi kuwa anaingia vitani. Alitembelea kata zote na kutoa misaada ya mabati na sementi.

Taarifa kuwa aligawa fedha kuanzia Sh. 10,000 hadi 100,000 kwa viongozi wa CCM wa vijiji na kata, hazikuweza kuthibitishwa ingawa Edson Matai wa Kasumulu, mpakani na Malawi anadai anajua hili kuwa ni kweli.

Kwa mujibu wa ndugu zake wanaoendesha biashara kwenye jengo la Kyela Development Corporation (KDC) mjini Kyela, Mwakalinga alirejea London Septemba mwaka huu na hadi leo hajarudi Kyela. Aliacha nyuma “kamati ya kampeni” inayodaiwa kuratibiwa na Mwakipesile.

Hunter Mwakifuna ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) wa Wilaya, ambaye vilevile ni daktari mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Ipinda.

Mwakifuna anaandamwa na tuhuma za kushusha umri wake kutoka miaka 35 hadi 28 ili kugombea nafasi hiyo ya vijana. Analalamikiwa pia na wakazi wa Kata ya Ipinda kuwa anatumia muda mwingi kufanya siasa kuliko kazi yake.

Elias Mwanjala, ni mfanyabiashara maarufu anayeishi Dar es Salaam na ni mpwa wa Dk. Mwakyembe, ambaye inadaiwa ameungana na kundi linalomwandama mjomba wake. Haijafahamika ni kwa mapatano gani.

Mwanjala hakupatikana kuzungumzia hilo, bali inadaiwa ameachana na biashara ya malori ya uchukuzi na kwamba hivi sasa anaendesha baa iitwayo Stereo, Kinondoni, Dar es Salaam na anaagiza matairi ya magari kutoka Dubai.

Uchunguzi wa gazeti umethibitisha kuwa Mwakipesile anatumia muda mwingi wilayani Kyela kuliko kituo chake kikuu cha kazi mjini Mbeya.

Taarifa zinasema Mwakipesile amekuwa akifanya mikutano nyumbani kwake na hata kwa marafiki zake wakubwa wawili waliotajwa kwa majina ya Glaswel Mwakalulwa wa kijiji cha Talatala na Mahamudu Silwamba wa kijiji cha Isaki.

Baadhi ya watumishi wa serikali wilayani Kyela wanamtetea Mwakipesile kuwa pamoja na safari zake Kyela kuwa nyingi, bado huko ndiko nyumbani kwa wazazi wake na baadhi ya safari ni za “kiserikali,” ingawa wanashindwa kueleza iweje kila ziara ya kikazi iwe ya kumpiga vijembe mbunge Mwakyembe.

Madai makuu ya Mwakipesile dhidi ya Dk. Mwakyembe ni kuwa mbunge huyo ni mgomvi na kwamba hakumtendea haki aliyekuwa waziri mkuu aliyeachia ngazi, Edward Lowassa, katika kashfa ya Richmond.

Inadaiwa kuwa Lowassa ni rafiki wa karibu wa Mwakipesile, ambaye inaaminika alifanya kazi kubwa kumshawishi Rais Kikwete kumpa wadhifa huo wa mkoa wa Mbeya.

Madiwani wa Kyela wanaodaiwa kuwa mstari wa mbele kumnadi Mwakipesile na “vijana” wake ni Christopher Mullemwa wa Ipinda, Zuhura Omari wa Viti Maalum, Frida Mwampiki wa Matema, Viski Mahenge wa Kyela, Edimasta Mwakibinga wa Ikama, Solomon Mwangalaba wa Ipande, I. Mwaipaja wa Lusungo na Watson Majuni wa Kajunjumele.

Magazeti wanayogawa ni yale yanayobeba ujumbe kuwa Mwakyembe hafai kwa vile amegombana na viongozi wenzake, akina Rostam, Lowassa, Karamagi na Mwakipesile na kwamba “Rais Kikwete hamtaki,” anadai Godwin Mwaipopo wa Ipinda, ambaye alidai kuhudhuria baadhi ya mikutano yao.

Msaidizi wa mbunge wa Kyela, Emmanuel Kiketelo Mwamlinge, amepuuzia madai hayo na kusema yanatokana na uelewa mdogo wa taratibu za bunge kwani maamuzi juu ya Richmond hayakuwa ya Dk. Mwakyembe bali ya bunge.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: