Uchafuzi Ziwa Viktoria watishia maisha


Meddy Mulisa's picture

Na Meddy Mulisa - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version

AFYA za mamilioni ya wakazi wa Bonde la Ziwa Viktoria ziko hatarini kutokana na ongezeko la uchafuzi wa maji ya ziwa hilo unaoandamana na uvuvi haramu wa kutumia sumu.

Uchuguzi uliofanywa kwa miezi minne katika mialo mbalimbali umebaini kuwa  kuna ongezeko kubwa la uchafuzi wa Ziwa Viktoria hali ambayo inatishia usalama wa afya za binadamu, wanyama pamoja na viumbe hai wengine wanaolitegemea ziwa hilo pamoja na mimea na wanyama.

Bonde la Ziwa Viktoria lina wakazi wapatao milioni 40 katika nchi tatu zinazounda Bonde hilo ikiwemo Tanzania, Kenya na Uganda. Nchi nyingine zinazotegemea Bonde hilo ni Rwanda na Burundi.

Tanzania pia ni mwanachama wa Bonde la Nile lenye nchi tisa – Kenya, Ethiopia, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Misri, Uganda, Sudan  na Burundi.

Ziwa hili lina umuhimu mkubwa katika ustawi wa nchi wanachama wa bonde hilo. Ziwa Viktoria ndilo kubwa zaidi kuliko maziwa yote barani Afrika na ni la pili duniani baada ya Ziwa Superior la Canada.

Ziwa Viktoria linamilikiwa kwa pamoja na nchi tatu ambapo Uganda inamiliki asilimia 43, Tanzania asilimia 51 na Kenya asilimia sita.

Hata hivyo, bonde hilo liko hatarini kutokana na uvuvi haramu, shughuli za kilimo na ufugaji pamoja na uchafuzi wa taka za viwandani.

Jiji la Mwanza pekee linaripotiwa kuzalisha jumla ya lita milioni 65 za taka kila siku ambazo hutiririkia ziwani humo.

Taasisi ya Utafiti Tanzania (TAFIRI) imeripoti kuwa kutokana na uvuvi haramu, samaki aina ya sangara katika Ziwa Viktoria wamepungua kutoka tani 790,000 mwaka 2006 hadi tani 227,365 mwezi Agosti 2008.

Utafiti huo umebaini kuwa sangara wanaovuliwa wanakuwa chini ya kiwango kinachotakiwa kuvuliwa ambacho ni urefu wa kati ya sentimita 50 na 85. Kiwango kinachovuliwa sasa ni sentimita 25 hadi 40.

Kushuka huko kwa idadi ya sangara kumesababisha viwanda kumi vya kusindika minofu nchini Tanzania, Kenya na Uganda kufungwa wakati viwanda vingine 25 vinazalisha kati ya wastani wa asilimia 30 na 40 tu.

Kanda ya Ziwa pekee nchini Tanzania ina viwanda 10 vinavyochakata samaki chini ya tani 400 kwa siku; wakati uwezo wake ni tani 800 kwa siku.

Sekta ya uvuvi nchini Tanzania huchangia asilimia 1.6 ya Pato la Taifa wakati asilimia 90 ya mchango huo unatoka Ziwa Victoria.

Mwaka 2007 Tanzania ilizalisha jumla ya tani 575,339 za samaki ambapo tani 57,000 zenye thamani ya Sh. 224 bilioni ziliuzwa nje. Kati ya mauzo hayo, Ziwa Vikctoria lilichangia Sh. 198 bilioni (sawa na asilimia 88.4).

Nchi za Afrika Mashariki hupata hasara ya dola milioni 310 kila mwaka kutokana na uvuvi haramu.

Sasa kutokana na unyeti wa tatizo hilo, nchi hizo zimekubaliana kuendesha operesheni maalum kukamata zana zote zinazotumika katika uvuvi haramu katika Ziwa Viktoria.

Katika kikao cha mawaziri wa nchi hizo kilichofanyika hivi karibuni mjini Jinja, nchini Uganda, ilikubaliwa kuwa tarehe 31 Desemba 2011 uwe mwisho wa matumizi ya nyavu haramu katika ziwa hili.

Katika makubaliano yaliyopitishwa na mawaziri hao, nyavu zinazoruhusiwa kuvua sangara ni aina ya “makira,”  zenye inchi tano hadi saba, wakati dagaa ni nyavu za milimita 10.

Kadhalika, wanaonunua sangara kwa kutumia vipimo vya 'long size' kipimo kilichoruhusiwa ni inchi nne hadi tisa.

Kadhalika, umbali unaoruhusiwa kuvua ni kilomita mbili kutoka kwenye ufukwe. Juhudi hizo zinalenga kuhifadhi mazalia na makulio ya samaki hasa aina ya sangara, sato na furu.

Ilikubaliwa pia kuwa utoaji leseni za uvuvi katika Ziwa Viktoria katika nchi hizi tatu uzingatie sensa ya uvuvi ya mwaka 2006 ambayo inazingatia na kudhibiti wingi wa uvuaji katika ziwa hilo.

Hata hivyo, ziwa linakabiliwa na changamoto nyingi zikiwa ni pamoja na magendo ya samaki miongoni mwa nchi zinazochangia Ziwa Viktoria.

Nyingine ni wamiliki wa viwanda vya kusindika minofu ya samaki kuendelea kuvuna samaki wachanga; vikundi vya ulinzi na rasilimali za ziwa (BMUs) kutokuwa na zana za kisasa kuweza kukabiliana na uharamia wa uvuvi haramu na kuwepo kwa njia nyingi za panya katika mialo isiyo rasmi.

0
No votes yet