Uchaguzi na ‘mbayuwayu’ wa JK


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 11 August 2010

Printer-friendly version

RAIS Jakaya Kikwete aliwahi kutamka waziwazi kuwa kama shinikizo la wafanyakazi kupandishwa mishahara limesukumwa na mazingira kuwa atagombea urais mwaka huu, basi hataki kura zao.

Je, wafanyakazi nao, ambao kwa mujibu wa rais wapo 350,000, waseme kuwa hawataki kumpa kura zao?

Rais alitoa kauli ya kukataa kura za wafanyakazi wakati alipoongea na wanaoitwa, “wazee wa mkoa wa Dar es Salaam” baada ya Shirikisho huru la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kutangaza mgomo nchi nzima kuanzia 15 Mei 2010.

Alisema serikali yake haiko tayari kulipa kima cha chini cha mshahara cha Sh. 315,000 kilichokuwa kikidaiwa na TUCTA.

Alitishia wafanyakazi kuwa iwapo wakigoma wasishangae polisi wakatumia nguvu na wengine kutiwa ngeu.

Aidha, inaonyesha ni jinsi gani waziri mwenye dhamana ya masuala ya kazi, Profesa Juma Kapuya alivyoshindwa, ama kumshauri vizuri bosi wake, au alivyompotosha, kwani sula la migomo kazini lipo kisheria na TUCTA ilikuwa katika utaratibu unaotakiwa.

Vilevile, inaonyesha washauri wa rais ndani ya serikali na katika chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM) walivyoshindwa kumpa ushauri sitahiki.

Kususa kura za wafanyakazi kipindi cha kuelekea uchaguzi ni sawa na watu wanaojilipua kwa mabomu ili wapate haki zao.

Sasa tunajiuliza kama Kikwete alikataa kura za wafanyakazi, muda wa kampeni ndiyo umefika. Je, atatembea tena nchi nzima kuomba kura za wafanyakazi?

Je, atawaambia nini wafanyakazi ambao ni majuzi tu aliwaambia kuwa hahitaji kura zao?

Je, atawaahidi nini ikiwa alishasema kuwa hawezi kuongeza kima cha chini hata kama wafanyakazi hao watagoma kwa miaka minane?

Hii ina maana kuwa hata akichaguliwa hataongeza mishahara ya kima cha chini mpaka aondoke madarakani.

Hata kama aliyoyasema ni kweli kuwa uchumi hauruhusu, ingawa kila mtu anajua uchumi wetu unaweza kulipa kima cha chini cha zaidi ya hiyo, basi angetumia lugha muwafaka na isiyo ya vitisho.

Je, Kikwete na CCM wametufundisha nini katika utawala wa Tanzania? Maanake kama mwenyekiti wa CCM amekataa kura za wafanyakazi, ina maana chama kwa ujumla kinakubaliana naye.

Si Makamu Mwenyekiti wa CCM Pius Msekwa au Yusufu Makamba, katibu mkuu, aliyesimama na kukanusha au kusema labda mwenyekiti aliteleza.

Hiyo ni katika chama. Lakini rais alikuwa akiongea katika nafasi yake ya mkuu wa nchi. Hakuna mtu kutoka serikalini ambaye alisahihisha kauli hiyo. Kwa msingi huo, hiyo ndiyo tabia ya chama na serikali yake.

Rais Kikwete aliwaambia wafanyakazi wasikilize ushauri na wachanganye na akili zao “kama mbayuwayu.”

Sasa wafanyakazi wamesikiliza ushauri wa rais, kuwa hataki kura zao. Wametumia akili zao na kuchanganya kama mbayuwayu. Je, sasa kura zao wazipeleke wapi?

Wazipeleke kwa aliyewashauri kuwa hazitaki au waangalie pembeni na kutafuta anayezihitaji zaidi na anayeweza kuzitumia kuwaondoa katika janga walilomo?

Ushauri wa rais wa kuchanganya akili “kama mbayuwayu,” yawezekana unatumika kwa wafanyakazi peke yao.

Je, wabunge wanapodai nyongeza kwa mishahara yao, nao waweza kuambiwa kuchanganya akili kama mbayuwayu?

Bali hili la kukataa kura za wafanyakazi lina sura nyingine. Ni ubaguzi. Kwa nini rais atake kura kutoka kwa wengine lakini akatae zile za wafanyakazi?

Kama rais hataki kura za wafanyakazi, yeye na chama chake wana mpango gani wa kupata kura za kuziba pengo?

0
No votes yet