Uchaguzi Ufaransa watikisa uchumi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 09 May 2012

Printer-friendly version

WANANCHI wa Ufaransa wamemchagua Mjamaa, Francois Hollande kuwa rais wa nchi hiyo, katika ushindi unaotarajiwa kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa Ulaya unaoyumba, vita vya Afganistan na diplomasia ya dunia kwa ujumla.

Hollande ambaye hakuwa anafahamika nje ya mipaka ya Ufaransa, amemshinda mtangulizi wake, Rais Nicolas Sarkozy. Rais Sarkozy amechukiwa na wananchi wa nchi hiyo kutokana na sera zake za kichumi.

Holande amebadili mwelekeo wa mjadala wa mataifa 17 yanayoshirikiana kiuchumi barani Ulaya.

Hadi sasa, Ufaransa na Ujerumani, zikiongozwa na Sarkozy na Angela Merkel, wameweka mkakati wa namna ya kurekebisha uchumi ulioparaganyika. Mkakati wao unalenga kupunguza matumizi ili kukwepa madeni na kuongeza masoko ya bidhaa zao.

Lakini suluhisho la Hollande limelenga katika serikali kutoa fedha kufidia biashara zilizoanguka ili kukuza uchumi wan chi hiyo.

Kwa upande wa diplomasia, Hollande hafahamiki, lakini ameahidi kuandaa mpango wa miaka mitano kwa nchi hiyo yenye silaha za nyuklia, lakini ikiwa na kiti cha kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Sarkozy ndiye rais wa Ufaransa ambaye ni kipenzi zaidi cha Marekani katika miaka 50 iliyopita. Ameshirikiana na nchi hiyo kuweka msimamo dhidi ya Iran na Syria, na katika kupeleka majeshi Afghanistan. Pia ametoa mchango kwa majeshi ya NATO katika harakati za kumwangusha Moammar Gadhafi wa Libya.

Lakini Hollande anataka kurejesha nyumbani majeshi ya Ufaransa kutoka haraka Afghanstan, na hatakuwa kiongozi wa kutumia mabavu nje ya nchi yake.

Hollande anataka matajiri walipe asilimia 75 ya kodi ya mapato na anakusudia kuongeza kodi za kampuni ambazo hutoa gawio la faida kwa wanahisa, badala ya kuwekeza katika biashara zao.

Sarkozy alikuwa ameahidi kupunguza mzigo wa kodi kwa wananchi. Kodi hizo ziko juu zaidi barani Ulaya. Pia aliahidi ongezeko la kodi ya mauzo.

Kuhusu uhamiaji, Sarkozy alitoa ahadi ya kupunguza nusu ya wahamiaji haramu wanaoingia Ufaransa hadi kufikia 100,000 na kuongeza udhibiti mipakani; lakini; Hollande angetoa uraia kwa wahamiaji haramu kwa kuzingatia mazingira ya kila mhusika.

Mjadala wa uhamiaji ulipata nguvu zaidi kuhusu mila za kiislamu katika nchi hiyo isiyo ya kidini, ikiwa na waislamu wapata milioni 5.

Hollande (57) alishinda uchaguzi wa marudio kwa asilimia 51 ya kura huku mpinzani wake ambaye wanayelingana umri, Rais Sarkozy akiambulia asilimia 48.1.

Hollande pia alimshinda Sarkozy katika uchaguzi wa awali wiki mbili zilizopita, lakini hakutangazwa mshindi kwa kuwa hakupata zaidi ya nusu ya kura zinazotakiwa kwa sheria ya Ufaransa.

Ilibidi uchaguzi huo kurejea baina ya wagombea wawili waliotangulia, ndipo Hollande akaibuka mshindi.

Uchaguzi huo unamaanisha kuwa Ufaransa kwa mara ya kwanza imepata rais mjamaa baada ya Francois Mitterrand aliyeongoza nchi hiyo kati ya mwaka 1981 hadi 1995.

Kumwondoa Sarkozy Ikulu ina maana kwamba wananchi wa nchi hiyo wamekataa mgogoro wa uchumi unaoisumbua Ulaya kwa sasa.

Muda mufupi baada ya televisheni za nchi hiyo kutangaza matokeo hayo, Rais Sarkozy aliwaeleza wafuasi wake kuwa amempigia mpinzani wake simu na kumpongeza.

“Ninawajibika kwa kupoteza kiti hiki. Niko tayari kuwa mtu wa kawaida miongoni mwa Wafaransa, na zaidi ya yote nina mapenzi ya dhati kwa nchi yangu,’ amesema Sarkozy.

0
No votes yet