Uchaguzi utapita, nchi itabaki


Ezekiel Kamwaga's picture

Na Ezekiel Kamwaga - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Waraka wa Wiki

HADI miaka miwili iliyopita, Kenya ilikuwa imefaidi amani na utulivu kwa zaidi ya miaka 40 tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Uingereza mwaka 1963.

Kitu kilichokuja kuharibu amani na utulivu huo kilikuwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2007 uliotoa matokeo tata ya ushindi kwa Mwai Kibaki dhidi ya Raila Odinga.

Wengi wanakumbuka kilichotokea baada ya matokeo yale kutangazwa. Maelfu ya watu waliuawa kwa risasi za moto, mapanga na mashoka kutokana na matokeo ya uchaguzi huo.Kama usingekuwapo uchaguzi, mauaji hayo pengine yasingetokea.

Si Kenya tu, kila unapofanyika uchaguzi katika maeneo mengi duniani, usalama wa nchi huwa katika hali tete.

Ndiyo maana, ninaamini, Watanzania wanatakiwa kuwa makini mno katika kipindi hiki wanapoelekea kufanya uchaguzi wa nani atawaongoza kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais.

Katika nchi zilizojaaliwa amani, ni rahisi kwa watu kupuuza uwezekano wa kutokea fujo na mauaji katika nchi zao. Lakini, hili limeonekana kuwa ni jambo linalowezekana kila mahali.

Kuna mambo mengi ya msingi ambayo Watanzania wanatakiwa kuyaangalia ili kuepuka uchafuzi wa amani na uvunjifu wa umoja katika nchi yetu.

Hatua ya kwanza inaanza kwa serikali yenyewe. Kama kuna kitu ambacho serikali nyingi za Afrika na nchi nyingine zinazoendelea zimekuwa zikishindwa kufanya ni kutimiza haki; “Haki haipaswi kutendeka tu lakini inapaswa kuonekana kuwa imetendeka.”

Katika uchaguzi wowote, ni lazima ziwepo ishara kuwa kura za kila mmoja zinahesabiwa kwa usahihi na mshindi wa haki anatangazwa.

Nchini Kenya, vurugu zilitokea kwa sababu raia wengi waliamini aliyetangazwa mshindi hakuwa mshindi wa halali. Kama serikali itaruhusu hili mwaka huu, ni wazi milango ya vurugu itakuwa imefunguliwa.

Matukio ya kuhesabu na kupiga kura ni lazima yafanyike katika misingi yote ya uwazi. Mambo kufanyika kwa kificho na kuzuia watu wasipige kura kwa namna yoyote ile, hakutasaidia amani na umoja wa nchi yetu.

Ni muhimu watu wahamasishwe kupiga kura, lakini ni muhimu pia kuhakikisha kuwa kila aliyejitokeza kupiga kura anaruhusiwa kupiga kura na kura yake inahesabiwa.

Kama ningekuwa na mamlaka ndani ya nchi yetu, ningewaomba wagombea wakuu wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu kujitokeza hadharani na kutangaza ya kuwa wako tayari kukubali matokeo ya aina yoyote ya uchaguzi.

Sharti lao kuu liwe kwamba uchaguzi wenyewe uwe kweli huru na wa haki. Kama wananchi wakiwasikia viongozi na wagombea wakisisitiza umuhimu wa kukubali matokeo, itakuwa rahisi kwao kuyapokea na kuyakubali.

Hii ndiyo kazi kubwa zaidi ambayo serikali iliyopo madarakani sasa inatakiwa kuifanya. Hii ni kazi ambayo serikali kama ya Ghana, katika bara hili hili la Afrika, imeweza kuifanya vizuri.

Baada ya hapo, unakuja wajibu wa vyama vinavyoshindana kushiriki katika aina ya siasa ambazo haziwagawi wafuasi wao bali zinawaunganisha.

Hapa ndipo unapokuja umuhimu wa viongozi kuacha aina ya siasa zinazoweza kuwagawa watu katika misingi ya udini, ukabila na itikadi za vyama. Watumie kauli njema.

Katika wiki hii ya mwisho kabla ya uchaguzi, joto la kisiasa linakuwa limepanda sana na ni muhimu kwa wagombea na vyama vyao kujaribu kuliteremsha ili lisigeuke kuwa jazba na chuki.

Kauli za uchochezi, uzushi na matusi hazitakiwi kupewa nafasi kwa namna yoyote ile. Huu ni wakati ambapo wagombea wanatakiwa kumwagia mbolea yale ambayo wananchi wameanza kuyaelewa kutoka kwao.

Kundi la mwisho ambalo ni muhimu sana kuligusia leo ni lile la wananchi. Na hapa nitagusia sana kuhusu matumizi ya simu za mkononi.

Kama kuna kitu ambacho kilisababisha kuenea kwa mauaji nchini Kenya ni matumizi ya simu za mkononi kupitia njia ya ujumbe mfupi wa maneno.

Kupitia simu za mkononi, watu walikuwa wakitumiana meseji kuelezana namna ya kuua na wapi walipo watu wa kuwaua. Zilikuwapo pia meseji nyingi kuhusu nani hasa amefanya nini, na mara nyingi zote zilikuwa za uchochezi.

Ni muhimu kwa wananchi kufikiri mara mbili kabla ya kutuma meseji isije ikachangia uvunjifu wa amani na umoja.

Simu moja, ya bei nafuu au ghali, inaweza kusababisha taifa zima likaelekea shimoni. Kila mtu ana simu yake lakini ni heri wale wenye nazo wakafahamu umuhimu wa amani na umoja.

Na hili ni eneo ambalo tayari watu wengi wameanza kuona athari zake. Katika wakati huu wa kampeni, wengi wamejikuta wakitumiwa meseji mbalimbali, mbaya na nzuri na watu ambao hata hawawafahamu.

Vyombo vya dola ni lazima vijiwezeshe kufahamu ni wapi na nani anasambaza meseji hizi mbaya. Katika wakati ambapo tayari athari za matumizi ya meseji yamejulikana, ni muhimu vyombo vya usalama vikawa tayari kukabili hili.

Vyombo vya dola vitimize wajibu wake. Wananchi nao wawe wa kwanza kujiuliza kabla hawajatuma meseji ili isiwe ile ambayo inaweza kuleta taharuki kwa taifa.

Jambo la muhimu kuliko yote ni kwa wananchi kufahamu ya kuwa uchaguzi; japo ni muhimu kwa mustakabali wa taifa, ni jambo la kupita tu lakini nchi ni jambo la kudumu.

Wakati tukielekea kupiga kura Jumapili ijayo, ni vema; serikali, wananchi na vyama vya siasa wakafahamu wajibu wao katika kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa kitu kimoja baada ya Oktoba 31 mwaka huu.

Kila la kheri kwa wananchi na wagombea wa vyama vyote vilivyojitokeza kushindana katika uchaguzi wa mwaka huu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: