Uchaguzi UV-CCM waingia dosari


Siame Baramia's picture

Na Siame Baramia - Imechapwa 01 July 2008

Printer-friendly version

UCHAGUZI mkuu ndani ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UV-CCM) umeanza kuingia dosari kutokana na kubainika kuwa baadhi ya wagombea wametoa taarifa za uwongo kuhusu umri wao wakitarajia 'kutetewa na viongozi ngazi ya taifa.'

Dosari hizo zimegundulika katika mkoa wa Pwani miongoni mwa wagombea nafasi ya Mwenyekiti ngazi ya Mkoa. Wanachama wapatao watano wanawania nafasi hiyo.

Kanuni ya UV-CCM ya mwaka 2008 inasema, anayegombea uongozi sharti awe na umri ambao, wakati wa utumishi wake na hadi mwisho wa kipindi chake cha uongozi, hatakuwa amevuka miaka 35.

Hata hivyo, kuna taarifa kuwa mmoja wa wagombea 'anatarajia uongozi wa juu wa UV-CCM utabadili kipengele hicho cha umri ili kumpa upendeleo maalum' wa kugombea, licha ya kuwa na umri mkubwa. Haikufahamika nani anampa faraja, ujasiri na matumaini hayo.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa UV-CCM Pwani, Hassan Abdallah Daudi Kulwa, ambaye pia ni mgombea, aliiambia MwanaHALISI kwa njia ya simu kuwa tayari wamebaini 'kitu kama hicho' – umri mkubwa – na kwamba 'tutayadhibiti kwa kutumia kanuni.'

Aidha, amesema kuna hata wanaotaka kugombea nafasi za Pwani wakati wao wanaishi Dar es Salaam. 'Hawa wametumwa. Tutawaripoti kunakohusika katika vyombo vya ngazi ya juu,' alisema.

Ibara ya 17(f) ya kanuni hizo katika toleo la 8 la mwaka 2008 ndiyo dira maalum ya umri wa wagombea wote katika kukabiliana na uwezekano wa umoja huo kuongozwa na wenye umri unaokinzana na ujana.

Kwa mujibu wa ibara hiyo na kwa mujibu wa taarifa za kuaminika, walioomba kugombea wana umri mkubwa kuliko ule walioonyesha kwenye fomu zao za kugombea.

Naye Katibu wa UV-CCM Pwani, Ernest Makunga, alipoulizwa juu ya waliozidi umri wa kugombea alisema, 'Tunajua wapo ambao wanaweza kudanganya. Hili likitokea tutapeleka ngazi za juu za chama.'

Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa la Vijana, Mtanda Mohammed Said, aliiambia MwanaHALISI kwa simu kuwa suala la umri halina utata na kwamba 'Kanuni iko wazi.'

Mmoja wa waomba nafasi hiyo amenukuliwa akisema kuwa iwapo mwenzake, ambaye anajua fika kuwa ana umri mkubwa, atateuliwa kugombea, basi yeye atazua 'kasheshe' ili akubaliwe kugombea.

Kwenye fomu zao za sasa, waombaji wameonyesha kuwa na umri wa miaka 30 au chini yake. Lakini ni umri huohuo waliuonyesha mwaka 2003, miaka sita iliyopita, walipokuwa wanasaka nafasi katika umoja huo.

Gazeti hili lina taarifa zao binafsi kama walivyozitoa mwaka 2003.

'Hapa itabidi uongozi wa umoja wetu uthibitishe kuwa umri wao haujaongezeka au siyo walewale waliogombea uongozi mwaka 2003,' ameeleza kiongozi mmoja wa UV-CCM, wilayani Kibaha.

Taarifa zilizozagaa mjini hapa zinasema iwapo mmoja wao, au hata wengine kwa ngazi tofauti, wataruhusiwa kugombea, hiyo itakuwa hatua ya uongozi wa kitaifa kuzika UV-CCM mkoani Pwani.

Aidha, kifungu kidogo cha 'c' cha Ibara 17 kinasema kiongozi sharti awe 'mwadilifu, mkweli na mwaminifu kwa Umoja wa Vijana, CCM na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.'

'Uko wapi sasa uadilifu, ukweli na uaminifu wakati wanaotaka kugombea tayari wanaanza kwa kutosema ukweli juu ya jambo dogo kama umri?' ameuliza mmoja wa viongozi wa UV-CCM wilayani hapa.

Nafasi ambayo inagombewa na wanaodaiwa kukiuka kanuni ni muhimu mno kichama. Ni mwenyekiti anayepaswa kuwa msimamizi wa kanuni na hata kujadili wanachama wengine wanaotaka kuingia katika uongozi.

Mchakato wa uchaguzi ndani ya UV-CCM unaonyesha kuwa juzi Jumatatu, 30 Juni, ndiyo ilikuwa siku ya mwisho ya kurudisha fomu za wagombea uongozi ngazi ya mkoa.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: