Uchaguzi UWT: Kambi za 2005 hazijavunjwa


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 23 September 2008

Printer-friendly version
Mwenyekiti wa UWT, Sophia Simba

INAWEZEKANA RAIS Jakaya Kikwete amevunja kambi yake ya wakati wa uchaguzi mwaka 2005, lakini ameivunjia rohoni mwake.

Inasadikika ni rohoni mwake kwa kuwa wale waliokuwa wapambe wake wanaonekana kuwa bado wana donge la mwaka 2005.

Kwani kila uchwao vitimbi vinavyotokana na kinyang’anyiro cha ugombeaji uteuzi ndani ya CCM mwaka 2005 vinaendelea kuibuka.

Wakati waliokuwa wapinzani wa Kikwete katika kinyang’anyiro hicho na wapambe wao wakiendelea kusakamwa, washirika wake wanalindwa kwa gharama kubwa huku hoja ya “huyu ni mwenzetu” ikijengwa wazi.

Tayari baadhi ya wananchi wameanza kuhoji: Iwapi kauli ya Kikwete ya kumaliza makundi ya uchaguzi ndani na nje ya chama chake?

Je, kauli yake kwamba uchaguzi umemalizika na sasa wananchi washughulikie harakati za kutafuta maendeleo ilikuwa na maana gani? Je, ilitolewa kwa dhati kweli?

Ni muhimu kujadili hili kutokana na yanayotendeka sasa ndani ya CCM na jumuiya zake kwa ujumla.

Ijumaa iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Wanawake (UWT-CCM) lilipendekeza kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kupitisha majina ya wanachama watatu kuwania nafasi ya mwenyekiti.

Waliopitishwa ni Janeth Kahama, Sophia Simba na Joyce Masunga. Kahama amepewa alama A, Simba na Masunga wamepewa alama B kila mmoja.

Wagombea wengine wawili, Dk. Odija Rujaji na Zerulia Maneno wamepewa alama C wakati Halima Mamuya, ambaye aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa UWT, amepewa alama E.

Kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi ndani ya CCM, mgombea anayepewa alama E, hastahili kupitishwa kuwania nafasi anayoipigania.

Inawezekana Kahama hakuwa mwanamtandao moja kwa moja, lakini ni wazi kwamba yeye hakuwa tishio kwa mtandao wa Kikwete.

Sophia Simba anafahamika. Huyu alikuwa mfuasi wa karibu wa mtandao. Awali aligombea ubunge katika jimbo la Ilala, lakini hakufanikiwa kupenya.

Baada ya kushindwa katika kura za maoni za ubunge wa Ilala, Simba akaibukia kusaka ubunge wa viti maalum, ambako nako aliangukia pua.

Hatimaye akapata ngekewa. Akateuliwa na rais kuwa mbunge kupitia nafasi 10 ambazo rais anapewa na katiba; hatimaye akaukwaa uwaziri. Hakika, ilikuwa ngekewa juu ya ngekewa au ukitaka, mpangilio mwanana.

Masunga anajulikana. Ni mwanamtandao asio na shaka. Amekuwa mfuasi wa mtandao tangu mwaka 1995.  

Mkutano wa UWT umefanyika wiki mbili baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana (UV-CCM) kupitisha majina ya wagombea wake wa uenyekiti.

Kama ilivyokuwa kwa Baraza Kuu la UWT, Kamati ya Utekelezaji ya UV-CCM, ilimpa Nape Nnauye alama E kabla ya Baraza Kuu kupitisha uamuzi wa kumfuta uanachama.

Hakuna mashaka kwamba Nape na Mamuya hawakuwa wanamtandao; na kwamba maamuzi yaliyochukuliwa dhidi yao yalitokana na kile kinachoweza kuitwa, “kulipiza kisasi.”

Madai kwamba Mamuya alishiriki kuangamiza UWT kutokana na kuingiza jumuiya hiyo katika “mkataba wa kinyonyaji,” hayana mantiki wala hoja za msingi.

Madai hayo yalitolewa kikaoni na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuph Makamba akieleza kuwa Mamuya alishiriki katika kufanikisha mkataba huo ambao Makamba aliita wa kinyonyaji. Huu ni mkataba wa uwekezaji kwenye kiwanja cha City Ambassador, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Mradi huo uliopo katika viwanja Na. 186158/45 na 24140 Kitalu 41, ni kati ya UWT na kampuni ya Manji Holdings Limited.

Ni Makamba aliyeshinikiza, mbele ya wajumbe, kuwa Mamuya ajiuzulu. Hakuishia hapo, alitoa maonyo na vitisho akisema, “Usipojiuzulu tutakuvua uanachama.”

Ni wajumbe walewale waliokutana 16 Agosti 2007 na kuelezwa na Makamba kuwa katibu wao amehujumu umoja wao, waliokutana Alhamisi iliyopita na kumpa Mamuya alama E.

Lakini kila mmoja anajua kwamba mkataba ambao Mamuya na wenzake waliingia, una manufaa makubwa ukilinganisha na ule wa UV-CCM ambao Makamba amejiapiza kuulinda “mpaka mwisho.”

Kwa mfano, UWT na kampuni ya Manji Holdings Limited hawakuingia ubia, bali UWT imekodisha kiwanja chake.

Kiwanja kilichokodishwa kitajengwa kitegauchumi cha ghorofa nane kwa thamani ya dola za Marekani 10 milioni (zaidi ya Sh. 10 bilioni).

Kampuni iliyokodishwa watalipa kwa UWT gharama ya pango la dola za Marekani 200,000 kila mwezi.

Lakini pia tofauti na mkataba wa UV-CCM, kitegauchumi cha UWT kitakachojengwa, yatakuwa makao makuu ya kampuni ya simu za mkononi ya Celtel (sasa Zain), kanda ya Afrika Mashariki.

Aidha, mkataba huu si wa milele na milele kama ulivyo ule wa kinyonyaji wa UV-CCM ambao Makamba ameamua “kufa nao.” Mkataba wa UWT utadumu kwa miaka 33 na katika muda wote, jengo litakalojengwa litakuwa mali ya UWT.

Hii ina maana kwamba kilichokubaliwa na washirika hawa wawili, ni mkataba wa upangishaji si vinginevyo.

Lakini ukiacha yote hayo, Baraza la Wadhanini chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba, hata mara moja, halijakana mkataba wa Mamuya na wenzake.

Tofauti na mkataba wa Edward Lowassa, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la UV-CCM, ambao wajumbe wote wamekana mwenyekiti wao, mkataba wa UWT umepata baraka zote za wajumbe wa Baraza la Wadhamini.

Hata vikao vya Baraza Kuu na Kamati ya Utekelezaji vya UWT, havikuwahi kukana mkataba, badala yake vyombo vya habari vilimnukuu, si mara moja wala mbili, Anna Abdallah akitoa taarifa ya kuwapo kwa mkataba huo na hatua zinazoendelea kuchukuliwa na vikao husika.

Kutokana na hali hiyo, watu makini lazima wajiulize, Mamuya amekosa nini kustahili alama E. Amemkosea nani? Jibu ni moja. Hakuwa mwanamtandao. Alikuwa mfuasi wa karibu wa Dk. Salim Ahmed Salim. Hiyo ndiyo dhambi inayomhukumu sasa.

Ni kutokana na ukweli huo, Sophia Simba na Janeth Kahama ambao “wamevuana nguo hadharani,” bado wanalindwa kwa kupendekezwa kugombea nafasi ya mwenyekiti UWT.

Hatua ya kutokomeza wapinzani wa Kikwete ndani ya chama haikuanza leo. Orodha ya wanachama ambao hawakumuunga mkono Kikwete ambao walishughulikiwa kikamilifu ni ndefu, ingawa wengine walifanikiwa kupenya.

Kwa mfano, George Mkuchika, alisukiwa zengwe ili asiwe Katibu wa Wabunge wa CCM.

Kilichomuokoa Mkuchika hadi akafanikiwa kuwa Naibu Katibu Mkuu ni msimamo wake usioyumba ambao hata Kikwete anautambua.

Profesa Mark Mwandosya: Huyu alisukiwa mipango mara kadhaa ya kumuangamiza kisiasa. Katika uchaguzi uliopita, alitajwa hadi kwenye kikao cha Kamati Kuu (CC).

Ni mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale-Mwiru aliyesema, “Mwandosya si mwenzetu.” Ilikuwa wakati wa kupitisha jina la mgombea uenyekiti wa CCM wilayani Rungwe.

Profesa Mwandosya ni mmoja wa wanachama 11 wa CCM waliowania urais katika uchaguzi wa mwaka 2005. 

Hata Dk. Abdallah Kigoda naye hayuko salama. Kila kukicha malalamiko mapya yanaongezeka kuwa anasukiwa njama za kumtokomeza. Kigoda kama ilivyokuwa Mwandosya, aligombea urais na Kikwete.

Tayari Mujuni Kataraia ametokomezwa. Huyu hakuwa mfuasi wa mtandao wa Kikwete lakini alitokomezwa kwa hoja ya “kutafuna fedha” za chama. Walioiba mabilioni Benki Kuu wameachwa kupeta.

Mwingine aliyetokomezwa ni Abiud Meregesi, mfuasi mkubwa wa Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye. Huyu, kama ilivyo kwa Kataraia, amedaiwa “kutafuna fedha” za chama.

Wakati Kataraia na Meregesi wakitolewa kafara, Kapteni John Komba, mwanachama wa kundi la mtandao, analindwa kwa hoja, “huyu ni mwenzetu.”

Komba anatuhumiwa kutafuna mamilioni ya shilingi za CCM ikiwa ni pamoja na kuficha nyaraka zinazohusu magari.
 
Hata Frank Uhahula, pamoja na kwamba amefanikiwa kubaki katika nafasi yake ya ukuu wa wilaya, wanamtandao walimshughulikia kikamilifu hadi akashindwa katika kinyang’anyiro cha ujumbe wa NEC.

Uhahula, mwanasiasa mwenye uwezo mkubwa wa kujenga hoja, alijikuta akipigwa mweleka na baadhi ya wanasiasa wachanga, kwa kile kilichoitwa, “safisha wasiotuunga mkono.”

Hawa ni mfano mdogo tu. Kuna wengi walioathirika kutokana na uamuzi wao wa kutounga mkono Kikwete. Inawezekana haya yanafanyika bila baraka za Kikwete. Lakini je, anapoyaona anachukua hatua gani?

Mifano yote hapo juu inaonyesha kuwa CCM inakwenda pabaya. Wanaomlaumu Makamba, kwa kauli zake na vitendo, hasa katika masuala mawili ya Nape na Mamuya, nao wana hoja nzito ambazo hawezi kuzikimbia kirahisi.

Je, mpaka sasa Makamba bado anaiva kweli na Kikwete? Juu ya kambi zinazoleta mgawanyiko ndani ya CCM? Kikwete anajua anachosubiri.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: