Uchaguzi wa CCM, si mwarobaini wa ufisadi


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 18 January 2012

Printer-friendly version

MWAKA 2012 umewadia. Ni mwaka wa uchaguzi wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kuna mengi yanasemwa kuhusu uchaguzi huu na kuwajengea matumaini bandia wengi wa wanachama wake.

Hata kama kwa kawaida uchaguzi huleta sura mpya na mambo mapya katika taasisi, ni ndoto kutumaini kuwa uchaguzi wa ndani wa chama hiki unaweza kufanya hivyo. Sababu ni nyingi, lakini mbili ni kubwa.

Kwanza, tumaini linalongojewa kwa hamu na wanachama wengi wa CCM, ni kuutumia uchaguzi huo kuondokana na viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi. Kwamba, kwa kuwa imeshindikana kuwafukuza au hata kuwakemea kwa majina yao, basi jitihada zifanyike ili wakigombea nafasi yoyote waenguliwe kupitia vikao vya mchujo.

Pili, kwa kuwa baadhi ya nafasi zilizokuwa zinagombea kwa ngazi ya taifa sasa zitagombewa ngazi ya wilaya, basi mafisadi hao wataenguliwa huko huko kwa sababu kwanza, labda si maarufu huko wilayani, na pili, watakosa nguvu ya kuingilia mchujo ngazi ya mikoa na taifa.

Dhana zote mbili zina mapungufu makubwa ya kiuongozi. Ni kama mwindaji anayelazimika kuvaa miwani ya mbao ili kumpiga nyani kwa hofu ya kuwa atamhurumia akimwangalia uso kwa uso.

Kimsingi, ili upambane na mafisadi inabidi uuchukie ufisadi. Ufisadi ndicho kiini na kiota ambamo mafisadi wanazaliwa na kukulia. Ni mfumo unaoendekezwa na taratibu za kuwapata viongozi bila kulazimika kuangalia maadili yao binafsi na historia zao.

Mfumo huo ukiachwa unaota mizizi na kuenea kila kona ya maisha ya watu. Hivi sasa, katika taifa letu ni vigumu sana kupata mahali ambapo hakuna rushwa wala ufisadi. Hata zile sehemu “takatifu zilizoheshimiwa” zinanuka rushwa.

Wingi wa fedha na ujanja wa kudanganya bila kukamatwa ni sifa muhimu ya kiongozi wa umma. Fitina na mizengwe ndizo kanuni za kuwapata viongozi; hali hii imeachwa ikawa sehemu ya kawaida ya maisha ya wanachama na viongozi wa chama hiki. Bila kulichukia hili na kuamua kwa dhati kuondokana nalo, ufisadi utaendelea kukitafuna chama hiki na taifa kwa jumla.

Wakati naandaa makala hiii nimewatembelea viongozi watatu wastaafu wa taifa letu. Kwa mshangao mkubwa nimewasikia wakijenga matumaini makubwa kuwa uchaguzi wa ndani ya chama utawaondoa watuhumiwa wa ufisadi.

Nilipowauliza ikiwa itashindikana kuwaengua katika mchujo nini kitatokea, haraka wamenijibu kuwa basi watachaguliwa na hiyo ina maana wananchi wanawapenda. Kwa maneno mengine, wastaafu wetu hawa wanaamini kuwa kuchaguliwa kwa kura nyingi ni ushahidi wa kuwa yule aliyechaguliwa ni kiongozi safi na anakubalika.

Nimeasikia baadhi ya wapambe wa mwenyekiti wa taifa wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, wakisema kamati za maadili zitahakikisha zinawaengua mafisadi wote. Nikawauliza: Ni wepi mafisadi watakaoenguliwa? Jibu walilonipa, “unawajua, subiri uje kuona.”

Hali hii pia anayo mwenyekiti Kikwete. Wakati wote wa mjadala ndani ya vikao vya chama chetu amekuwa mtu wa kumung’unya maneno bila kutaja wazi wazi kama na yeye anakerwa na ufisadi.

Ni mara chache sana wapambe wake wa karibu, ndiyo amewatumia kutuhumu na kueneza fitina dhidi ya anaowaita mafisadi. Matokeo ya kigugumizi cha Kikwete, ni kudorola kwa jitihada zote za kweli za kuondokana na ufisadi na mafisadi.

Pamoja na kwamba ni yeye anayeendesha kampeni kuwa mafisadi waenguliwe kupitia uchaguzi wa ndani wa CCM, lakini ukweli ni kwamba wakati wa mchujo ukiwadia atawapitisha kwa kisingizio cha kutaka wakakataliwe na wapigakura.

Jingine ambalo haliwezi kuondoa ufisadi, ni mfumo wa mtandao ulioenea hata nje ya chama chenyewe. Mtandao huu ulioasisiwa ndani ya chama na ukaenea nje yake, hata kama utauondoa ndani ya CCM, hakuna uhakika wa kuondokana na ufisadi.

Mathalani, ufisadi ulio katika vyombo vya utoaji haki kama mahakama, polisi, taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa (TAKUKURU), ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu wa serikali (DPP), mahakana na kwenye vyombo vingine vya utoaji huduma, hauwezi kuondolewa kwa kuwapo uchaguzi wa ndani ya CCM.

Kuna uwezekano hata wa jitihada za CCM kuondokana na ufisadi zikakwamishwa na ufisadi uliomo katika vyombo hivyo.

Aidha, uongozi wa sasa wa CCM na serikali yake ni tunda la ufisadi mpevu. Ni CCM hii hii iliyoasisi siasa chafu za kutumia fedha kununua uongozi, kutumia fedha kutandaza nyaya za mitandao ya kuchafuana na kununua wapigakura na hata wapigadebe.

Ni CCM hii hii na uongozi wake, iliyoasisi kebehi kwa viongozi waadilifu na hata kuwatisha ikiwa watadiriki kuhoji mbinu chafu za kujipatia uongozi wa njia ya fedha. Hivyo basi, uongozi wa sasa wa CCM hauwezi kupambana na ufisadi ulioasisiwa na viongozi waliopo. Badala yake, ufisadi huu unaweza kuuondoa uongozi huu madarakani.

Vilevile, ufisadi haukuingia ndani ya chama hiki kwa njia ya demokrasia, ili uweze kuondoka kwa njia ya sanduku la kuraa. Umeingia kwa hila na hivyo ni makosa kujaribu kuuondoa kwa njia ya demokrasia.

Kuweka matumaini kuwa uchaguzi wa ndani ya chama utumike kuondoa ufisadi, kunaweza kuwa ni kuitumia vibaya demokrasia. Historia ya tawala za dunia inaonyesha uovu hauondolewi kwa demokrasia. Bali pale uovu ulipokithiri na kuambukiza mihimili ya msingi ya kupinga uovu, wananchi husimama na kuuondoa ili kutafuta ahueni.

Pale ambapo uovu umekua lakini bado haujaishambulia mihimili mingine, demokrasia inaweza kutumika lakini kwa lengo la kubadili mfumo ili kuziba mianya inayolea huo uovu.

Ufisadi nchini ni ule wa aina ya kwanza, yaani uliokwishapevuka na kuishambulia mihimili mingine. Hii ni kwa sababu, unakuta fisadi mmoja au kundi lake, ana watu wake kila kona ya nchi na katika taasisi nyeti. Imefika mahali hata mkuu wa nchi hana uhakika kama watu wake wako naye au wako na mafisadi.

Akiagiza fisadi fulani achukuliwe hatua, wale wanaopaswa kumchukulia hatua anakuta ni watu wa fisadi yule na yeye kubaki kuishia kupewa visingizio lukuki vya utawala wa sheria. Mtandao huu wa ufisadi hauwezi kuondolewa kwenye enzi yake kwa kutumia demokrasia. 

Wiki iliyopita katika kipindi cha “kipima Joto” kinachorushwa na ITV, nilimsikia Nape Nnauye akiwahakikishia Watanzania kuwa CCM “itafanya kweli” kwa kuwaondoa mafisadi ndani ya chama. Kwamba hata baada ya kuwapa siku 90 wakagoma, mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ukakutana mara mbili, nako ikashindikana, bado yeye anaamini itawezekana kuwaondoa mafisadi!

Yaelekea hata yeye anajiunga na wale wanaohubiri kutumia uchaguzi wa ndani ya chama kuondokana na mafisadi. Kitu kimoja ambacho Nape hakuweza kutamka hadharani, ni ikiwa hiyo itashindikana kutokana na ukwasi wa fedha za mafisadi, nini itakuwa hatima ya CCM na yeye mwenyewe?

Kiini cha yote haya, ni kwamba CCM inawachukia mafisadi, lakini inataka fedha zao. Ndiyo maana dhamira ya kweli kuwaondoa mafisadi ndani ya chama haipo.

tutikondo@yahoo.com
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: