Uchonganishi Tarime hapana!


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 30 September 2008

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

WATANZANIA wilayani Tarime wanasubiri uchaguzi mdogo ili kujaza nafasi za wawakilishi wao katika udiwani na ubunge. Kifo cha Chacha Zakayo Wangwe, aliyekuwa na nafasi hizo, ndio chimbuko la uchaguzi huo.

Kwa hivyo, kwa sasa kunafanyika kampeni kwa vyama vilivyosimamisha wagombea. Wenzetu wamo katika wiki ya nne ambapo wananchi wamepata fursa ya kuwasikiliza viongozi wa vyama vilivyosimamisha wagombea.

Wananchi wanatakiwa wasikilize sera za vyama hivi au misimamo ya wagombea wao. Kwamba chama kitafanya nini na wagombea wake atafanya nini kwa ajili ya maendeleo ya wana Tarime. Hivyo ndivyo inavyotakiwa na ilivyotarajiwa kuwa.

Kwa bahati mbaya, sivyo inavyotokea. Tarime sasa kuna mfumuko wa kampeni za kuchafuana na zilizojaa vitisho na kauli za kubezana.

 Hali ni mbaya na ya kutisha tunapoona wingi wa askari Polisi na vyombo vingine vinavyosimamia ulinzi na usalama. Ukweli Tarime hawakutaka majeshi bali kampeni safi na uhuru wa kuchagua mgombea wanayemtaka itakapofika 12 Oktoba.

Inaonekana Tarime ni kama vile kuna hatua za kudhibiti au kuwekea mipaka watu katika kutumia uhuru wa kutembea, kusema na kujikusanya.

 Ni mtizamo huu wa kampeni chafu uliomtia matatani Mwenyekiti wa chama cha siasa cha Democratic Party (DP), Mchungaji Christopher Mtikila “alipopopolewa mawe” jukwaani wakati akinadi aliyemuita mgombea ubunge wa chama chake.

Tunaona namna kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Tarime zilivyoingiliwa. Hili ni hatari kama tuonavyo matukio ya vurugu na ghasia kwenda sambamba na kampeni hizi.

Tanzania ina miaka 16 tangu ilipokubali tena mfumo wa vyama vingi vya siasa. Sasa inasikitisha kuona kipindi chote hicho bado wapo wanasiasa hawajajifunza umuhimu wa kuendesha siasa za ustarabu.

Si rahisi kupata majibu ya kwanini taifa linapita hapo. Ila tunaweza kusema panahitajika tafakari jadidi ya mwelekeo wa siasa za Tanzania.

Si vema watu wakashuhudia vurugu unapokuja uchaguzi. Hii si njia nzuri ya kutafuta maisha bora wala kutafuta demokrasia ya kweli. Watanzania hawako tayari kuona damu yao au ile ya ndugu zao inamwagika kila baada ya uchaguzi.

Ni muhimu pia kuangalia upande mwingine, maana inaonyesha hali hii inachochewa kwa kusudi. Wapo wanasiasa wamechoka kufikiri na sasa wanaamini vurugu ndio njia nzuri ya kutimiza matakwa yao.

Watanzania wanataka siasa za kistaarabu zinazowaelekeza katika kushiriki harakati za kuondokana na umasikini na uchumi duni wa nchi yao. Wala hawataki wanasiasa wanaoamini kwamba Watanzania ni watu wa kupumbazwa kwa maneno na ahadi zisizotekelezeka.

Ripoti za karibuni hapa zimemuonesha Mchungaji Mtikila akituhumu waziwazi baadhi ya watu – tena wengine wenye umashuhuri mkubwa katika jamii – kwamba walihusika kumuua Wangwe.

Mchungaji Mtikila anajua fika kwamba kwenye Mahakama ipo kesi inayohusu tukio la kifo cha Wangwe kilichotokea katika kijiji cha Pandamili, wilayani Kongwa, mkoani Dodoma. Hili analijua, maana ana akili timamu.

Inakuaje anatuhumu watu hata kwenye jukwaa la kampeni ya uchaguzi mdogo huku vyombo vya ulinzi na usalama vikimuangalia?

Hivi haoni kwamba kufanya hivyo ni kuchochea vurugu na watu kuasi serikali yao? Anataka kupata manufaa gani kwa kusema Chadema kinahusika na mauwaji ya Wangwe?

Wakati tunaamini Wangwe amefariki dunia, hatuna nafasi ya kusikiliza eti mtu fulani amehusika. Angalau tungesikia haya kwenye mitaa lakini yakisemwa na kiongozi wa chama cha siasa kilichosajiliwa, inasumbua. Inaonyesha kwamba kiongozi anayetoa tuhuma hizo amefilisika kisiasa.

Hebu tuache hisia za namna hiyo. Mbona huu si wakati tena wa kuhamasisha watu kuamini tuhuma za chanzo cha kifo kile? Mbona sisi tunaona huu ni wakati wa kusahau na kugeukia vipi watu wa Tarime watatumikiwa?

Watu wa Tarime wanachotaka ni mtu wa mfano wa Wangwe. Mtu atakayechukua mawazo yao, mahitaji yao, matumaini yao na kuyakomaza kwa serikali ili kupatiwa ufumbuzi. Yale yanayohitaji kurekebishwa yarekebishwe.

Inatukera kuona kwamba Mchungaji Mtikila amerudia tuhuma za kifo hiki ndani ya mwezi mmoja. Hatujui kwanini anaziamini hata kuzitoa hadharani. Lakini tunajiuliza viko wapi vyombo vinavyohusika kudhibiti utoaji tuhuma kama huu? Au yeye ni mtu baki? Au wao ndiyo waliomtuma!

Hatuamini kama Mchungaji Mtikila kupanda kwenye jukwaa na kusema fulani amehusika na kifo cha Wangwe ndio anafanya kampeni ya uchaguzi? Kwamba hapo ndio ananadi wagombea wake, hatuamini. 

Lazima tutambue kifo kile kimeumiza watu wengi na wengine majeraha yangali mabichi. Kuwazidishia machungu si jambo zuri hata kidogo na wala huo si uungwana. Uungwana wa mtu ni vitendo vizuri si uchonganishi na maudhi.

Binafsi, ningefurahi iwapo mtindo huu utakoma mara moja. Si kwa Mchungaji Mtikila tu, bali mwanasiasa yeyote anayedhani ana haki ya kupoteza muda wa wananchi kipindi hiki.

Ipo haja kila Mtanzania kujiegemeza katika kutafuta uchumi imara wa familia yake na kuongeza mchango wake katika kukuza uchumi wa taifa lake. Haitasaidia kitu kumpumbaza kwa sababu mtu anataka kutimiza matakwa yake binafsi.

Tungependa wanasiasa wakajifunza kutokana na matukio ndani ya nchi. Watumie uzoefu unaopatikana kutokana nayo kuelekeza jamii penye neema badala ya gharika.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: