Uchumi Kagera waporomoka kwa kasi


Meddy Mulisa's picture

Na Meddy Mulisa - Imechapwa 18 May 2011

Printer-friendly version
Ndani ya Jamii

KWA miaka mitano mfululizo, tangu 2005, mkoa wa Kagera umekuwa miongoni mwa mikoa mitano inayoshika nafasi za mwisho kwenye kiashiria cha wastani wa kipato cha mwananchi.

Kati ya mikoa 21, Kagera inashika nafasi ya 19. Mikoa mingine inayoshika mkia kwa kupokezana ni Kigoma, Shinyanga, Dodoma na Singida.

Kulingana na takwimu za Taasisi ya Taifa ya Takwimu (National Bureau of Statistics – NBS) za mwaka 2009, wastani wa kipato cha mwananchi wa mkoa wa Kagera ulikuwa Sh. 483,158/- kwa mwaka.

Kiwango hicho ni kidogo ikilinganishwa na wastani wa pato la mtu kitaifa la shilingi 693,470/- kwa mwaka.

Takwimu zilizotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mohammed Babu, kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyetembelea mkoa huo hivi karibuni zinatisha. Ebu angalia wastani wa pato la mtu kwa mwaka katika kila Halmashauri ya Wilaya kama zilivyotolewa kwa waziri mkuu.

Wastani wa pato la mtu kwa mwaka katika wilaya ya Muleba ni Sh. 150,000/-; sawa na pato la Sh. 417/- kwa siku.

Katika wilaya ya Ngara, pato la mtu kwa mwaka ni Sh. 245,000/-, sawa na Sh. 670/- kwa siku. Kwa wilaya ya Chato, pato la mtu kwa mwaka ni Sh. 360,000/-, sawa na shilingi 1,000/- kwa siku.

Katika Manispaa ya Bukoba, pato la mtu kwa mwaka ni Sh. 385,000/-, sawa na shilingi 1,069/- kwa siku. Wilaya ya Bukoba Vijijini ina pato la mtu kwa mwaka la Sh. 386,000/-, sawa na shilingi1,072/- kwa siku.

Wilaya ya Biharamulo ina pato la Sh. 420,000/-kwa mtu kwa mwaka, sawa na Sh. 1,167/- kwa siku; wakati wilaya ya Karagwe ina pato la mtu kwa mwaka la Sh. 425,000/-, sawa na Sh. ,181/- kwa siku.

Wastani wa pato la mtu kimkoa ni Sh. 483,158 kwa mwaka, sawa na shilingi 1,342/- kwa siku. Kitaifa, wastani wa pato la mtu kwa mwaka ni Sh. 693,470/-, sawa na shilingi 1,926 kwa siku.

Wakati wa majumlisho ya ziara yake ya siku tano mkoani Kagera, Pnda  alisema, pamoja na mambo mengine, “… wilaya nilizotembelea wastani wa vipato vyao ni chini ya wastani wa kitaifa wa sh 693,470.

“Tatizo ninaloliona mimi, hamjawa wabunifu kuwashirikisha wananchi wenu kikamilifu katika kuibua na kutekeleza miradi ya maendeleo. Nawataka viongozi wote kujipanga vizuri ili kujibu hoja hiyo ya pato dogo kwa kuongeza uzalishaji,” alisema.

Mkoa wa Kagera una fursa nyingi za kupata mapato mengi kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi, lakini mapato hayo hayawiani na hali ya maisha ya wananchi wa mkoa huo.

Mathalan mwaka 2010/2011 mkoa ulipata mapato ya Sh. bilioni 41.6 kutokana na zao la kahawa wakati zao la pamba  liliuingizia mkoa pato la Sh. milioni 176.7.

Mkoa wa Kagera una fursa kubwa ya kuongeza tija na uzalishaji kwenye sekta za kilimo, mifugo  na uvuvi. Una ardhi nzuri, maji mengi, mabonde kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na hali nzuri ya hewa.

Eneo linalofaa kwa kilimo mkoani Kagera ni hekta 1,593,758, lakini eneo linalolimwa ni hekta 674,174 tu, sawa na asilimia 46.7. Mkoa una eneo linalofaa kwa umwagiliaji la hekta 29,798 lakini eneo linalolimwa ni hekta 18,370, sawa na asilimia 62.

Wilaya ya Ngara ina eneo linalofaa kwa kilimo cha umwagiliaji la hekta 303,483 lakini eneo linalotumika ni hekta 56,210, sawa na asilimia 18.5 tu.

Wilaya ya Chato ina eneo la hekta 267,900 linalofaa kwa umwagiliaji lakini ni hekta 99,123 zinazotumika, sawa na asilimia 37 tu, wakati wilaya ya Muleba ina hekta 288,000 zinazofaa kwa umwagiliaji lakini ni hekta 143,137 zinazotumika, sawa na asilimia 50.

Takwimu  zinaonesha kuwa utekelezaji wa maelekezo ya serikali ya ununuzi wa matrekta madogo (power tillers) 50 kwa kila Halmashauri ya Wilaya; na matrekta madogo 20 kwa manispaa bado hauridhishi.

Mkoa mzima una matrekta makubwa 75 na matrekta madogo 130 tu. Ili kuongeza eneo la kilimo ni muhimu wananchi wahimizwe kutumia zana bora za kilimo yakiwemo matrekta madogo na plau ili kuwapunguzia suluba za jembe la mkono ambalo haliwezi kuleta mapinduzi ya kilimo.

Changamoto kubwa kwa uongozi wa  mkoa wa Kagera ni kuhimiza kilimo cha umwagiliaji, matumizi ya zana za kisasa za kilimo na matumizi ya mbolea.

Viongozi katika kila halmashauri ya wilaya  wanatakiwa kujiuliza wana watu wangapi  na kati ya hao ni wangapi wenye uwezo wa kufanya  kazi. Pia, wanatakiwa kufahamu sekta muhimu za uzalishaji na fusra nyingine zilizopo kwenye kila halmashauri.

Mkoa wa Kagera pia unatakiwa kuweka mikakati ya kupunguza kasi ya ongezeko la idadi ya watu la asilimia 3.1 kwa mwaka, ikilinganishwa na kiwango cha asilimia 2.9 kwa mwaka kwa sasa.

Viongozi wa ngazi zote wanatakiwa kuwa wabunifu na kuwapanga wananchi, ili waweze kujiletea maendeleo.

Kadhalika, wawatumie wataalam wa kilimo ili katika hatua ya mwanzo, kila mwananchi aweze kuongeza tija kwa ekari kabla ya kufikilia kuongeza eneo.

0
Your rating: None Average: 1 (1 vote)