Udekwa sekondari iliachwa ifelishe


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 18 January 2012

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

MATOKEO ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2010, kihistoria ndiyo yalikuwa mabaya zaidi nchini, na kila mdau wa elimu alijitetea au alitoa sababu kwa nini hali hiyo ilijitokeza.

Walimu walijitokeza kueleza changamoto mbalimbali zilizowakumba katika mchakato wa utoaji elimu na hasa mazingira magumu waliyofanyia kazi.

Uhaba wa walimu, ukosefu wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, ukosefu wa maabara na maktaba, walimu kuishi mbali na vitui vya kazi na kufundisha masomo wasiyoyasomea, ni miongoni mwa matatizo makuu.

Maafisa elimu na wawakilishi wengine wa serikali ngazi ya wilaya waliwasuta walimu kwa kutowajibika ipasavyo katika ufundishaji. Walidai wengi ni watoro, walevi, hawaandai masomo, hawatoi kazi darasani na wanajali mambo yao zaidi.

Wazazi na wanafunzi waliwalaumu walimu kutoroka vipindi, wakuu wa shule kutafuna fedha za miradi ya ujenzi wa shule, ulevi na kutowajibika ipasavyo.

Hata hivyo, ripoti ya ukaguzi maalum uliofanywa na Idara ya Ukaguzi wa Shule Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kwa shule 14 zilizofanya vibaya mkoani Iringa inaonyesha kuwa baadhi ya shule, ikiwemo Sekondari ya Udekwa wilayani Kilolo, ziliandaliwa kufelisha wanafunzi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyosainiwa na wakaguzi Janet A.D. Kitosi na Beatrice Komba, ilibainika wakati wa ukaguzi wa shule hiyo kuwa ilipoanzishwa mwaka 2007 ilikuwa na walimu wawili tu tena wa leseni au wale walioitwa Vodafasta. Hapakuwa na mkuu wa shule.

Badala yake, Mratibu wa Elimu kata ya Udekwa alijipa cheo cha usimamizi wa shughuli za shule. Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo haikuona nongwa.

Mkuu wa shule wa kwanza aliteuliwa mwaka mmoja baadaye na aliwasili Machi 2008. Lakini alikaa miezi miwili tu, akatimka kwenda masomoni na akaacha usimamizi wa shule chini ya mwalimu wa leseni aliyemteua kama mkuu wa shule msaidizi.

Kwa maana hiyo basi, shule ilibaki tena chini ya walimu wale wawili wa leseni. Oktoba 2008 mwalimu mmoja wa leseni akaenda masomoni na kumwacha mwenzake. Hapo Mratibu wa Elimu wa Kata akarudi tena kusaidia kuokoa jahazi.

Katika mazingira haya, shule iligeuka kijiwe cha wanafunzi badala ya kuwa mahali pa kuchota elimu na ujuzi kwa ajili ya maisha yao. Mkuu wa shule mwingine alipelekwa Oktoba 2009.

Ripoti inasema mkuu huyo mpya alibaki akiwayawaya kwani yule mwalimu aliyekuwa ameachiwa madaraka alikataa kuachia ukubwa huo hadi Aprili 2010 ilipotumika nguvu.

Kwanza alipuuza barua aliyopewa 22 Januari 2010 na baadaye Machi alikabidhi ofisi kwa mdomo na hata alipokubali Aprili, hakukabidhi nyaraka za ofisi.

Kwa hiyo shule haikuwa na nyaraka zozote za kiutawala na hakukuwa na faili lolote lenye taarifa za wanafunzi, walimu na taarifa nyingine muhimu za shule. Shule imeendeshwa kienyeji hivyo huku Mratibu wa Elimu akiwepo.

Ripoti hiyo, ambayo nakala zilipelekwa kwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Katibu Mkuu Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI); Mkurugenzi Mtendaji Wilaya ya Kilolo; na Katibu Tawala Mkoa wa Iringa, inasema hicho ndiyo chanzo kikuu cha shule hiyo kufanya vibaya.

 “Kukosekana kwa mkuu wa shule kulisababisha kuzorota kwa usimamizi wa masuala ya utawala na taaluma shuleni na hivyo ufundishaji na kujifunza kuwa kwa kiwango duni. Matokeo yake shule ilifanya vibaya katika mtihani wa kidato cha IV mwaka 2010,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.

Kati ya wanafunzi 52 waliofanya mtihani huo, hakuna hata mmoja aliyepata daraja la I, II na III. Wanafunzi 14 walipata daraja la IV na 38 walipata sifuri.

Wakati kukiwa na sarakasi juu ya utawala, mwalimu wa kwanza mwenye diploma alipelekwa Sekondari Udekwa Machi 2010. Lakini kwa vile mwalimu mmoja wa leseni alikwenda kusoma na “mkuu wa shule wa leseni” kujiondoa baada ya kukabidhi madaraka, shule ilibaki tena na walimu wawili.

Hali hiyo ndiyo ilikuwepo hadi wanafunzi walioingia kidato cha I mwaka 2007 wanaingia kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha IV mwaka 2010.

“Ni wazi walimu hao wawili wasingemudu kazi ya kufundisha masomo yote na madarasa yote shuleni,” inasisitiza ripoti hiyo. “Kwa hiyo ukosefu wa walimu ulichangia kwa kiasi kikubwa kufanya shule iwe na ufaulu wa chini katika mtihani wa kidato cha nne.”

Wakaguzi hao wanasema kwamba wakati shule hiyo ikiwa na uhaba mkubwa wa walimu wenye ujuzi, pia ilikuwa na uhaba mkubwa wa vitabu vya kiada na ziada.

Ripoti inasema hakukuwa na kitabu hata kimoja kwa ajili ya wanafunzi kwa masomo yote tangu walipoingia sekondari hadi wanamaliza, isipokuwa nakala ya mwalimu. Mihutasari ya masomo ilipatikana wakati wanafunzi wameingia kidato cha IV mwanzoni mwa mwaka 2010.

Wanafunzi wa kidato cha nne waliohojiwa walisema kuwa tangu waanze kidato cha I walikuwa hawajawahi kupewa kitabu chochote cha kiada wala cha ziada cha aina yoyote ile kwa ajili ya kujisomea. Walimu wa shule hiyo walithibitisha.

Katika mazingira ambayo hakuna walimu wa kutosha, kuwepo vitabu husaidia wanafunzi kujifunza kwa njia ya kujisomea wenyewe. Mkuu wa shule alisema alipowasili shuleni Udekwa Januari 2010 hakukuta hata muhtasari wa somo lolote.

Kwa hiyo uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo unaweza uwe ulifurahia kuwa na shule nyingi za kata, lakini ulizitelekeza kama ripoti inavyoonyesha kwa shule ya Udekwa.

Matatizo mengine ambayo yameikumba Udekwa tangu ilipoanzishwa hadi mwaka jana ulipofanyika ukaguzi ni ukosefu wa nyumba. Kuna wakati Chuo cha Ualimu cha Kleruu kilipeleka walimu wa mafunzo, lakini adha waliyopata hakuna walimu wanaopelekwa tena kwa ajili ya mafunzo.

Wizi

Kati ya mwaka 2007 na 2009 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kupitia mpango wa MMES, ilipeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vinne vya madarasa na nyumba za walimu, na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) nao ulipeleka fedha kwa miradi hiyo. Hadi unafanyika ukaguzi huu hakukuwa na vyumba wala nyumba ya mwalimu. Nani amekula fedha hizo kiasi cha Sh. 36 milioni? Shule nyingine nchini zikoje? Tafakari!

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
No votes yet