Udhaifu wa JK bungeni


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 27 June 2012

Printer-friendly version
Rais Jakaya Kikwete

KAMBI ya upinzani imerejesha mjadala wa “udhaifu wa rais” bungeni kwa kutaja maeneo mbalimbali ambayo Rais Jakaya Kikwete alitakiwa kuchukua hatua, lakini badala yake alikaa kimya.

Michango ya wabunge wa upinzani, hata “majasiri” wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wamekariri orodha ya mambo ambayo serikali ya Rais Kikwete ilipaswa kuyachukulia hatua lakini haikufanya hivyo.

Tangu Jumanne wiki iliyopita, wakati John Mnyika (Ubungo- CHADEMA) alipotolewa nje ya bunge kwa kusema “rais ni dhaifu,” wabunge wamezidisha lawama kwa serikali kusita, kushindwa au kudharau kuchukua hatua katika mambo muhimu ya kitaifa.

Alikuwa Freeman Mbowe, kiongozi wa upinzani na mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo, aliyesema bungeni Dodoma juzi, kuwa hata mshikamano wa taifa umeachwa kumomonyoka.

Akijadili bajeti ya waziri mkuu, Mbowe alisema kutokana na propaganda za chuki zinazofanywa na viongozi wa CCM na vyama washirika, sasa mshikamano wa taifa uko hatarini kubomoka.

Alitoa mfano wa kauli za viongozi wa CCM kwamba chama chake ni cha kikabila na kikanda; na hivyo kupanda mbegu za ubaguzi katika jamii iliyokuwa imeungana.

Kinachofanywa na chama cha Kikwete, “…kinapandikiza chuki na mpasuko miongoni mwa Watanzania; kwani maneno huumba,” amesema Mbowe na kuongeza kuwa sura hiyo ya mpasuko kwa misingi ya ukanda na ukabila, imeanza kujitokeza hata wakati wa mijadala ndani ya bunge.

Mbowe ametaja mambo ambayo serikali ya Rais Kikwete haijatolea kauli kuwa ni pamoja na taarifa za makusanyo ya mabilioni ya shilingi na matumizi yake wakati wa kuadhimisha miaka 50 ya uhuru.

“Kambi ya upinzani inaitaka serikali kutoa mchanganuo wa matumizi hayo…ili kutekeleza dhana ya uwazi ambayo ni msingi wa utawala bora,” amesema Mbowe.

Ametaka pia kuwepo uwazi kuhusu matumizi katika kukimbiza mwenge – makusanyo na matumizi – ili wananchi waweze kuona iwapo bado kuna haja ya kuwa na zoezi hilo katika mazingira ya sasa kisiasa.

Kauli ya Mbowe ilitonesha vidonda vya lawama na shutuma kwa rais kutochukua hatua katika masuala mazito.

John Mnyika, katika andishi maalum kwa vyombo vya habari, akieleza alichotaka kusema bungeni kabla hajatolewa nje, anafafanua udhaifu wa rais.

Anasema katiba imempa rais mamlaka makubwa juu ya bunge. Kwa mfano, bunge likikataa bajeti ya serikali (Ibara 90 (2) (b)); rais analivunja.

“Kadhalika, udhaifu wa kanuni za Kudumu za Bunge umefanya wabunge kuwekewa mipaka (Kanuni 97 (2)). Hawaruhusiwi kupendekeza mabadiliko katika makadirio ya mapato na matumizi ya serikali,” anasema.

Anahitimisha kwa kusema, udhaifu wa kikatiba umetoa nguvu kubwa kwa rais juu ya bajeti na uendeshaji nchi; kwa hiyo,  udhaifu wa rais unaathiri maisha ya wananchi.

Mnyika anasema woga wa wabunge wengi, hususan wa chama kinachotawala ndio huwafanya wapige kura ya NDIYO hata kama walikosoa bajeti wakati wa kuchangia. Wanaogopa bunge likivunjwa huenda wasirudi “mjengoni.”

Hoja za rais kuwa dhaifu zilianza kujitokeza tangu miaka ya awali ya utawala wake. Ilifika mahali, aliyekuwa spika wa bunge, Samuel Sitta akamwambia aongeze “ukali kidogo” au alete bungeni muswada maalum wa kumwongezea makali ya kufanya maamuzi magumu.”

Udhaifu wa serikali ya Rais Kikwete ambao unawekwa kichwani kwake, ni pamoja na kushindwa kukusanya kodi kwa kiwango cha kuwezesha serikali kujitegemea kwa fedha za ndani ya nchi.

Mfano ni serikali kushindwa kukusanya kodi na huku ikitoa misamaha ya zaidi ya Sh. 1.7 trilioni wakati haina dawa, barabara wala vifaa vya shule, mishahara ya walimu na madaktari.

Udhaifu mwingine ni ule wa serikali kutumia zaidi ya kile inachokusanya na kusababisha serikali kukopa kutoka benki za kibiashara tena kwa matumizi ya kawaida na siyo maendeleo.

Kinachoonekana kukera wananchi, hasa katika siku za karibuni, ni serikali ya Rais Kikwete kukaa kimya juu ya madai ya walimu na madaktari.

Ni mwaka sasa tangu waahidiwe kutimiziwa madai yao; lakini serikali, ama imeshindwa, imesahau wajibu, ni dhaifu au haitaki kutimiza ahadi zake.

Yamekuwa mazoea kwa serikali kukimbilia mahakama kuu, katika dakika za mwisho, kuzuia migomo; wakati tayari wananchi wameanza kuumia na hata wengine kufa.

Rais na serikali yake wamelaumiwa kwa udhaifu wa kutochukua hatua dhidi ya mafisadi – ndani ya serikali na CCM.

Ama wamepuuza, wamekaa kimya, wamekuwa wapole, au wamesamehe tu kwa misingi ya kulindana kama ilivyoonyesha katika wizi mpevu na ufisadi wa akaunti ya madeni ya nje (EPA) katika Benki Kuu (BoT).

Kwa mfano, wizi wa kampuni ya Kagoda Agriculture Limited wa zaidi ya Sh. 40 bilioni; unaoelezeka kuhusu nani alichukua fedha, kupitia benki ipi na baadaye katika benki zipi, umeachwa bila kushughulikiwa.

Katika midomo ya wahisani, neno udhaifu limekuwa msamiati wa kudumu. Wamekuwa wakitaka serikali kuondoa udhaifu katika matumizi ya fedha za umma na katika kukabiliana na rushwa kubwa na ndogo.

Kuna wakati wafadhili walitishia, na hata kusitisha misaada kwenye bajeti ya taifa, kwa kukerwa na udhaifu katika utekelezaji wa makubaliano na serikali.

Udhaifu mwingine umeonekana katika kwenda nje ya nchi kuomba misaada, wakati huohuo misaada anayopewa hailingani na thamani na raslimali zinazovunwa kwenye nchi anakotoka rais.

Au kutoa ahadi 99 ambazo thamani yake ni zaidi ya Sh. 9 trilioni wakati ahadi hizo hazitekelezeki; au serikali kutenga asilimia 70 kwa matumizi kwenye bajeti yake na asilimia 30 kwenye maendeleo. Huu dhahiri ni aina ya udhaifu wa serikali na viongozi wavivu wa kufikiri.

Inatarajiwa neno “udhaifu” litatawala mjadala wa mkutano wa bajeti hadi Agosti; huku wabunge wa CCM wakijibu mapigo na hata kutishia kupigana na kutishia kifo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: