Udhaifu wa mawaziri wa Kikwete hadharani


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 01 November 2009

Printer-friendly version

KUZOROTA kwa utendaji wa serikali ya Rais Jakaya Kikwete kunatokana, pamoja na mambo mengine, baadhi ya watendaji wake kuhujumiana, imefahamika.

Uchunguzi wa MwanaHALISI unaonyesha kuwa baadhi ya watendaji, wakiwamo mawaziri na naibu mawaziri, hawafanyi kazi kama timu moja.

Baadhi ya mawaziri ndani ya serikali ya Kikwete wamefikia hatua ya kuanikana mapungufu yao hadharani.

Hali hii ya mawaziri na watendaji wengine wa serikali kuhujumiana ilianza mara baada ya Kikwete kuunda serikali.

“Mambo mengi ndani ya serikali yamekwama kutokana na watendaji kuhujumiana. Hata ndani ya Baraza la Mawaziri, hali si nzuri,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi katika serikali kwa sharti la kutotajwa jina.

Amesema wakati mawaziri wanahujumu naibu mawaziri, nao naibu mawaziri wanahujumu mawaziri wao.

MwanaHALISI limefanikiwa kunasa baadhi ya barua na ujumbe mbalimbali vilivyoandikwa na mawaziri na naibu mawaziri ambavyo vimejaa malalamiko, tuhuma na shutuma dhidi ya wenzao.

Mfano mzuri ni ujumbe ulioandikwa na naibu waziri mmoja (jina tunalo) na kupelekwa kwa mbunge mmoja mwanamke wa Bunge la Muungano.

Sehemu ya ujumbe huo inasema, “Dada yangu, Kilicho nileta leo ni posho tu! Niko hoi!”

Ujumbe huu uliandikwa na mmoja wa mawaziri ambaye wakati huo alikuwa naibu waziri.

“Kuweni na wikendi njema (Have a nice weekend). Mimi nakwenda Dar leo (I am going to Dar today!)…Kuhusu huyu waziri, we acha tu! Aibu,” unasema ujumbe ukilalamikia na kukejeli waziri.

Taarifa zinasema wakati naibu waziri akitupa kijembe hicho kwa waziri wake, waziri husika alikuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake bungeni.

Baadhi ya wabunge waliozungumza na mwandishi wa habari hizi wamesema naibu waziri huyo alikuwa “amechacha” na asingeweza kufuatilia kilichokuwa kinaendelea bungeni.

“Unaona, mawaziri wa aina hii hawana msaada kwa rais, serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM). Waziri mzima anasema ameingia bungeni kufuata posho, badala ya kutetea serikali yake au wananchi?” ameuliza mbunge mmoja.

Anasema mawaziri wenye uhusiano wa aina hii hawawezi kufanya kazi pamoja; na yule aliyeandika ujumbe ameonyesha yumo serikalini kutafuta “mbwembwe na fedha tu.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: