Udikteta wa chama usipewe nafasi


Joseph Mihangwa's picture

Na Joseph Mihangwa - Imechapwa 09 September 2008

Printer-friendly version
Makamu Mwenyekiti CCM, Pius Msekwa

WAASISI wa demokrasia – nchi za magharibi – huipima Afrika kwa kigezo cha kuwa na vyama vingi hata kama huzaa serikali kandamizi.

Tatizo barani Afrika ni kung’ang’ania sera ya chama kushika hatamu. Kupitia itikadi ya ujamaa, hutekeleza malengo maalum ya kisiasa huku azma hasa ikiwa kujiimarisha kiutawala dhidi ya wananchi.

Hapo ndipo chama cha siasa kinapojigeuza genge la waatamia madaraka wanaojuana na wapambe wao wasiotaka mtawala mwingine kuingia.

Chini ya mfumo huu, vyombo vya dola huwa sehemu ya utawala ili kuendeleza watawala hao huku upinzani ukibaki jina tu. Kazi ya kufikiri na kupanga “maendeleo” huwa jukumu la viongozi badala ya kushirikisha wananchi.

Mwalimu Julius Nyerere alianzisha mjadala ambao mwishowe ulifanikisha kurudishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1993.

Mwalimu alipohutubia mkutano wa Jumuiya ya Vijana ya CCM Februari 1990, na baadaye 26 Juni 1990 kwa mkutano wa Jumuiya hiyohiyo Mkoa wa Mwanza, alisema: “CCM imesahau jukumu na sababu za kuwapo kwake; chama kilichopaswa kuwa chombo cha maendeleo ya watu, sasa kipo kwa ajili ya chaguzi tu: kinaendelea kuwapo kwa sababu kinabebwa na sheria inayozua upinzani. Kukosekana kwa upinzani kunafanya kilale usingizi....”

Alisema CCM ilikuwa ikijiendesha kwa njozi za ukuu wa chama (Party Supremacy), uongozi ulijiweka mbali na wavuja jasho, ufa katika kunufaika na rasilimali za taifa ulipanuka kati ya viongozi na wavuja jasho, na hivyo mabadiliko yalikuwa hayakwepeki.

Vyama vingi vimechochea mabadiliko yoyote? Jibu ni hakuna. Tofauti na awali, tunachoshuhudia ni migogoro na uhasama wa vyama, vya upinzani vyenyewe au kati ya chama na wanachama wake, na kuzua mitafaruku inayodhoofisha umoja wa kitaifa.

Vyama vya siasa vyote vimetekeleza au havielewi majukumu yake, na kama alivyobaini Mwalimu, vimebaki na jukumu pekee la kupigana kubakia au kutaka kuingia Ikulu badala ya kupanga maendeleo ya Taifa. Wananchi wamegeuzwa watu wa kuunga mkono vita vya wanasiasa.

Leo hakuna chama – si CCM wala cha upinzani – chenye mtizamo wa wakulima na wafanyakazi kama ilivyokuwa zama za harakati za uhuru. Makundi hayo yameachwa yatima baada ya kufa kwa TANU na Afro-Shirazi (ASP).

Kuikosoa Serikali ni kujitafutia balaa, licha ya katiba kutoa haki hiyo. Hali ilivyo, kikundi kidogo cha watawala kinahodhi mamlaka ya nchi nzima.

Mfano, tumweleweje mzee Kingunge Ngombale-Mwiru anaposema wabunge wa CCM wanaokemea ufisadi wanasaidia upinzani? Au pale Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa anaposema wabunge wa CCM wanapaswa kufuata taratibu maalum wanapoihoji serikali bungeni?

Tuseme Msekwa ambaye ni mwanasheria kitaaluma, amesahau kuwa serikali inawajibika kwa Bunge ambalo linapaswa kuwakilisha matakwa ya wananchi badala ya chama tawala, na kwamba wabunge wanaapa na kuwajibika (kutekeleza) bungeni kwa mujibu wa katiba ya nchi na siyo kwa chama?

Tueleweje tunapoambiwa Bunge liwachemshe tu mawaziri siyo “kuwayeyusha?”

Baraza la Mawaziri katika ujumla wake na kwa waziri mmoja mmoja, wanawajibika kwa Bunge kwa kazi zao. Inakuaje kuwepo wigo wa kuwakingia kifua wasihojiwe bungeni.

Hivi si kweli kwamba kuuliza utendaji wa serikali ni jukumu la haki la kila mbunge bila ya kujali chama kilichompeleka bungeni?

Kwa mfano, ufisadi ni dhambi kama ilivyo udikteta kwa demokrasia na utawala bora. Mzee Kingune na Msekwa wanaposhutumu wabunge wakemeaji ufisadi wanatetea kitu gani?

Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba naye anaposema chama kisihusishwe na ufisadi kwa sababu tu baadhi ya watuhumiwa ni wanachama wake anakusudia kutenganisha nini?

Kauli za viongozi hawa watatu zinaonyesha dhahiri kulea ufisadi na mwenendo unaokiuka maadili mema. Hiyo ni hatari na kwa kweli haikubaliki.

Ni kauli zinazolenga kutisha wabunge wakakamavu ambao hawana isipokuwa kutetea chama chao pamoja na wananchi wanaowawakilisha.

Msimamo huo unajenga udikteta uleule uliotumiwa na Mwalimu kuanzisha mchakato wa mabadiliko.

Ngombale-Mwiru ni mbunge wa kuteuliwa anayepaswa kuzungumza lugha ya kinchi vinginevyo umma utahoji sababu za kuwapo kwake maana hawakilishi matakwa ya wananchi. Hakuna anayeamini amezuiwa kuikosoa serikali.

Kiongozi wa Upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed, aliteuliwa mbunge na Rais Benjamin Mkapa mwaka 2000. Mbona hakuvutana na rais kwa kuikosoa serikali mpaka muda ulipokwisha?

Komredi tuliyenaye, si yule tuliyemjua wakati wa mapambano ya uhuru. Alikuwa akiita “koleo” koleo na akisema nyeupe aliyoamini ni nyeupe. Amelishwa nini hata kubadilika misingi ya fikra.

Kuna pengo kubwa la matajiri na masikini na hatari iliopo ni kwamba linazidi kupanuka kwa sababu hakuna hatua za kulidhibiti. Ufisadi unasaidia kuliimarisha badala ya kulipunguza.

Chama kilichokuwa tumaini la masikini kimegeuka cha kutetea ufisadi. Kimekuwa chama kilichosheheni viongozi wa fikra mgando, ambao wanalaumu wale wanaokemea ufisadi wakati wanaamini unagawa raia kimatabaka.

Ingawa ni kada wa CCM, natofautiana na fikra hizi maana naziona zinachochea uasi dhidi ya chama. Zinaelekeza taifa katika machafuko kwani wakichoka – na ipo siku watachoka tu – wanyonge wataamua kivyao.

Pasipo siasa tengamano panazuka taifa legelege. Watu wake wanabaki kutuhumiana na huko kunajengeka chuki baina ya wanyonge na viongozi wao.

Matokeo ya hali hii ni kuibuka kwa chembe za uanaharakati. Wanatokea watu wanaanzisha harakati za kimapinduzi ili kurudisha taifa mikononi mwao.

Chama tawala kilitakiwa kuwa kimebadilika na kimeingia katika kuhakikisha hata katiba ya nchi inaelekeza taifa kwenye misingi inayojenga mshikamano madhubuti miongoni mwa jamii.

Udhaifu wa vyama unaweza kuondoka iwapo vitaundwa vyama vya kitaifa kikwelikweli siyo kama ilivyo sasa. Vipo vyama vipovipo tu na laiti pangekuwa na udhati hasa upande wa Msajili, vingi vingekuwa vimefutwa.

Viongozi wakuu wa CCM lazima wakubali kuwa upinzani ni halali Tanzania. Hawawezi kuishi kwa imani kwamba wana uhalali peke yao wa kuongoza au kwamba si watu wa kuhojiwa.

Taifa linalonuka kwa utawala mbaya wa uchumi, rushwa, uzembe na ubadhirifu haliwezi kutoka hapo bila ya wabunge na wanaharakati wengine wasiokuwa wanasiasa kuhoji utendaji wa serikali.

Ukomavu wa kisiasa chini ya demokrasia ya uwakilishi unathibishwa na maneno ya Edmund Burke: “Bunge si mkutano wa mabalozi kuwakilisha vikundi vyenye uhasama, kila kikundi kikishikilia msimamo wake ishinde, kama wakala na wakili dhidi ya mawakala na mawakili wengine; bali Bunge ni baraza lenye malengo ya kitaifa kwa taifa moja, lenye takwa moja kwa ajili ya wote na ambalo ubinafsi na chuki za ovyo hazipaswi kuongoza, bali mazuri yote kwa walio wengi yanapaswa kutekelezwa.”

Kauli za baadhi ya wanasiasa zinachefua. Wanapaswa kusoma alama za nyakati ili kujua na watu wanafikiri na kutaka nini. Wakipingana na fikra za wengi, watakuwa wanapigana na wakati; na wakati ni ukuta.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: