Udini isiwe silaha ya uhalifu


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 28 September 2011

Printer-friendly version
Gumzo la Wiki

KAMPENI za uchaguzi mdogo wa ubunge katika jimbo la Igunga, mkoani Tabora, zinazokaribia kufika ukingoni Jumamosi wiki hii, zimewaibua hata wasiyotarajiwa. Walianza Baraza Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA), lililozusha mtafaruku kwa tamko lao la kuwataka waislamu wa Igunga waskipigie kura Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kwa kile walichodai, “ni adui wa uislamu na waislamu.”

Akafuatia Katibu mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilson Mukama aliyeutangazia ulimwengu kwamba CHADEMA kilipeleka baadhi ya vijana katika baadhi ya nchi ikiwamo Pakistan, Libya na Afghanistan kujifunza ugaidi kwa nia ya kuleta vurugu nchini.

Akaja Hamis Makala, katibu kata wa CCM katika kata ya Nyandekwa, wilayani Igunga ambaye alidai kuchomewa nyumba yake ndogo kwa moto pamoja na banda lake la kuku. Nyumba aliyodai imechomwa moto alisema ilikuwa anaitumia kama jiko.

Katika kupalilia uwongo huo, Mukama alifika hadi kunakoitwa eneo la tukio, ambako Makala alidai watu wasiojulikana walifika nyumbani kwake usiku wa manane na kuchoma nyumba yake hiyo ya nyuma moto. Katika tukio hilo, alidai kuku 15 kati ya 21 waliokuwamo ndani ya banda hilo waliteketea na moto.

Tuanze na hili la BAKWATA. Hii si mara ya kwanza kwa baraza hilo kutoa tamko linalowataka waislamu wasikiunge mkono CHADEMA kwa madai kuwa ni chama cha wakiristo.

Katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu uliyopita, kiongozi wa BAKWATA, Sheikh Issa Shaban Simba alinukuliwa akisema waislam wasifungamane na CHADEMA kwa kuwa chama hicho hakifuati mafundisho na itikadi ya dini ya kiislamu kwa kuwa kinamuandama Rais Jakaya Kikwete kwa sababu ya dini yake.

Kuwaambia watu wa dini fulani wasifungamane na chama fulani kwa sababu tu chama hicho kinaonekana kutofuata mafundisho na itikadi ya dini hiyo, ni jambo lisilowezekana kama ambavyo ni vigumu kuwalazimisha watu kukipenda chama fulani kwa sababu kinependelea dini fulani.

Hatua ya BAKWATA mjini Igunga kutaka waislamu wasiichague CHADEMA, na hata kauli zile za awali, zinazua maswali mengi na kuleta sononeko katika mioyo ya wapenda uislamu, siasa safi na taifa lenye umoja. Zinahitajika akili za ziada kuelewa malengo ya BAKWATA katika mwenendo huu.

Hii ni kwa sababu, matamshi haya yanawagawa waislamu na yanagawa taifa. Kwa mfano, ndani ya CHADEMA kuna watu wa dini zote kama ilivyo ndani ya CCM. Wanafahamu maana ya vazi la kiislamu. Wameona na wengine wameshuhudia, kwamba Bi. Fatuma Kimario hakuwa amevaa kiislamu. Wala hicho kinachoitwa hijab, haikuwa haijab yenyewe. Bi. Fatuma alivaa mtandio ambao unavaliwa na kila mwanamke bila kujali itikadi ya dini yake.

Lakini kuna hili pia: Ni lini Uislam umekuwa rafiki wa chama tawala? Yako maandiko mengi yaliyoibuka miaka ya karibuni yanayoonyesha kuwa dhuluma kubwa imefanywa kwa waislam tangu tupate uhuru. Ikiwa dai hili ni kweli, iweje leo chama tawala kilindwe na waislam kwa kukitetea na kutaka kipewe Igunga?

Najiunga na wanaohoji kwa sababu, naamini kabisa kuwa uislam na ukiristo ni zaidi ya mtu mmoja aliye kiongozi katika taasisi. Tukijenga hoja zetu na misimamo kwa sababu ya chama fulani, tutajinyima thawabu tunayoitafuta kwa udi na uvumba katika dini zetu.

Baadhi ya waislamu niliozungumza nao, wanapingana na msimamo wa BAKWATA waziwazi. Wengine wanafika mbali zaidi kwa kusema, kudai chombo hicho kinawakilisha waislamu wote ni kuudhalisha uislamu wenyewe. Kwamba ni ruksa kuongelea BAKWATA bila kuzungumzia uislam na kuzungumzia uislamu bila kuzungumzia BAKWATA.

Kwangu mimi, hii ni mada pekee nisiyoweza kuigusia kwa sasa, lakini niseme inagusa kiini cha mtafaruku unaoonekana katika matamko ya BAKWATA ya sasa na yale ya huko nyuma.

Lakini ukweli ni kwamba ni hatari kuilinda CCM kwa silaha bandia ya udini. Kulazimika kutazama matatizo ya nchi kwa kutumia miwani ya udini na hata kujaribu kuyatatua kwa kutumia udini, kunaweza kuingia nchi katika mgogoro mkubwa. Matatizo ya taifa letu ni makubwa kuliko udini wa kulazimisha au kuchonganisha vyama na wanachama wake.

Hata sasa, waislamu wengi walio nje ya BAKWATA, wanaliona baraza hilo kuwa ndio adui mkubwa wa uislamu kuliko CHADEMA na serikali. Kwamba kukosekana kwa mwelekeo katika dini ya kiislamu nchini kunatokana na BAKWATA yenyewe kujisalimisha mikononi mwa serikali na kujigeuzwa tawi la CCM.

Aidha, kauli ya BAKWATA kwamba CHADEMA ni adui wa waislamu kutokana na hatua ya wanaodaiwa kuwa wafuasi wake kumvua mkuu wa wilaya hijab yake, kunaiondoa hoja kuu ya baadhi ya waislamu, kwamba adui wa uislamu ni mfumo – kristo uliojikita katika utawala na uendeshaji wa serikali.

Je, mambo haya yanatokana na nini? Jibu liko wazi, kwamba CCM wanahaha kutaka kuliokoa jimbo la Igunga. Ndiyo maana kabla BAKWATA haijatoa tamko lake, walikutana na baadhi ya viongozi wa CCM. Walijadili na kwenda mbele zaidi kwa kuwaandalia wanaojiita viongozi wa dini tamko la kusoma mbele ya wandishi wa habari.

Kana kwamba hiyo haitoshi, CCM waliwalipa hata posho viongozi hao, waliwasafirisha na kuwapatia ulinzi ili wazungumze walichoandaliwa. Kama madai haya ni kweli, basi ni sahihi kusema adui wa uislamu ni BAKWATA, siyo kanisa wala CHADEMA.

Ni sahihi pia kusema, kwamba chanzo cha kiwewe hiki ni unafiki huu wa baadhi ya viongozi wa BAKWATA.

Naweza kusema pasipo shaka kuwa uislam wa aina ya matamshi ya BAKWATA waweza kutia kasoro mapenzi waliyonayo wakristo kwa CCM na hatimaye CHADEMA wakaibuka washindi Igunga. Tamko la namna hii linawakatisha tamaa wale wasio wa dini pia. Ni hatari kuilinda CCM kwa silaha bandia ya udini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: