Udini wa CCM huu hapa


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinalia, kinalalamika, kinapigia magoti wanachama, kinadharau, kinatoa kauli chafu; kimeshikwa kikashika.

CCM wanatafuta pa kutokea, wanajiuliza wamekosea wapi, wanasaka mchawi wao, wanaomba wasamehewe ili waendelee kutawala. Mambo ni magumu kwao, sasa wameamua kutisha wananchi, wameibua vitisho vya udini na ukabila.

Viongozi wake wakuu wanapita kila kona kukemea kile wanachodai baadhi ya wagombea wa upinzani kufanya kampeni za udini na ukabila.

Wanaolalamika ni pamoja na mgombea urais kupitia CCM, Jakaya Kikwete.

Sawa, chama kilichopewa dhamana ya kuongoza nchi kina kila sababu ya kukemea dalili zozote za udini na ukabila katika kampeni na katika uongozi kwa ujumla kwani madhara yake ni makubwa na hatari mno.

Madhara ya udini yanajionyesha vizuri katika nchi za Nigeria (kusini Wakristo, kaskazini Waislamu). Vile vile tumeshuhudia Sudan ikikatwa mapande kutokana na tofauti za kidini; Kusini kuna Wakristo na Kaskazini Waislamu wanaoongoza serikali. Kosovo iliteketea kutokana na udini.

Madhara ya ukabila tumeyaona nchi jirani za Rwanda na Burundi ambazo hata kabla ya kupata uhuru zilikuwa zinatafunwa na ukabila (Wahutu na Watutsi) ilhali Somalia inateketea kwa ubaguzi wa koo.

Viongozi wa CCM wamekusanya matukio hayo ya nje na kupandikiza woga kwa wananchi.

Tujiulize, hivi ni kweli kuna udini kama wa Nigeria na Sudan au kuna ukabila kama wa Rwanda na Burundi? Kuna eneo Tanzania unaloweza kusema ni ukanda wa Wakristo au Waislamu tu?

Tujiulize, ni kweli kuna chama kinafanya kampeni zake kwa misingi ya udini na ukabila? Hivi kuna chama kinachoungwa mkono na Wakristo tu au Waislamu tu?

Hizi ni kampeni chafu za CCM; wamebaki wanatafuta huruma ya wapigakura na wanatumia njia ya kusingizia, kubambikia udini kwa Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Deomkrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Kijuujuu CCM inaonekana ina uongozi mchanganyiko wa Waislamu na Wakristo, lakini si kweli.

Tazama Kikwete anapita akijipigia kampeni achaguliwe tena kuwa rais; anasaidiwa na Mgombea mwenza, Dk. Gharib Bilali huku Meneja kampeni ni Abdulrahman Kinana.

Wanaopita mikoani kuomba kura kwa mgombea huyo na wabunge ni Yusuf Makamba, mke wa rais, Salma Kikwete, mtoto wao Ridhiwan Kikwete. Kuna Mkristo hapo?

Wana CCM wenyewe wanalalamikia safu hii wakisema kuwa haitoi uwakilishi mzuri katika uongozi wa taifa alioulea Mwalimu Julius Nyerere kwa miaka mingi.

Watu wajiulize kwa nini makamu wa mwenyekiti, Pius Msekwa hashirikishwi? Yuko wapi, Mizengo Peter Pinda katika kampeni? Jibu ni kwamba wamebaguliwa.

Safu ya CUF, Mwenyekiti ni Prof. Ibrahim Lipumba, Makamu mwenyekiti ni, Machano Khamis Ali, Katibu mkuu ni Seif Shariff Hamad. Meneja wa kampeni ni Joram Bashange.

Safu hiyo ya CUF ina tofauti gani na CCM? Kwa nini watu waamini kuna udini kwenye CUF na siyo CCM?

Katika CHADEMA Mwenyekiti ni Freeman Mbowe, Makamu mwenyekiti ni Said Arfi (Mbunge wa Mpanda Kati), Katibu mkuu ni Dk. Willibrod Slaa (Karatu) ambaye ni mgombea urais na Naibu Katibu mkuu, Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini). Uko wapi udini na ukabila katika safu hiyo?

CCM ni wazushi, waongo na wanafiki. Mwaka 1995 wakati uongozi wa CCM ulikuwa chini ya mwenyekiti, Benjamin Mkapa ilizushwa ionekane CUF ina udini na NCCR-Mageuzi ina ukabila. Udini uliokuwa unasemwa wakati ule ni Uislamu.

Kwa vile tangu mwaka 2005, uongozi wa CCM una Waislamu, inalazimisha ionekane CHADEMA ina udini na ukabila. Udini unaolalamikiwa leo ni Ukristo.

Wanafiki! Mwaka huo huo maaskofu walitamka wazi, “Kikwete ni chaguo la Mungu” na hadi leo, hakuna aliyetengua kauli hiyo. Udini wanaohofia CCM uko chama kipi?

Mbinu chafu hizi za CCM zitatuchanganya, kujenga chuki na kutufarakanisha—tusiwakubali. Adui mkubwa wa maisha ya watu ni ufisadi wa CCM siyo Usilamu na Ukristo.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: