Udini wateka bunge


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 07 July 2009

Printer-friendly version

KIRUSI kimeanza kulimung’unya Bunge. Ni udini. Baadhi ya wabunge wanalalamika kuwa wanasakamwa kutokana na imani za kidini.
 
Baadhi yao wanadai kuwa mawaziri wengi wanaosakamwa bungeni ni wale kutoka madhehebu ya Kiislamu.
 
Juzi Jumamosi kulikuwa na baadhi waliokuwa wakidai kuwa hata kukwama kwa bajeti ya Waziri wa Miundombinu, Shukuru Kawambwa (Dk. Shukuru), Waziri wa Miundombinu, kunatokana na udini,” ameeleza mbunge mmoja wa viti maalum.
 
“Nakwambia baadhi ya watu wameanza kujificha nyuma ya pazia ya udini. Kama serikali haikuchukua hatua, nchi itakwenda kombo,” ameeleza mbunge huyo.
 
Alhamisi iliyopita, Bunge liliahirisha hatua ya kupitisha bajeti ya wizara ya miundombinu baada ya mbunge wa Ilemela (CCM), Anthony Dialo kuwasilisha hoja pana iliyohitaji mjadala mrefu na serikali.
 
Dialo alitaka kuhamishwa kwa kiasi cha fedha kutoka mradi wa ujenzi wa barabara ya Handeni-Mkata na Kilosa-Dumila, kwenda kwenye ujenzi wa barabara ya Iringa-Dodoma-Babati.
 
 Wanaoeneza dhana ya udini wanahusisha hata kile kinachoitwa, “mtafaruku” kati ya waziri Hawa Ghasia na Jenista Mhagama.
 
Wakati wa kupitisha makadirio na matumizi ya bajeti ya Ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejementi ya Utumishi wa Umma, Mhagama ambaye ni mbunge wa Peramiho, alimkomalia waziri Ghasia akimtuhumu “kukalia matatizo” bila kutoa maamuzi.
 
Mhagama alikuwa anamlalamikia waziri Ghasia kwa kushindwa kutatua matatizo ya watumishi wa serikali na kwamba hata pale anapopelekewa taarifa anashindwa kuzifanyia kazi au inamchukua muda mrefu kufanya maamuzi.
 
Wakitaka kugeuza hoja hiyo kuwa ya udini, mbunge huyo anasema, wanadai kuwa kama tatizo ni kushindwa kutekelezwa kwa baadhi ya ahadi za serikali, basi wabunge wangekuwa wakali katika suala la Kadhi lililomo katika Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
 
Amesema katika hilo , wabunge hawakuja juu “kwa sababu waziri aliyetoa tamko la serikali bungeni siyo Muislamu.”  Tamko la serikali kutorudisha mahakama ya Kadhi lilitolewa bungeni na Mathias Chikawe, waziri wa sheria na katiba katika serikali ya rais Jakaya Kikwete.
 
Chikawe  aliliambia bunge wiki iliyopita kuwa sheria za Kiislamu zitajumuishwa katika sheria za kawaida za nchi.
 
Mbunge mwingine amesema wanaoeneza udini wanadai kuwa suala la Kadhi sasa limetwishwa mbunge wa Kigoma Kusini, Manju Msabya (CCM), “…kana kwamba yeye ndiye anataka awe Kadhi.”
 
Kadri uchaguzi mkuu wa mwakani unavyokaribia, ndivyo joto linavyoongezeka miongoni mwa wabunge na watawala.
 
Tayari kuna taarifa kuwa baadhi ya wabunge akiwamo mmoja mwanamke wamejipanga kukwamisha bajeti ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwanguka kwa madai hayohayo ya udini.
 
Mwingine ambaye taarifa zinasema kuwa alikomaliwa na wabunge kutokana na udini, ni Waziri wa Fedha Mustafa Mkullo.
 
Hata hivyo, Diallo alipoulizwa iwapo amesikia taarifa hizo, alisema amewahi kusikia hayo, lakini hakutaka mabadiliko katika bajeti kutokana na “kusukumwa na udini bali maslahi ya taifa.”
 
Uchunguzi wa MwanaHALISI umebaini kwamba hata katika uchaguzi wa kumtafuta mbunge wa Bunge la Afrika (PAC) kutoka kambi ya upinzani ambapo mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP) alipambana na mbunge wa Gando, Pemba , Khalifa Sulemani Khalifa (CUF), ulitawaliwa kwa misingi ya udini.
 
Taarifa zinasema kwamba awali Kamati ya wabunge ya CCM iliweka msimamo wa pamoja kwa wabunge wake kumchagua Cheyo, lakini agizo hili halikuweza kutekelezwa kutokana na wabunge ambao ni waislamu kuamua kumchagua Khalifa.
 
“Katika mazingira ya kawaida, ni jambo gumu kwa wabunge wa CCM, Zanzibar kuchagua mwanachama wa CUF. Lakini katika hili, mambo yalibadilika na wabunge walimchagua Khalifa,” alisema mbunge mmoja wa CCM kutoka Zanzibar .
 
Alisema, “CCM walikubaliana kumpa Cheyo, lakini wabunge wakajenga uasi na kumpa kura Khalifa. Hili limefanyika kutokana na msukumo wa kidini,” alisema.
 
Mwingine ambaye ametajwa kuandaliwa zengwe katika kupitisha bajeti yake kwa misingi ya udini, ni Profesa Jumanne Maghembe, ambaye ni waziri wa elimu na mafunzo ya ufundi. Bajeti ya Profesa Maghembe inatarajiwa kuwasilishwa bungeni 22 Julai 2009.
 
Alipoulizwa Katibu wa Bunge la Jamhuri, Dk. Dk. Thomas Kashilila juu ya kusikia malalamiko hayo, alikiri kwamba amewahi kuyasikia madai hayo. Alisemea hadi sasa, hakuna mtu yoyote aliyepeleka malalamiko rasmi kwake, kwamba anasakamwa au kukwamishwa kwa sababu za udini.
 
 “Bunge hili lina mambo mengi. Hapa kuna mambo zaidi ya hapo. Ukiyachunguza yote, huwezi hata kufanya kazi. Nimelisikia kama ninavyosikia uvumi mwingine, lakini hakuna mtu ambaye ameleta malalamiko rasmi,” alisema na kuongeza, “Kusikia unaweza kusikia,lakini huwezi kuyathibitisha kwa sababu kama yanasemwa basi itakuwa yanaongewa kwa kificho sana .”
 
Tayari mwanasiasa na msomi mahiri nchini, Dk. Juma Ngasongwa amenukuliwa akisema, “Serikali inatakiwa kushughulikia suala hili kwa haraka.
 
Ngasongwa ambaye amewahi kuwa waziri katika serikali ya awamu ya pili na ya tatu,  amesema ikiwa serikali inaogopa kulitolea uamuzi suala la Mahakama ya Kadhi ni bora ikasema na kuweka wazi kuwa inaogopa.
 
 “…Ni muda mfupi umebaki kabla ya uchaguzi mkuu, lakini serikali haijatoa uamuzi. Kama inaogopa kufanya hivyo ni bora iseme. Mimi ni miongoni mwa walioshiriki kuitunga ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, nilikuwemo na tulisema tulimalize kabla ya uchaguzi mkuu ujao, “alisisitiza Dk. Ngasongwa.
 
Alisema kuchelewa kulitolea uamuzi suala hilo , kunaiweka serikali kwenye wakati mgumu. Alisema, “Kimsingi yalikuwapo makubaliano kuwa serikali imalize suala hilo na kutoa uamuzi sasa.”
 
Dk Juma Ngasongwa, ambaye pia ni mbunge wa Ulanga Magharibi (CCM), alisema serikali inatakiwa kufanya maamuzi ya msingi kuhusu mambo makubwa na ya msingi kama la Mahakama ya Kadhi.
 
Dk Ngasongwa ambaye amewahi kuwa waziri kwa vipindi tofauti kuanzia serikali ya awamu ya pili, alifafanua kuwa haoni tatizo kwa serikali kutolea uamuzi suala hilo . Alikumbusha kwamba wakati wa utawala wa ukoloni Mahakama ya Kadhi ilikuwepo, lakini serikali iliifuta
 
Tayari viongozi wa madhehebu ya Kiislamu wameapa kushinikiza kupatikana kwa Kadhi kwa maandamano na “njia yoyote ile.”
 
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilisema mwaka 2005 katika Ilani yake ya uchaguzi kwamba “itashughulikia suala la Kadhi.” Tangu hapo huo ndio umekuwa msingi wa waumini wengi wa Kiislam kwamba mahakama ya kadhi “inakuja.”
 
Hata hivyo, CCM ilisema tu kuwa “itashughulikia.” Kushughulikia kunaweza kuwa ni pamoja na kufuta kabisa mpango huo katika shughuli za serikali; kuliahirisha kwa sasa au kuachia mjadala wa muda mrefu.
 
Lugha hiyo ya ushawishi lakini isiyopimika kiutekelezaji, imechukuliwa na baadhi ya Waislam kuwa ya ulaghai na ubabaishaji; huku wanasiasa wakidai ni moja ya “hoja za kufanyia kazi.”

0
No votes yet