Ufisadi hautakwisha kwa ahadi


editor's picture

Na editor - Imechapwa 07 October 2008

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

INSPEKTA Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema amesikika akisema, katika mkutano wake na waandishi wa habari wiki iliyopita mjini Dar es Salaam, kwamba hakuna fisadi atakayenusurika.

Alikuwa akizungumzia watuhumiwa katika kashfa ya ufisadi katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Mwema alisema timu yao haiogopi mtu yeyote na kwamba muda ukifika hakuna atakayenusurika.

Mwema ni miongoni mwa viongozi walioteuliwa katika Timu ya Rais kufuatilia ukwapuaji wa Sh. 133 bilioni za EPA.

Alipewa jukumu hilo na Rais Jakaya Kikwete tarehe 8 Januari mwaka huu. Wengine ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Edward Hoseah na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika.   

Wakuu hao watatu walitakiwa kufanya uchunguzi kwa miezi sita na kuhakikisha fedha zilizochotwa zinarudishwa na wahusika wanashughulikiwa kulingana na sheria.

Gavana mpya wa BoT, Profesa Beno Ndullu, naye aliagizwa kuchunguza benki ili kujua watendaji wake walihusika vipi katika kufanikisha ufisadi huo, na achukue hatua za nidhamu kulingana na taratibu za Benki.

Watanzania walijulishwa kuwa maodita wamethibitisha makampuni 22 yalichotewa mabilioni ya shilingi na serikali na washirika wake baada ya kughushi nyaraka.

Timu ya Rais, ingawa ilipitiliza muda iliopewa awali, ilikabidhi ripoti yake kwa rais tarehe 8 Agosti. Tukio la makabidhiano lilifanywa kwa usiri mkubwa.

Siku tatu baadaye, 21 Agosti, Rais alihutubia Bunge na suala hilo likawa moja ya ajenda zake. Alieleza kile alichoita “hatua ya watuhumiwa kurudisha kiasi cha Sh. 53 bilioni kati ya Sh. 133 bilioni. Ndio kusema hata nusu ya kilichoibwa, haijapatikana.

Lakini wakati Watanzania wangali wanatatizwa na kutojua hatima ya hao wanaotajwa kuwa wameanza kurudisha fedha.

Hata leo haijulikani iwapo wahusika au wamiliki wa makampuni hayo 22, yaliyothibitishwa kushiriki katika ufisadi huo, watachukuliwa hatua zaidi ifikapo 30 Oktoba, hata baada ya kurejesha walichoiba. 

Alichokieleza IGP Mwema ni maneno tu na ahadi zilezile ambazo hata Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo na wengineo, walipata kuzitoa. Tunasema mapema kabisa, kwamba wananchi hawawezi kuishi kwa ahadi; wanataka matokeo ya ahadi hizo.

IGP anaposema timu yao haiogopi mtu yeyote ni sawa. Lakini hajaeleza kingine zaidi ya kuendeleza tambo za kiutendaji na ahadi zisizo na mipaka.

Na lazima watawala wajue na kuamini kuwa Watanzania wamechoka tambo na ahadi, maana hazijasaidia kubadilisha chochote.

Tunarudia kusema kwamba wanachotaka wananchi ni hatua zinazoonekana. Sasa wala hawataki kuelezwa bali kuona watuhumiwa wanapelekwa mahakamani.

Kama waliiba au walichukua au walipewa kwa idhini ya wanaodaiwa kupewa mamlaka ya kuidhinisha, itajulikana wakifikishwa huko maana watapata nafasi ya kueleza na kujitetea mbele ya sheria. 

Kinacholeta mashaka ni IGP na wenzake kusema “hawamwogopi mtu yeyote.” Hivi nani aliwaambia kuwa wanaogopa mtu au hiyo ni njia ya kukiri kuelemewa?

Watanzania wataendelea kuamini watuhumiwa wanaogopwa; tena si na Timu hiyo peke yake, bali hata Ikulu na serikali kwa ujumla, kwani hadi sasa hakuna kauli ya kuwashitaki iliyowahi kutolewa

0
No votes yet