Ufisadi umewashinda CCM


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala
Wanaotazamia mabadiliko ya ajabu ya sera na mwelekeo wamepotea – Kikwete, Desemba 21, 2005

TUNAWEZA kudanganyana kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinaongoza vita dhidi ya ufisadi; vita hii imepamba moto na inaonesha kuzaa matunda; na tunaweza kabisa kukumbatiana kwa kupongezana kuwa miaka mitano iliyopita utawala unaomaliza muda wake 31 Oktoba 2010 umefanikiwa kuufumua mfumo wa utawala wa kifisadi ambao umejikita katika jamii yetu kwa takribani miaka 25 sasa.

Wapo wanaoweza kufanya hivyo kwa furaha na kicheko cha machozi. Hawa ni wale waliohudhuria mkutano wa kampeni wa CCM katika viwanja vya Jangwani, jijini Dar es Salaam.

Lakini ni ukweli usio na shaka kwamba walichonacho ni imani isiyo na msingi wowote.

Miaka mitano iliyopita Watanzania walitarajia kuona kuwa serikali safi, yenye maono ya kupambana na ufisadi na kuelekeza nguvu zake katika kurejesha tunu za uadilifu, uaminifu na umakini katika utumishi wa umma inashika madaraka.

Walitarajia kuona ujenzi mpya wa taifa unaanza kwa kasi mpya, nguvu mpya na ari mpya.

Walitarajia kuwa mikataba mibovu haitaingiwa tena, fedha za umma zitalindwa vizuri zaidi, na chama kilichopo ikulu kitajisahihisha na kujisafisha.

Lakini njozi hizo zimetoweka kama ukungu wa asubuhi.

Yaliyotokea miaka mitano iliyopita ni yale yaliyohofiwa na ambayo hayakutarajiwa. Bado kama taifa tunahangaika na mfumo uleule wa utawala wa kifisadi, huku masuala muhimu ambayo tuliona yakichomoza miaka kumi kabla ya Kikwete kuingia madarakani yakizidi kujirudia.

Kimsingi linapokuja suala la ufisadi wenyewe bado serikali imeshindwa kuonyesha kama inatambua kuwapo kwa tatizo.

Kwa maandishi mbalimbali CCM na serikali yake wanatambua kuwa rushwa (ambayo ni sehemu ya ufisadi) ni tatizo kubwa sana na la hatari.

Kikwete mwenyewe amelizungumzia suala hili wakati akifungua mkutano wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani Mbeya.

Alisema, “…Kuenea kwa rushwa katika jamii ni ishara ya mapungufu katika uwezo wetu wa kuizuia. Ni ishara ya kushindwa kwa ushawishi wa kisiasa, kijamii na kidini kwa jamii ili ichukie, ikemee na iikatae rushwa.

“Rushwa inafanya uongozi kuwa kitu kinachonunulika kama bidhaa.

Hali hii, inapunguza uhalali wa mamlaka za uongozi na utawala kwa wanaoingia kwa rushwa. Ikiachwa kuendelea kushamiri itapunguza imani ya wananchi kwa mfumo mzima wa demokrasia.”

Akaongeza, siyo tu ni hatari kwa haki lakini vilevile inatishia “usalama wa taifa.” Akataka wote kuungana kuitokomeza.

Lakini kilichotokea ndani ya chama chake na yeye mwenyewe kushindwa kuchukua hatua, ni kielelezo kingine kwamba Kikwete ni bingwa wa kunena, lakini si kutenda.

Kwamba anakiri kuwa rushwa ni hatari na mbaya. Wakati hotuba hiyo inatolewa kashifa ya Richmond lilikuwa linaanza kufukuta taratibu.

Wala tulikuwa hatujafikia kwenye Buzwagi na ukwapuaji katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ndio kabisa lilikuwa halijaiva.

Wakati anazungumza hayo suala la Meremeta na ufujaji katika halmashauri zetu ulikuwa haujawa wazi kwa umma kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali (CAG).

Huku Kikwete akitapa kupambana na rushwa, orodha ile ya mafisadi ilikuwa haijatangazwa katika viwanja vya Jangawani kama ilivyofanywa na Dk. Willibrod Slaa.

Ninachosema ni kuwa kama serikali ya rais Kikwete iliweza kuona hatari na ubaya wa rushwa kinadharia namna hiyo, basi tulitarajia kuwa pindi kashfa zile zilipoibuliwa, angetenda kulingana na uzito wake.

Hakufanya hivyo.

Matokeo yake ni kuwa Buzwagi imeendelea kuwa Buzwagi, Richmond imegeuzwa kuwa ajali ya kisiasa; wezi halizi wa fedha za EPA bado wako hewani na mashtaka dhidi yao hayajafunguliwa.

Sakata la Meremeta halijafunuliwa vema. Serikali haijasema, fedha zilikwenda wapi? Nani alisaidia kufanikisha wizi. Amechukuliwa hatua gani?

Nayo kampuni ya Tangold iliyochota kutoka BoT, mpaka sasa bado haijaguswa. Wakwapuaji wa mabilioni kupitia kampuni ya Deep Green Finance Limited, nao wanaendelea kutesa.

Kibaya zaidi, kampuni ya uwakili ambayo ndiyo iliyoshiriki kufanikisha wizi, imeajiri mtoto wa rais, Ridhiwani Kikwete, jambo ambalo linawapa wakati mgumu wakuu wa vyombo vya dola kuchukua hatua.

Nako kwenye halmashauri za wilaya hatua hazijachukuliwa, pamoja na kwamba mabilioni ya fedha yameyeyuka.

Kwa hakika, taifa hili halihitaji mnajibu wa kisiasa kuweza kutuambia kuwa CCM na serikali yake kwa miaka mitano iliyopita, wameshindwa kupambana na ufisadi kwa uzito unaostahili.

Si kwamba haijachukua hatua zozote kupambana na vitendo vya rushwa, hapana! Haijalipa suala la ufisadi uzito sahihi.

Kwamba bado CCM haijatambua kivitendo kuwa suala la rushwa ni la hatari kwa uwepo mzima wa taifa na vitendo vya ufisadi – ubadhirifu, undugunizationi, kuzungusha watendaji wabovu kutoka upande mmoja kwenda mwingine – ni mambo ambayo yamebarikiwa na watawala waliopo.

Kama serikali ya CCM ingetambua kivitendo ubaya wa vitendo vya ufisadi, meremeta isingefumbiwa macho; Tangold na Deep Green zingefunuliwa; sheria ya maadili ya viongozi ingefanyiwa marekebisho na TAKUKURU kingekuwa kweli chombo cha kupambana na rushwa.

Hata wahusika wa Kagoda na EPA wangetiwa pingu chini ya sheria ya uhujumu uchumi; wabadhirifu na maofisa wabovu waliochangia kuvunjika Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) wasingezawadiwa vyeo vingine.

Haya yote hayawezi kutokea na hayajatokea hadi hivi sasa si kwa bahati mbaya. Ni kwa sababu viongozi waliopo hawana ubavu wa kupambana na maovu.

Hawawezi, si kwa sababu hawana uwezo, si kwa sababu hawajui nini cha kufanya, na si kwa sababu hawana watu wenye uwezo wa kufanya kinachopaswa kufanya.

Hawezi kufanya kwa sababu itakuwa ni sawasawa na mtu kukata mkono unaomlisha au kukata tawi ambalo mtu amelikalia.

Mfumo uliopo sasa unawafaa wao na unawasaidia kuendelea kubaki madarakani; ukifumuliwa watapoteza uhai.

Hata hivyo, waamuzi wa mwisho siyo wao. Waamuzi wa mwisho siyo wa kina Yusuph Makamba na Kingunge Ngombale Mwiru.

Yule ambaye ameridhika na utawala wa miaka mitano iliyopita, anatakiwa kuwarudisha watawala wetu walioshindwa madarakani. Yule ambaye hajaridhika anajua la kufanya.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: