Ugunduzi wa EPA uanikwe sasa


editor's picture

Na editor - Imechapwa 15 July 2008

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

JANUARI 8, mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete aliunda timu maalum ya kufuatilia wahusika wa ufisadi wa mabilioni ya shilingi yaliyochotwa katika Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA), ndani ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Jumla ya Sh. 133 bilioni zilikwapuliwa huku maodita wa kimataifa wa Ernst & Young waliochunguza akaunti hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2005/06, wakitaja makampuni 22 yaliyohusika.

Timu hiyo inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika. Wenzake ni Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk. Edward Hoseah.

Rais aliipa timu hiyo miezi sita kukamilisha kazi yake na kutoa ripoti ili ukweli uelezwe. Alisisitiza kurudishwa fedha zilizoibwa na kuchukuliwa hatua za kisheria wale walioziiba.

Julai 9 ndiyo siku ya mwisho ya timu na sasa Watanzania wanatarajia majibu ya uchunguzi huo.

Kwa kuwa mwisho wa muda wa timu ilikuwa 9 Julai, wakati umefika ukweli kuelezwa pamoja na usiri mkubwa uliokuwepo tangu mwanzo.

Hatukuwahi hata mara moja kuridhia ubabaishaji wakati uchunguzi ukiendelea ndio maana hatukutilia maanani hata kauli ya Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, aliyoitoa bungeni mwezi uliopita kuwa fedha za EPA si za serikali.

Tuliidharau kwa kuamini ni yake mwenyewe. Msingi wa imani yetu hiyo ni mmoja tu: imetofautiana kwa mbali na taarifa makini aliyoitoa Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo alipotoa tamko la Rais Kikwete kuhusu matokeo ya ukaguzi wa EPA.

Luhanjo alisema fedha za EPA ni za serikali zilizohamishiwa Benki Kuu baada ya kuwa chini ya Benki ya NBC tangu miaka ya 1980.

Na hiyo ilikuwa ni kuungana na msimamo wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali, Ludovick Utouh, aliyethibitisha ugunduzi wa maodita katika EPA baada ya kupitia ripoti yao kabla hajapeleka maoni yake kwa Rais.

Tunatoa kilio cha umma bila ya kupapasa maneno, kwamba Watanzania wanataka taarifa ya uchunguzi wa ufisadi wa fedha zao. Wanataka taarifa yenye ufasaha katika kubainisha hatua zilizochukuliwa dhidi ya wahusika na ufisadi huo.

Changamoto iliopo kwa suala hili ni kwa serikali kujivua gamba chafu linaloizunguka taswira yake, wakati huu inapotumiwa lawama nyingi kwa namna uongozi wa juu unavyokalia taarifa au ripoti za Kamati za Uchunguzi.

Yaliyoisibu serikali kuhusu kamati nne zilizopata kuchunguza sekta ya madini nchini yanatosha. Uchunguzi unakosa mantiki iwapo kilichogunduliwa, kinafichwa. Lazima kitolewe ili kurekebisha kasoro zilizogunduliwa.

Wananchi wamekaa kwa shauku kusikiliza sauti ya serikali inayojiamini inavuma kwa mshindo baada ya kimya cha muda mrefu? Tuambiwe nani walichukua fedha? Wamezipeleka au kuzitumia vipi? Tuambiwe wamechukuliwa hatua zipi?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: