Uhafidhina umewakimbiza kwenye mdahalo


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 15 September 2010

Printer-friendly version
Tafakuri

KATIKA maisha ya binadamu, mabadiliko ya kimaendeleo yanayosukumwa na nguvu za mabadiliko ya sayansi na teknolojia humlazimisha kubadili mbinu na mikakati ya kutawala maisha yake.

Ni vigumu kwa binadamu kujifungia ndani ya boksi wakati dunia au tuseme mazingira yanayomzunguka yakibadilika kwa kasi kubwa, ndiyo maana watu wanaokuwa wa kwanza katika ugunduzi wa kitu chochote changamoto yao kubwa imekuwa ni jinsi gani watabakia kwenye nafasi hiyo ya kwanza.

Bila kuwa na ubunifu na kukubali changamoto mpya na kuzifanyia kazi, inawezekana kabisa aliyekuwa amepiga hatua nzuri za maendeleo akabakia hapo alipo akijivunia historia tu, lakini kwa wakati uliopo akawa hana nguvu zozote za kuhimili mabadiliko na hivyo kumezwa na ushidani.

Ukitazama kwa makini, taifa sasa lipo katika kampeni za Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 31, 2010. Nchi kwa sasa imechemka, wapo wagombea saba wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , na msururu wa wanaowania ama ubunge au udiwani..

Kwa miaka mingi Tanzania imekuwa na mfumo wa kampeni wa wagombea kuitisha mikutano ya hadhara kwa ajili ya kunadi sera na mikakati yao kwa nia ya kushawishi umma. Mbinu hizi tungeweza kuziita mbinu za kizamani (traditional).

Kwa kawaida mbinu hizi zina faida na hasara zake; faida mojawapo ni mgombea kuonana ana kwa ana na wapigakura, kupanda jukwaani na kuzungumza mwenyewe moja kwa moja, ni fursa ambayo wapigakura huitumia kuwapima wagombea kwa kuwasikiliza.

Ni fursa ambayo mgombea anasema kile ambacho anakusudia kufanya, atafanyaje na kwa nini afanye hayo endapo atachaguliwa ama kuwa rais, mbunge au diwani.

Hata hivyo, mbinu hii ina changamoto zake, kubwa ya yote ni nadra sana kwa wagombea kutoa nafasi ya kuulizwa maswali. Kwa maana hiyo kinachotokea ni sawa na mahubiri tu.

Kwamba mgombea ndiye anayejua kila kitu, ndiye mzungumzaji tu, kwamba wananchi au wapigakura hawana nafasi ya ama kumhoji mgombea husika juu ya hizo zinazoitwa sera na kama zinaakisi mahitaji na matarajio ya wapigakura wa eneo husika.

Inawezekana mfumo huu wa mikutano ya jukwaani ulikuwa muhimu zaidi zama hizo wakati maendeleo ya njezo za mawasiliano yakiwa hajafikia hatua kama ya sasa. Katika dunia ya leo binadamu anapenda zaidi kuwa mshiriki katika kila kitu kinachohusu maisha yake na njia za kushiriki ziko nyingi na rahisi.

Ndiyo maana kuna vitu kama midahalo ya wazi, ambayo wagombea si tu wanashindana wao kwa wao kueleza watafanya nini kama watachaguliwa, bali pia hutoa fursa kwa wapigakura kuwahoji kwa kuwapima kwa pamoja wagombea katika mazingira ya aina moja.

Ni ukweli kutokana na tofauti ya vyama kwa maana ya nguvu za kiuchumi na mikakati, si rahisi mikutano ya kampeni ya wagombea wote ikawa na wasikilizaji sawa, wingi wa wananchi katika mikutano ya hadhara ya kampeni inaathiriwa na mambo mengi.

Wingi huo unaweza kuwa ni kwa sababu ya umaarufu wa mgombea; inaweza kuwa ni kwa sababu ya umaarufu wa chama lakini pia inawezakana ni matokeo ya mbinu nyingine kama vile uwezo wa kuwasafirisha wananchi au wanachama kutoka sehemu moja hadi nyingine.

Kwa hali hiyo ubora wa mgombea kupimwa kwa mikutano ya hadhara tu inaweza kuwa si njia nzuri sana ya kutafuta kiongozi bora.

Ni kwa maana hiyo, watu katika zama za sasa wangetarajia kuona mfumo wa midahalo ya kwenye televisheni ukichukua nafasi kubwa zaidi kwa maana ya kuwapima wagombea.

Ni jambo la bahati mbaya kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho katika mchakato wake wa kura za maoni kilipanga utaratibu mzuri kabisa wa wanachama wake kuwatambua wote waliokuwa wanatafuta tiketi ya chama hicho kuteuliwa kuwa wagombea ubunge kwa kuwahoji, ndicho kimekimbia utaratibu wa midahalo.

Hofu hii ya CCM kuwakataza wagombea wake wa ngazi ya ubunge kushiriki midahalo ni mwendelezo wa maamuzi ya mgombea wao wa urais, Rais Jakaya Kikwete kukataa pia mdahalo na wagombea wengine wa ngazi hiyo.

CCM inajigamba kwamba wana njia nyingine mbadala za kuwafikia wanachama wake katika kusaka kura, mojawapo wanasema ni mikutano ya ndani, mikutano ya nyumba kwa nyumba na mikutano ya hadhara.

Ukitafakari kwa makini mbinu zote CCM inazotambia ni traditional. Ni taratibu ambazo hazimbani mgombea kuwajibika kwa wapigakura, hakuna kuhojiwa na kuelezwa matarajio ya wananchi/wagombea.

Mdahalo kwa kawaida ni fursa mojawapo muhimu ya kupima uwezo wa mgombea, je, anayatambua mambo kwa kiwango gani; je, anaelewa shida na mahitaji ya wapigakura kwa kiasi gani na ni kwa kiwango gani anasikiliza na kupokea changamoto nje ya zile anazojua yeye?

Kwa mara ya kwanza wagombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walifanya mdahalo mwaka 1995 wakati wa uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi. Walioshiriki mdahalo ule walikuwa ni mgombea wa CCM, Rais Benjamin Mkapa; mgombea wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba; mgombea wa UDP, John Cheyo na mgombea wa NCCR-Mageuzi, Augustine Mrema.

Watu wengi walisema Mrema alishindwa urais kwenye mdahalo ule; umma ulitambua uwezo wake wa kutambua mambo, nguvu zake za hoja na changamoto zake za kiongozi.

Ukweli wa mdahalo hauwezi kupuuzwa kokote duniani, kwa mfano nchini Uingereza katika uchaguzi mkuu uliomalizika hivi karibuni, mdahalo uliokutanisha viongozi watatu wa vyama viliovyokuwa vinasaka ridhaa; Labour, Gordon Brown; Conservative, David Cameron na Liberal Democrats, Nick Clegg, ndio ulimuongezea chati Clegg kiasi cha kuja kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na Cameron baada ya Conservative kuongoza kwa idadi nyingi ya viti vya wabunge.

Ni aibu kwamba CCM inakosa ujasiri wa kukabiliana na changamoto za midahalo kiasi cha kuingiwa na kiwewe hadi kufikia hatua ya kuwapiga marufuku wagombea wake kushiriki katika midahalo hiyo kwa kutoa sababu nyepesi mno.

Wakati CCM ikiwapiga marufuku wagombea wake kushiriki mijadala hii ya wazi, inatarajia kutoa viongozi hodari wanaoweza kumudu changamoto za sasa katika ushindani wa kila kitu.

CCM inatumia fedha nyingi mno kwenye kampeni kwa vitu ambavyo katu haviwapi wananchi nafasi ya kupima nguvu na uwezo wa wagombea wake, vitu kama mabango, fulana, kofia havimuunganishi mpigakura na mgombea.

Hata mikutano ya hadhara mara nyingi haitoi nafasi ya mjadala. Ni mahubiri ya upande mmoja tu. Wenye uelewa wao walidhani kwamba mdahalo ni fursa nyingine ya kukua kisiasa na kidemokrasia, lakini kwa wahafidhina ni njia ya kukwepwa kwa sababu inawafungua na kuwapa nguvu ya maamuzi wapiga kura, hizo ndizo fikra za Yusufu Makamba, Katibu Mkuu wa CCM, wafunge kifikra ili tuwatawale. Huu ni uhafidhina na kwa zama za sasa utashindwa tu.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: