Uhalali serikali ya JK ni wa kura tu?


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 18 April 2012

Printer-friendly version
Tafakuri

PROFESA Dani Nabudere Wadada ni miongoni mwa wasomi wachache ambao bara la Afrika lilipata kuwa nao. Msomi huo raia wa Uganda katika miaka ya mwanzoni mwa 1990 alikuwa miongoni mwa wanazuoni kutoka pande zote za dunia, waliokutana Dar es Salaam kujadili hatima ya siasa za kijamaa.

Halikuwa suala dogo kwa wanazuoni wa kijamaa kama akina Profesa Wadada kuona ngome ya kijamaa iliyokuwa inaongozwa na Shirikisho la Dola za Kijamaa za Kirusi (USSR) ikifikia ukomo, hasa baada ya kusambaratika na kuibuka kwa mataifa huru yaliyokuwa yanaunda dola ya USSR.

Kusambaratika kwa USSR kuliibua mahusiano mapya ya kimataifa na kijamii duniani kote, dunia iligeuka kutoka iliyokuwa imegawanyika katika kambi mbili kuu, mashariki na magharibi, ile ya mashariki ilikuwa ni ya kijamaa na iliongozwa na Urusi na magharibi kinara wao alikuwa Marekani na ilijiegemeza kwenye mfumo wa kibepari.

Ingawa mkutano ule ulionekana kama ni wa kujadili mfumo wa kijamaa ambao tayari ulikuwa umeshindwa na kwa kweli kufa, wanazuoni wengi walioshiriki mkutano ule walikuwa na sababu zao za kufikiwa mwisho kwa kambi ya mashariki.

Mengi yalizungumzwa, lakini ninachokumbuka hadi leo ni kauli ya Profesa Wadada ambaye alisema “tunaishi katika kipindi cha kutokufuata sheria (lawlessness), ni kipindi cha kukosoa kila kitu; kataeni kila kitu; hakuna kutii kitu na hakuna mfumo uliosimama kwa sasa.”

Wakati Wadada anatoa kauli hii, alikuwa anasumbuliwa na kitu kimoja kwa mawazo yangu nilivyomuelewa. Ni kipindi ambacho dunia ilikuwa imegeuka na kuanza kutambua na kuheshimwa kwa haki za raia kwa kiwango cha juu zaidi, ni kipindi nguvu na mamlaka za kiimla zilikuwa zinakabiliwa na changamoto kubwa ya nguvu ya umma.

Ndicho kipindi madai ya demokrasia pana zaidi yalikuwa yanatikisa dunia. Ni kipindi ambacho mataifa yaliyokuwa yanafuata mfumo wa chama kimoja cha siasa yalikuwa yanapambana na wanaharakati waliokuwa wanadai vyama vingi vya siasa, ushiriki mpana zaidi wa wananchi katika kupanga na kuamua mambo yao.

Hali hii hata hivyo haikuiacha Tanzania kando, nayo ilikumbwa na msukosuko hadi pale ilipoundwa Tume ya Jaji Francis Nyalali kupata maoni ya wananchi kama Tanzania ingefaa ifuate mfumo upi wa kisiasa, wa chama kimoja au vyama vingi. Matokeo ya Tume ile yalikuwa wazi mwaka 1992 na mengine yanabaki kuwa historia.

Chini ya mwavuli wa uhuru zaidi kwa wananchi, chini ya harakati za kudai haki zaidi na kwa kweli mataifa yaliyokuwa yanafuata mfumo wa chama kimoja ambao kimsingi ni wa kiimla, aina mpya ya utawala iliibuka katika mataifa haya.

Tanzania haikukwepa hali hii. Leo tunapojitazama tunajikuta tukifanana na kile alichosema Profesa Wadada “kosoa kila kitu.”

Ingawa ukosoaji ni siha kwa afya ya kisiasa na uwajibikaji wa viongozi, na pengine kujenga mfumo wa uwajibikaji kwa ujumla wake, hapa kwetu mfumo huo umezaa aina mpya ya uongozi; tumezaa viongozi dhaifu, waoga wa kuchukua hatua na kwa kweli niseme tu wazembe kutekeleza wajibu wao kwa kuwa wanachojali wao si uwajibikaji tena, ila kutafuta kuungwa mkono na umma hata kama hawana wanachofanya. Nitafafanua hali hii.

Ukitazama kila kitu kinachotokea nchini, utagundua kuwa mambo hayaendi kwa sababu kuna mtu au kikundi cha watu kimeamua kuacha kuchukua hatua. Hawachukui hatua kwa sababu mbili kubwa, moja ama wanaogopa kuudhi watu, na kwao watu maana yake ni kura kila baada ya miaka mitano; mbili hawajui cha kufanya na wana mbinu za kubakia madarakani, fedha.

Ukimtazama kwa mfano Waziri Mkuu Mizengo Pinda huna sababu hata moja ya kutoshuku kwamba ni mfano mmojawapo wa aina ya watu wanaoacha kuchukua hatua kwa sababu ya ama woga au matarajio ya baadaye ya kisiasa ambayo leo hayako wazi sana.

Tujiulize mambo mawili tu kuhusu maamuzi ya waziri mkuu juu ya serikali kupunguza matumizi, Pinda alisema, ununuzi wa magari ya kifahari maarufu kama mashangingi umepigwa marufuku hadi kwa kibali maalum. Je, ni kweli kuna utekelezaji wowote wa suala hili? Ukweli ni kwamba leo serikali inamiliki mashangingi makubwa makubwa kuliko ilivyokuwa kabla ya Pinda kutoa agizio lake. Naamini hata sasa hivi mengine yako kwenye meli bahari kuu kuja nchini. Hakuna kitu.

La pili semina. Pinda alipiga marufuku semina na makongamano ya kila wakati ya watumishi wa serikali. Je, vimepungua kwa kiasi gani? Je, uwajibikaji ndani ya serikali umeongezeka zaidi baada ya katazo hili la Waziri Mkuu? Jibu ni jepesi tu, kila siku iendayo kwa Mungu sasa semina na mikutano ya kikazi nje ya ofisi za umma vimekuwa ni fasheni.

Ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 2011, umethibitisha kwa mara nyingine tena kuwa hakuna udhibiti wa maana katika matumizi ya fedha za serikali, Halmashauri zimezidi kutafuna fedha za wananchi, mishahara hewa bado inalipwa takribani mishahara hewa ya Sh. bilioni moja imelipwa katika halmashauri pekee bila kutaja serikali kuu, deni la taifa si tu linaongezela ila kasi ya ongezeko lake ni ya kupaa.  Kwa mfano wakati deni la taifa mwaka 2009/10 lilikuwa Sh. 10.5 trilioni, mwaka 2010/11 lilipaa hadi kufikia Sh. 14.4 trilioni.

Hali hii ikitazamwa na kuangazia misamaha ya kodi ambayo sasa imefikia Sh. 1.02 trilioni sawa na asilimia 18 ya mapato yote ya ndani. Kwa maneno mengine ni kwamba misamaha hiyo iliyotolewa kwa taasisi mbalimbali yenye thamani ya Sh. 1,016,320,300,000  sawa na asilimia 18 ya makusanyo yote ambayo ilikuwa ni Sh. 5,550,205,244,378, ni mkubwa ukilinganisha na viwango vya misamaha ya kodi vinavyotolewa kwenye nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda.

Hali hii haionyeshi kwa vyovyote kuwa sisi ni taifa linalojali, linaloongozwa hata kwa kuzingatia matamko yake yenyewe. Ndiyo maana nilimtaja Waziri Mkuu kuwa kauli zake za kubana matumizi kwa hakika hazina maana yoyote kwa taifa hili kama hali halisi ya mambo ndiyo ilivyo sasa.

Inawezekana kama alivyosema Profesa Wadada kwamba tuko katika kipindi cha kuyumba kwa mifumo, na kwa kweli labda kwa sheria kuwekwa pembeni kwa kisingizio cha uhuru, haki na kila aina ya kisingizio cha demokrasia, lakini kitu ambacho kinaonekana kuwa dhahiri ni kwamba mfumo wa sasa umeruhusu sana kuwa na viongozi dhaifu wasiojali. Matendo yao mara zote yamegongana na kauli zao, wameshindwa na hawana jipya wawezalo kuleta, wapo tu kwa kuwa wamehakikishwa kura iwe kwa haki au kwa ghilba ya fedha.

Kila nikitafakari hali ya mambo ulivyo sasa nchini, mfumuko wa bei, deni la taifa, kudorora kwa thamani ya sarafu yetu na ukiwatazama viongozi, kimsingi kuanzia juu kabisa kwa Rais, Makamu wake, Waziri Mkuu na mawaziri wote, nahofu kusema wote wamefika ukingoni kiasi kwamba sasa wanaamini tu katika kitu kimoja, “tulichaguliwa kwa njia ya kidemokrasia kwa maana hiyo tuna uhalali wa kuendelea kutawala hata kama tameshindwa kazi.”

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: