Uhuni nyumba za NSSF


Jacob Daffi's picture

Na Jacob Daffi - Imechapwa 02 November 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

JE, unataka nyumba ya kupanga kati ya zilizojengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF)? Usiende kwao. Njoo uniulize nitakusaidia.

Ukienda kwao utajisumbua bure. Watakwambia uandike barua, uwapelekee. Tena watasema uichape kwenye kompyuta ili wasipate tabu kusoma.

Hata ukiandika kwa maandishi manene au makubwa au kwa wino uliokoleza au ukajaza fomu waliyoandaa unajisumbua bure. NSSF wanajenga nyumba lakini hawamiliki nyumba hizo.

Usishangae. Andika barua uwapelekee. Utasubiri majibu miaka nenda miaka rudi hutapata nyumba. Ukisema ufuatilie unapoteza fedha bure. Wanaomiliki nyumba za NSSF ni wajanja wa mitaani – ‘misheni tauni’.

Unataka kuthibitisha? Nenda Masaki utaona nyumba zao. Baadhi ya nyumba ziko wazi, hazina wapangaji. Lakini usifunge safari kwenda NSSF unajisumbua bure. Wamejaza majina ya wapangaji wa uongo.

Utaugua bure ugonjwa wa moyo ukiambiwa wamiliki wa nyumba wakati ukweli wanaishi kwenye majumba yao ya kifahari kwingineko. Hujaelewa? Wale wanaotambuliwa na NSSF kama wapangaji sio wanaokaa.

Wanasiasa maarufu wenye nyumba kibao katika majiji ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Morogoro, Tanga ndio eti wamepanga. Majina yao yako NSSF. Wanasheria maarufu eti ndio wapangaji wakati wanaishi kwao.

Nasema hivi kwa uzoefu. Baada ya raia mwema, tena ndugu yangu ndani ya NSSF kuniuma sikio kwamba ameona watu wakihama Masaki tena kwa majina Block A na Block B nilipiga kiguu na njia kujionea. Nilifika nikashuhudia nikapata uhakika. Nikapiga picha kwa uthibitisho. Nikaamua kwenda NSSF kuona kama jina langu limesogea. Nilipigwa butwaa.

Nilikutana na mpasha habari wao. Akanihubiria sana. Akanieleza ambayo sikutaka kusikia. Akaeleza kuwa utaratibu wa upangishaji wa vyumba maeneo kama ya Masaki, hufanyika kipindi ambacho kuna uhitaji mkubwa wa nyumba hizo.

Akaongeza, kama mtu anataka kupanga inabidi aandike barua ya kuomba kupanga, na kama ikitokea mpangaji mwingine anahama au mkataba wake umeisha, ndipo nafasi hutolewa kwa mwombaji ambaye hupewa eneo hilo na kuingia mkataba ambao kodi hutozwa kila baada ya miezi mitatu.

Akasema maeneo hayo ambayo ni maalum kwa kupangisha hutofautiana kwa bei. Akanipa mifano. Eneo la Mikocheni wapangaji hutozwa kodi ya dola 800 (Sh.1.2m) mpaka 1200 (1.8m).

Masaki hutozwa kiasi cha Sh 500,000 na maeneo ya Mbezi kiasi ni Sh. 350,000.

Nikamwambia hilo si tatizo langu. Nikamwambia nimethibitisha pasi na shaka wapangaji wamehama nyumba za Masaki. Nikamtajia nyumba za Block A na Block B.

Alipochungulia katika orodha ya wapangaji akaona jina la mtoto wa kiongozi mstaafu Afrika na jengo jingine akaona jina la mwanasheria maarufu. Wameandikisha kampuni zao. Kampuni zao ndizo zimepanga.

Katika nyumba ambayo linaonekana jina la mtoto wa kiongozi mstaafu Afrika wiki iliyopita wamehama madaktari Wafilipino na kabla yao walikuwepo madaktari kutoka Cuba.

Majina ya wapangaji Wafilipino na Wacuba hayako NSSF, liko jina la mtoto huyo. Alipanga miaka mingi iliyopita. Naye anapangisha watu. Wanamlipa yeye. Wakihama anaingiza wengine, wanamlipa yeye dola halafu ‘chenji’ au ‘cha juu’ anapeleka fedha za madafu NSSF.

NSSF wanajua mchezo huu mchafu. Wanajua watu wanaocheza ‘dili’ hili lakini wanafumbia macho kwa vile ni watoto wa wakubwa.

Wamiliki wa nyumba hizi wanatoza kodi hadi dola 900 sawa na karibu Sh. 1.35m badala ya Sh. 500,000 tu.

NSSF wanajua mchezo huu mchafu, wanawajua na ‘misheni tauni’ hawa lakini wamekaa kimya. Wanakiri wanajua. Wanajitetea kwamba wamewahi kuvamia mara nne katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita na kuwatoa.

Ukweli hawajagusa nyumba za Masaki kwa vile wana maslahi. Meneja wa majengo hashtuki kuona aliowapangisha sio wanaoishi? Hashtuki kuona aliyeandikisha jina ni Mswahili tena Mhaya, Mmatumbi, Mnyalukolo, Mkurya lakini waliomo ni Wacuba? Kama ni jamaa zake mbona anawatoza zaidi? Kama ni washirika kibiashara jijini mbona anatoza zaidi ya kinachotakiwa? Hata wakubwa wanaishi kwa misheni tauni?

Nikamfuata mkubwa wao akasema, hawana tatizo na wapangaji wanaolipa. Hata hizo mara nne katika miaka mitatu walipovamia walilenga kuwatoa nje wasiolipa, siyo misheni tauni.

0
No votes yet