Uhuni umeangamiza mataifa mengi


Mwandishi wetu's picture

Na Mwandishi wetu - Imechapwa 14 December 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

KIONGOZI anayeiita Tanganyika kwa jina la Tanzania Bara anafanya uhuni. Tanganyika, kama ilivyo Tanzania ina sehemu ya bara, pwani na visiwa.

Hivyo basi, kuita Tanganyika kuwa ni Tanzania bara ni upotoshaji mkubwa. Wanaoita hivyo wanaitenga mikoa ya pwani na visiwa.

Mara zote tawala zinapoelekea ukomo hufanya uhuni mwingi. Haya tumeyasoma katika vitabu vya historia. Mfano hai ni ulivyokuja kuanguka Utawala wa Kirumi ulioitikisa sana dunia.

Kati ya mambo ambayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alikemea vikali ni uongozi wa kihuni. Mwaka 1995 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, ikiwa ni miaka 10 tangu ang’atuke urais, alitoa tamko zito.

Alisema, “Ukipewa kazi ya nchi, lazima ujiheshimu. Huwezi kupewa kazi ya nchi halafu unaishi kihunihuni. Kazi za kihuni ziko tele. Nenda kafanye uhuni wako kule. Nchi zote zina miiko ya uongozi. Hapa kwetu hatuna. Wameiacha miiko ya Azimio la Arusha, hawakuweka miiko mingine. Sasa ni holela tu”

Ukiyatafakari maneno haya utagundua kuwa Mwalimu Nyerere anaposema, ‘sasa ni holela tu’ kwakweli anasema, ‘sasa ni uhuni tu’. Uhuni siku zote ni holela. Ana maana gani anaposema ‘nchi zote zina miiko lakini hapa kwetu hakuna’. Tuna uongozi wa aina gani hapa kwetu kwa fikra za Nyerere?.

Wataalam wa falsafa wanasema, “Kusema ni kukiri na kukana kwa wakati mmoja.” Kama ni kweli wameiacha miiko ya Azimio la Arusha halafu hawakuweka miiko mingine na kwakuwa nchi zote duniani zina miiko, basi alichosema hapa Baba wa Taifa ni kwamba, uongozi wa nchi yetu tangu kuuawa kwa Azimio la Arusha ni wa kihuni tu.

Haya si maneno yangu. Natafakari tu maneno ya Baba wa Taifa. Siku hizi, ili kuzima kalamu na makala za ukosoaji, watalawa wameongeza neno ‘uchochezi’. Hiki ndiyo kizingizio chao kikubwa katika kampeni za kunyamazisha sauti huru za wanyonge kwenye vyombo vya habari.

Kikiandikwa kitu wasichopenda kukisoma au makala zinazochochea uelewa mpana, hutumia dola kutia ndani waandishi na wahariri.

Kuna viongozi waliingia madarakani huku wakitangaza mali zao, lakini walipoondoka hawakueleza waliondoka na nini. Je, ni kwa vile waliondoka na mali nyingi zaidi zisizo na maelezo?

Wengine hawajatangaza mali zao. Inawezekanaje mali waliyopata kihalali washindwe kuitangaza? Lakini, mali ya wizi wataitangazaje? Hii ni dosari ya uongozi na angekuwepo Mwalimu Nyerere leo angeita uhuni.

Lakini dosari kubwa, ambayo Mwalimu alithubutu kwa nafasi yake kuita ni uhuni ni kuendesha nchi bila kuwa na miiko ya uongozi.

Hivi, bila miiko ya uongozi tunaiendeshaje nchi? Je, tukubaliane na fikra za Mwalimu Nyerere kuwa tangu kufutwa kwa Azimio la Arusha tumekuwa tukiongozwa kihuni?

Jambo jingine ambalo Mwalimu angekemea vikali ni namna ulivyoendeshwa mchakato wa kupata katiba mpya. Kwamba Nyerere alifanya hivi, Mwinyi alifanya hivyo hivyo, Mkapa na sasa mimi nimefanya hivyo hivyo si utetezi wa maana.

Nyerere alikiri kwamba katika kipindi cha miaka 25 ya uongozi wake, wamefanya makosa hasa ikizingatiwa walipoingia madarakani hawakuwa na utaalamu wa kutosha wa uongozi.

Ndiyo maana yeye alifuta vyama vingi na mgombea binafsi, lakini uliporejeshwa mfumo huo mwaka 1992 alilaumu kitendo cha serikali kuzuia haki ya mgombea binafsi akisema wamefanya kosa la kimsingi.

Kwa hiyo, nafasi ya makubaliano na maridhiano juu ya sheria ya marekebisho ya katiba imefutwa na watawala. Rais Jakaya Kikwete amekiri kwa moyo wake kuwa kuna mapungufu makubwa yaliyojitokeza, alipokutana na viongozi wa ngazi ya juu wa CHADEMA, lakini akausaini muswada huo ili uwe sheria.

Rais Kikwete aliusaini muswada huo halafu akaanzisha mchakato mwingine wa kutafuta maoni mbalimbali ya kuirekebisha sheria hiyohiyo. Kwanini?

Kwa mtindo huu, katiba yenyewe itakuja kupatikana lini? Ni kweli asiye na bahati habahatishi. Rais wetu amepoteza nafasi ya dhahabu kwani kukataa kusaini kungeliweka jina lake katika kumbukumbu njema ya wanawema wa nchi hii.

Hata hivyo, hatua ya kusaini kunawasukuma wananchi kuyaamini maneno ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwamba nchi itaingia katika machafuko tukikubali uhuni!

Mwadhama Polycarp Kadinali Pengo ni mmoja kati ya viongozi wa nchi hii wenye wafuasi wengi sana. Kwa nafasi yake, kama mkuu wa taasisi mojawapo kubwa, kumpatia siku nne tu kutoa maoni kuhusu jambo kubwa kama kuandika katiba mpya haipendezi.

Hakupewa nafasi iliyotosha kutoa maoni ya Kanisa. Sasa Kanisa limekataa kuburuzwa! Limesema halitakaa kimya kuona nchi inawekwa rehani. Waumini wa dini zingine nao wakikataa kuburuzwa amani ya nchi itabaki vipi? Ni hatari kwa mustakbali wa taifa kudhani kuwa katiba ya nchi inaweza kuandikwa bila kuzingatia maoni ya waumini wa dini zote.

Nyerere amesema kazi ziko tele. Ukipewa kazi ya nchi lazima ujiheshimu. Wanaopuuza ushiriki wa wananchi na wayatafakari maneno haya! Mara nyingi uongozi ndiyo umekuwa chanzo cha mifarakano mingi katika nchi yetu!

Waliosema katiba ya wananchi itapatikana kwa mapambano hawakuwa wanachochea. Ndiyo inaweza kuwa hivyo, kwakuwa wajinga wanazidi kupungua.

Sasa imethibitika bila kuacha shaka yoyote kuwa ili amani ya kweli iendelee kutamalaki katika nchi yetu Azimio la Arusha ni lazima liwepo. Uongozi holela sasa basi. Madhali mbio za urais zimekwisha kuanza, ni muhimu kwa yeyote anayetaka kuwa rais akalizingatia hili.

0713334239 ngowe2006@yahoo.com
0
No votes yet