Uhuru gani anaolenga Dk. Mwinyihaji?


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 23 March 2011

Printer-friendly version
Kalamu ya Jabir

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Mwinyihaji Makame Mwadini anajidanganya. Nahofia anaishi ndotoni. Kwamba ingawa anaishi leo, anawaza maisha ya jana. Haiwezekani.

Anaposema serikali inathamini misaada ya nchi wahisani, zikiwemo za Ulaya (EU), lakini akazionya zisiingilie alichokiita “Mambo ya utendaji wa serikali,” hakika daktari anapotea.

Kwanza, hawa si ndio wale ambao siku hizi watawala wanawaita “washirika wa maendeleo?” Mshirika maana yake ni mtu mnayeshirikiana kimaslahi. Sasa washirika wasihoji kitu wakati wanaisaidia Zanzibar?

Lakini pili, hiyo jeuri ya kuwaambia washirika wasiingilie mambo ya nani ya utendaji, imetoka wapi katika nchi ambayo uhai wake unategemea sana misaada na mikopo ya haohao “washirika wa maendeleo?”

Dk. Mwinyihaji ni mwanataaluma anayejua namna serikali za Ulaya zinavyosaidia sekta ya kilimo tangu akiwa wizara ya kilimo, mifugo na maliasili. Nakumbuka Uholanzi kwa hifadhi ya mimea, Finland kwa uendelezaji misitu.

Daktari huyu anajua namna mashirika ya kimataifa ya misaada kama FAO, IFAD na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) yalivyosaidia hapo.

Lakini je, anaweza kusema leo tija ya misaada ile iko wapi? Anaweza kusema kile kilichoitwa, “MTAKULA” kiliishia wapi? Anaweza kusema walipo wale maelfu ya ng’ombe wa kizungu waliokuwa shamba la Bambi? Aseme leo kilimo cha mpunga wa kumwagilia kilipofikia.

Haya naona ndiyo mambo ya kufuatiliwa. Kumbe madaktari serikalini – hasahasa hawa waliopata vyeo vya kisiasa – wanafikiria maendeleo yepi?

Nilidhani watajiegemeza kwa shughuli walizokusudiwa kuzifanya kama zilivyotajwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinachoshika dola. Kumbe sivyo. Hayupo peke yake.

Miezi kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010, aliibuka kwa staili hiyohiyo Hamza Hassan Juma, aliyekuwa waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi. Aliwafyatukia wahisani eti waiachie Zanzibar ifanye mambo yake inavyojua na kutaka.

Wakati huo alikuwa anajua nchi kama Norway ilikuwa inafadhili mradi mkubwa wa kujenga miundombinu ya kusafirisha umeme unaotokana na nguvu ya maji ya Mto Pangani, mkoani Tanga, kuupeleka Wesha, kisiwani Pemba.

Norway ilitoa dola 72 milioni kuugharamia mradi huo, huku serikali yenyewe ikiishia kutoa dola 10 milioni tu! Nayo serikali ya Muungano ilitoa dola 5 milioni kugharamani mradi huo. Uko wapi uwiano?

Halafu useme Norway wanyamaze wanapoona serikali inatumia vibaya fedha za umma zikiwemo za wahisani. Waachwe viongozi wazitapanye kufanikisha safari zisizo tija na kuhudumia miradi ya kifisadi. Haikubaliki.

Sasa ugomvi ni serikali ya Norway kusaidia ukuaji wa demokrasia Zanzibar. Wametoa fedha kwa ajili ya elimu ya uongozi mwema unaoheshimu misingi ya utawala bora kwa masheha – viongozi wa ngazi ya chini serikalini.

Pamoja na kutambua mchango wa Denmark katika nyanja hiyo, daktari alipokuwa akifungua mafunzo hayo wiki iliyopita, akasema, “Lakini chondechonde wasiingilie mambo yetu ya ndani.”

Lakini, daktari anajua wajibu wa serikali kuongoza kwa misingi ya utawala bora hasa wakati huu ikishikwa na vyama viwili – kikiwemo Chama cha Wananchi (CUF) kilicho hasimu mkubwa wa CCM. Vyama hivi vinaongoza Serikali ya Umoja wa Kitaifa. Huko nyuma ilishindwa.

Na kufikia maendeleo ya kweli hakuji kwa ahadi tu kama Dk. Mwinyihaji na wenzake wanavyoshawishi watu kuamini. Ile anayoiita dhamira ya serikali kulinda amani na utulivu na kuinua maendeleo ya watu, haiji tu kwa kutamka. Inataka uongozi bora.

Dk. Mwinyihaji aliyekuwa waziri wa nchi anayeshughulikia fedha, chini ya rais Amani Abeid Karume hadi Oktoba 2010, anatakiwa kumsaidia waziri wa fedha wa sasa, Omar Yussuf Mzee, kutambua kilichokwamisha kasi ya ukusanyaji mapato. Anajua.

Ukusanyaji mapato ni eneo moja muhimu linalohitaji mapinduzi ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa Zanzibar, nchi inayokabiliwa na mzigo mkubwa wa kugharamia shughuli za utawala kutokana na hatua ya rais kuunda serikali kubwa kupindukia.

Dk. Mwinyihaji alipokuwa waziri wa fedha jinsi serikali ilivyoshindwa kukusanya mapato. Mengi yalivuja. Naapa anajua.

Chini yake, wafanyabiashara wachache walijipa utukufu. Wakaachiwa kuhodhi biashara, kuleta bidhaa mbovu zikiwemo vyakula na wakasakama watendaji wa serikali waliosimama imara kuwadhibiti. Anajua.

Anajua namna gani fedha za serikali zilichotwa na kuingizwa kwenye siasa kwa ajili ya kunufaisha chama chake. Masheha ambao leo wanapewa dozi kujua utendaji mwema, walihusika sana kuvuruga amani mitaani. Daktari anajua.

Sasa akubali huo ulikuwa uongozi mbaya; ulikiuka misingi ya utawala bora. Palikuwa na uongozi usiozingatia shida za wananchi, bali uliojaa viongozi walafi na mafisadi.

Hapo unakataaje kuchungwa? Kiongozi mwenye msimamo kama huo, ndio mhafidhina. Na ikiwa yeye na wenzake serikalini wanaamini hivyo, basi wote wanadanganya umma na ulimwengu kudai wamekusudia “kupiga hatua ya maendeleo inayoendana na mabadiliko ya kisayansi na kiteknolojia duniani.”

Mafanikio hayo yanataka nguvu za pamoja: kwanza za serikali yenyewe; bali pia nguvu za wananchi na wahisani, makundi muhimu sana. Mafanikio hayo yanadai utendaji uliotukuka. Utendaji adili. Jeuri si sehemu yake.

Viongozi wa Zanzibar wajue wana mafunzo ya kutosha. Wapo katika kipindi cha ukweli tu. Wanachotaraji ni kuiona serikali yao inatekeleza kazi za umma kwa kutumia uzoefu uliopatikana awamu zilizopita. Hapo, hakuna njia ya mkato bali uwajibikaji.

Oneni somo muhimu: Libya inabanwa na kinachoitwa jumuiya ya kimataifa iheshimu raia zake. Imefikia hata kufungiwa anga yake kwa hofu kuwa inaitumia kurushia raia makombora yanayowaangamiza. Yaweza kuwa kisingizio tu.

Libya ni nchi huru. Tena imepiga hatua kubwa ya maendeleo. Inalisha ndani na kuuza bidhaa hadi Ulaya.

Kiongozi wake, Kanali Muamar Ghaddafi amejenga miundombinu imara ya kuchochea uchumi na huduma nzuri za jamii, tena bila malipo kwa wananchi. Angalia inavyobanwa!

Hakuna uhuru huo anaoulenga daktari. Kuwa huru kwa nchi lazima kuendane na uwajibikaji wa serikali kwa watu wake. Ni lazima haki za watu hao ziheshimiwe. Zinapotishiwa, dunia haikubali.

Kwamba nchi fulani ni huru na kwa hivyo isiingiliwe na nchi huru nyingine hata inapoumiza wananchi, ni kauli ya kisiasa zaidi kuliko mantiki.

Mfungamano wa umuhimu wa utu na haki za raia unalazimisha kila utawala kuchungwa kwa kiasi gani unaheshimu haki za binadamu ndani ya eneo lake.

Zanzibar si kisiwa. Inapaswa kuchungwa vilevilea maana Ulaya, Marekani na kwingineko wanatoa fedha kuisaidia ikue. Ukuaji unaotajwa ni ule ambao tija yake inaonekana hadi kwa mtu wa chini kabisa kiuchumi.

Matamko ya kufyatuka kama risasi ni upuuzi. Dawa ni serikali kuthibitishia wahisani na wananchi tija iliyopo kwa misaada iliyotolewa. Toeni ahadi ya kutimiza matumaini ya watu. Hili ndilo linalotia hofu wahisani. Na hata Wazanzibari wanalihofia.

0
No votes yet