Uhuru wa kutoa maoni siyo uhaini


M. M. Mwanakijiji's picture

Na M. M. Mwanakijiji - Imechapwa 30 December 2009

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

KUNA watu wanajaribu kuwafanya wengine wajisikie vibaya wanapotoa mawazo yao kuwa Rais Jakaya Kikwete afikirie upya azma yake ya kugombea ngwe ya pili.

Wanajaribu kuwafanya watu wajisikie kama wasaliti au waonevu wanapotoa mawazo kuwa taifa letu linahitaji uongozi mpya na siyo tena wa Rais Kikwete.

Tukiangalia kwa karibu tunaweza kuona kuwa kuna kundi la watu ambao wanatishika sana na uwezekano wa Rais Kikwete kutokugombea tena urais.

Kundi hili linataka watu wote tujipange mstari mmoja, na kama tuliolishwa limbwata la woga, tuanze kuimba wimbo wa “Kikwete tena, Kikwete tena.” Eti tusiwe na uhuru wa kusema tukitakacho.

Hapa tunaona kuna wanaompenda Kikwete kama mtu binafsi; mwenye sura nzuri, sauti nzuri, tabasamu na mengineyo.

Lakini linapokuja suala la uongozi, wapo wanaoona kuwa ana mapungufu makubwa mno kiasi kwamba kumpa nafasi nyingine mwakani ni kuendeleza kile ambacho tayari kimeshaonekana miaka hii minne; yaani udhaifu mkubwa wa uongozi wa taifa tangu uhuru.

Tunapoelekea mwaka huu mpya ambao ni mwaka wa uchaguzi kambi za "Kikwete agombee" na "Kikwete asigombee" zitazidi kuibuka na kwa mara ya kwanza tutashuhudia mgongano wa wazi kati ya kambi hizi.

Tatizo kubwa ni la wale ambao wanaamini kuwa kutaka rais aliyemadarakani asigombee tena ni sawa na uhaini na kumtaka afikirie kutokugombea ni sawa na kumsaliti.

Tumefikia mahali kuna watu wameibuka wakijipa uwezo wa kimungu na kuwatisha watu wengine kuwa wakitaka kugombea urais, basi watakufa.

Ni vema watu hawa wakarudi kwenye ramli zao uchwara na kama wanatoa sadaka kwa mashetani waendelee kufanya hivyo kwa maangamizi yao wenyewe kwani Mungu aliyeumba mbingu na dunia hasimamii udhalimu hata siku moja.

Na zaidi ya yote hatuna budi kuwakataa viongozi ambao kutokana na nafasi zao wanataka kutufanya Watanzania wote tuzungumze kwa kumung’unya maneno kuwa Kikwete agombee tena.

Hawa wanataka tujisikie vibaya kana kwamba tunachopendekeza ni kinyume na Katiba au tunataka kuleta matatizo nchini.

Hii si kweli. Rais wa Tanzania anachaguliwa kwa kipindi kimoja tu na akitaka nafasi nyingine basi anapitia mchakato uleule na hawezi kutawala kwa vipindi zaidi ya viwili.

Kutokana na ukweli huu ni lazima watu wakubali kuwa utawala wa demokrasia una gharama yake na gharama mojawapo kubwa ni wananchi kuweza kumkataa kiongozi wao na hata kutaka asigombee tena.

Lakini wazo hili ni gumu kwa watu ambao wanaongozwa na ushabiki wa mtu; wanaoona kuwa Kikwete "amefika" hapo kwenye urais; mtu yeyote anayetoa mawazo kuwa asigombee au hana sababu ya kutosha kugombea tena basi ni haini.

Tumewasikia watu wazima na ambao ni wanasiasa wakongwe wakianza kutukuza huu ubia kati ya Kikwete na urais wa Jamhuri.

Kinachokera zaidi ni ujasiri wa baadhi yao; wamefikia mahali pa kulitukana taifa zima kwa kudai ati “hakuna Mtanzania mwingine anayeweza kuongoza nchi hii kama Kikwete.”

Sijui hawa mashabiki wa uongo huu wamelishwa kungu zinazotoka miti gani maana kuna uwezekano wa ndugu zetu hawa kuwa katika hali ya upotofu wa kifikra wa kudumu.

Hivi kweli ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) hakuna mtu yeyote anayeweza kuongoza taifa letu vizuri zaidi kuliko Kikwete? Je, Kikwete akimaliza ngwe yake, CCM hawataweka mshindani? Au hata kwenye upinzani hakuna kiongozi bora?

Hivi kweli kati ya wanachama wote wa CCM ni Kikwete tu ndiye mwenye uwezo wa kutuongoza kuelekea mafanikio ya kweli na ndiye pekee anaweza kuthubutu kupambana kweli na ufisadi na kulielekeza taifa katika kujitegemea?

Wenye imani ya namna hii ni wale ambao wananufaika moja kwa moja na uongozi dhaifu wa awamu ya nne na ambao kuwepo kwa Kikwete katika nafasi ya juu ya uongozi ni kama kinga.

Kama wapo wana CCM ambao wanaona Kikwete ndiye kiongozi bora zaidi na ndiye anafaa zaidi, basi wasimame waanze kampeni ya kurekebisha Katiba ili tuondoe ukomo wa madaraka.

Kwani, kama ukomo wa Kikwete (akikubali kusukumwa kugombea tena) utakuwa ni 2015 ina maana kuna mtu mwingine atashika madaraka hayo ndani ya miaka mitano ijayo.

Kama hilo ni kweli ina maana mtu huyo tayari yupo sasa. Kama hilo ni kweli pia, basi mtu huyo anaweza kuingia madarakani hata sasa.

Mwaka 2005 kinyume na inavyosemwa, Kikwete hakupitia kwenye tanuru ya moto; hakuwa na rekodi ya kusimamia lakini safari hii bila ya shaka tunayo rekodi yake ya kutosha na tunaweza kumpima kwa kile alichokifanya kama rais.

Na ni kipimo hicho tu ndicho ambacho kitatuamulia kama ana sababu ya kugombea tena au tutafute mtu mwingine.

Safari hii Kikwete kama anataka kuwa rais wetu tena itabidi ajibithibitishe kwa kufanya midahalo na wagombea wengine, kusimamia rekodi yake na kujibu hoja zitakazotolewa dhidi yake.

Safari hii urais hauji kwa kuuza jina, sura, au tabasamu. Safari hii, urais utakuja kwa kuustahili.

Na wana CCM ambao wanaona Kikwete hawezi kuwa chaguo lao wasijisikie vibaya wala kujiona kama wanasaliti chama; watambue kuwa wana wito mkubwa zaidi na sababu kubwa zaidi na kama wanaona kuwa Kikwete anahatarisha hata maslahi ya chama basi, ni jukumu lao kutokumpendekeza.

Hapo, Kikwete, kama Mkapa atakaa pembeni na kula pensheni yake na kuendelea kufurahia ving'ora na saluti za hapa na pale.

Kama Jenerali Powell aliweza kumuunga mkono Barack Obama wakati yeye ni wa kutoka chama cha Republican na mtu aliyefanya kazi na marais wa Republican kama Reagan, Bush na G. W. Bush, basi mwana CCM yeyote anaweza naye kumpendekeza mtu mwingine zaidi ya Kikwete.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: