Uhuru wetu umeliwa na CCM


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 10 August 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

BABA wa Taifa katika siku zake za mwisho kama rais mstaafu aliwahi kukemea tabia ya Ikulu kugeuzwa danguro la wafanyabiashara waovu. Leo hii, ikulu imegeuzwa ndanguro na baadhi ya wafanyabiashara na watendaji wa serikali waliokumbatia rushwa, jambo ambalo limeifanya nchi kuwa na uongozi tofauti na ule uliochaguliwa na wananchi.

Tusishangae kuona waandishi wa habari wakimwagiwa tindikali usoni; FFU wakilemaza watu na kuongeza idadi ya wajane wanaolea watoto yatima nchini; wenye migodi ya dhahabu wakitumia walinzi wao kama korokoroni wa Kiingereza na wakazi wa maeneo jirani kuitwa wavamizi na hivyo kuuawa.

Haya ndiyo matunda yaliyotarajiwa katika utatu usio mtakatifu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na mihimili yake katika uongozi. Hivi leo tuna viongozi wengi tu wa majina lakini si viongozi kwa uwezo, vitendo na dhamira. Wameacha uzalendo, badala yake wanakumbatia matajiri na wawekezaji wa nje.

Ndio maana mwenyekiti wao akitoa amri kuhusu kitu fulani, hakuna kiongozi wa chini anayesimamia utekelezaji. Agizo lake huishia alipolitoa. Hii ndio hasara ya kuzungukwa na watu wasiochaguliwa na wananchi bali mfumo wa ulinzi na usalama uliopo umewataka waongoze.

Wengi wa watu hao ni wafuasi wa CCM, marafiki, jamaa, ndugu, wabia, wateule wa mafisadi waliokisaidia chama kushinda uchaguzi mkuu.

Wakati wa mfumo wa chama kimoja, hapakuwa na ubaguzi katika hatua ya mtu kuchaguliwa. Chini yake tangu mwaka 1995 tumeiona ikichagua watu wasiofaa kuongoza wizara, mikoa, wilaya, tarafa na kata na taasisi nyinginezo kwa ubaguzi wa kichama.

Na hawa ndio viongozi wanaogoma kutekeleza amri ya mwenyekiti na rais, lakini ni wepesi wa kutekeleza yale yanayowanufaisha binafsi.

Kwa bahati mbaya viongozi wa CCM hawajui tofauti ya uchumi kukua na watu/jamii kuendelea. Uchumi unaweza kukua kwa kasi (asilimia 7 mpaka 12), lakini ukuaji huo usisaidie chochote katika wajibu wa serikali kupunguza umaskini wa wananchi.

Hili hutokea pale wawekezaji, matajiri na mafisadi wanavyochuma zaidi na chote au sehemu kubwa ya pato kupelekwa nje. Ni sawa na mkulima kuvuna chakula kingi, akauza chote au kingi; baadaye analia njaa.

Sehemu kubwa ya chakula kinacholimwa nchini, hupelekwa nje. Kidogo kinachobaki, huishia kwa matajiri na raia wengine wachache wenye uwezo.

Kama CCM ilivyoua Shirika la Uchumi na Kilimo (SUKITA) ndivyo ilivyoua Shirika la Madini Tanzania (STAMICO) ambalo lilistahili kuingia ubia na wasaka madini nchini badala ya kuyasabilia wageni.

STAMICO ingepata fedha za kutosha kusaidia wachimbaji wadogo ili waweze kushiriki katika utafutaji wa madini. Ingeweza kukuza utumiaji teknolojia katika kazi hiyo kama wafanyavyo wageni.

CCM hawajui tofauti hii. Kitu kibaya wanadhani na wengine nao hawaoni. Hawalijui tatizo. Wao ndio hawajui tatizo. Hapa, hawawezi kusaidia wenye tatizo hilo ambao ni mamilioni ya Watanzania masikini.

Chukua hali ilivyo katika miaka 40 tangu mwaka 1970. Watanzania waliokuwa wanajua kusoma na kuandika 1970 ni asilimia 80 wakati 2010 ni asilimia 55 tu. Watu waliokuwa wanapata maji safi na salama mwaka 1970 walikuwa asilimia 70 sasa ni asilimia 40 tu.

Waliokuwa wakiishi vizuri kwa mshahara uliowapatia mahitaji yote ya msingi walikuwa asilimia 90 mwaka 1970, sasa ni asilimia 30; waliokuwa na uwezo wa kusafiri ni asilimia 80, leo ni asilimia 40 tu na sasa tunaona wafu wakizikwa miji walipofia badala ya kusafirishwa kwao kwa asili.

Watu asilimia 70 walikuwa wanapata lishe au chakula bora mwaka 1970, leo ni chini ya asilimia 30; watu waliokuwa na makazi bora mwaka 1970 walikuwa asilimia 60, sasa ni chini ya asilimia 40.

Maeneo mengi ya vijijini yalikuwa yakijitosheleza kwa chakula, maji na nishati, leo vijiji vingi vina dhiki kwa hayo. Ni nadra kukuta kijiji kinajitosheleza kwa kila huduma.

Asili ya CCM ilianza kubadilika wakati ulipokaribia uchaguzi mkuu wa kwanza ndani ya vyama vingi. Ilijikuta haina njia ya uhakika ya kufadhili kampeni yake ya kuendelea kuongoza. Ikitegemea ruzuku tu ya serikali ambayo isingetosha kuhimili ushindani wa vyama chipukizi.

Ndipo utatu mtakatifu ulipoanza kati ya viongozi wake, mangimeza wa serikali waliopo kwenye taasisi za kiserikali na kutengeneza mianya ya kuchota mabilioni ya shilingi za umma. Na hiyo imekuwa ndiyo njia ya chama hiki kubaki madarakani.

Ni hapa viongozi wa CCM katika kikao cha juu kabisa waliruhusu kununuliwa kwa rada mbovu kwa bei zaidi ya ile iliyostahili kulipwa. Kama wengi, mnavyojua baada ya serikali ya Tanzania kulindwa na tawala zilizopita za Chama cha Labour cha Uingereza, baadaye Chama cha Conservative, waliamua kuufichua ufisadi huo.

Uingereza ikaliadabisha shirika lake la umma – British Aerospace System (BAE System) lililotoa kamisheni ya kinyume na sheria na ikazuia fedha za juu kuipatia serikali ya Tanzania. Uingereza ingependa fedha hizo zikabidhiwe mashirika ya kiraia ili zinufaishe watu wa kipato cha chini.

CCM iliahidi tangu mwaka 1970 makao makuu ya nchi yawepo Dodoma. Miaka 41 leo, hawana moyo tena kuzungumzia hili ingawa fedha nyingi zimeingizwa kwa miradi ya kutimiza lengo hilo.

Maamuzi kama haya yanayotekelezwa nusu nusu hufanywa tu na chama kisicho dira. CCM imekumbatia viongozi waovu na mafisadi na sasa wanaendesha dhulma isivyomithilika.

Dhulma na madhambi wanayoyafanya yanawakengeuka na kuwageuza watu wasiojua wala kutambua wanalolitaka wala lile wanalolifanya.

Wamekula mabilioni ya shilingi zilizotokana na ubinafsishaji mashirika na viwanda vya umma na vingi vimeshindwa kazi. Lakini chama hichohicho kimeshindwa kubuni mpango wa kuwawezesha wananchi mmoja mmoja na vikundi kujenga upya makampuni hayo kama nchi ya China ilivyofanya. Ama kweli CCM imekula uhuru.

Mwandishi amejitambulisha kama mzee mstaafu serikalini na katika CCM anayeishi Musoma mjini, mkoani Mara.
0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: