Ujanja kuwahi na kupata


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 17 November 2010

Printer-friendly version
Wazo Mbadala

SIRI ni ya mtu mmoja, wakiwa wawili hiyo si siri tena. Mmoja kati yao, atapata joto moyoni, atafurukutwa; na dawa ya utulivu huo ni kuweka wazi mpango wa siri alioshirikishwa.

Jamani, siri ya nani alikuwa anaandaliwa kuapishwa akalie “kiti cha enzi” imevuja. Walimu walioshirikishwa katika mpango huo wameshindwa kuficha siri.

Nafsi zimewasuta. Wamepiga simu kueleza walivyoona ishara za mpangaji wa ikulu wa 2005-2010 kuandaliwa kuapishwa hata kabla Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutaja mshindi.

Wanasema walipigiwa simu na maofisa elimu katika manispaa za Kinondoni, Temeke na Ilala kuwataka wajiandae kujaza uwanja wa Uhuru wakati wa kuapishwa rais mteule.

Walioandaa mpango huo walikuwa na hofu kwamba “mchezo” wa kusaka rais ungemalizika kwa vurugu kama chandimu; hivyo watu wangekosekana uwanjani.

Walimu waliohoji kwa nini wapigiwe simu wakati NEC haijatangaza mshindi, waliachwa na walioonyesha utiifu wanadai alipewa kofia, kanga au shati na fulana na ‘mkwanja’ – Sh.5,000 kama nauli.

Watu waliofika uwanja wa Uhuru kushuhudia hafla ya kuapishwa Jakaya Kikwete kubaki Ikulu, walipata bahati ya kusoma nyuso za waliohudhuria.

Wapo waliokuwa wamevalia fulana za njano, kofia na kanga huku wakiselebuka kwa furaha. Hao walikuwa ‘wenye mwali’ – Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka matawi mbalimbali mkoani Dar es Salaam.

Walikuwepo walioonekana kama wamemwagiwa maji; hawakuwa na furaha. Hao ni walimu walioshurutishwa kushangilia ‘harusi’ waliyoisusa kwenye kura.

Wanadai kuwa walishindwa kugoma kwa kuhofu hasira za maofisa elimu ambao huwa hawabishiwi. Wanaothubutu kuhoji hukomolewa kwa kuhamishiwa shule za pembezoni mwa nchi.

Wafalme Dodoma walishurutisha walimu wa shule za msingi kwenda na wanafunzi kwenye mikutano ya mgombea urais wa CCM; Mwanga majengo ya shule yalitumika kwa kampeni za usiku; Singida, Songea, Iringa nao wana yao.

Ungamo hilo ni uthibitisho kwamba rais wa mwaka 2010 hakusubiriwa atokane na tangazo la Tume ya Uchaguzi. Kweli, ujanja kupata.

Kwa hiyo, wakati Prof. Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF) na Dk. Willibrod Slaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wakisubiri matokeo ya mwisho ya NEC, mchezo ulishakwisha.

Nini Sh. 5,000? Sikiliza sauti za ungamo. “Sisi ndio tulikuwa wa kwanza kuitwa na kulainishwa mioyo tusione mabaya ila mazuri ya mteule.”

Watakuja wengi kukiri. Kwamba walioripoti habari za mteule kuchukua fomu za kugombea urais mwaka 2010 waliondoka na bahasha za khaki.

Soma hili: “Walipofungua walikuta ‘nauli nzito.’ Baadhi yao waliharakisha kuandika habari ile na wakachomoka kwenda maduka ya vifaa vya ujenzi kununua misumari na bati kwa nauli ileile.”

Kuna maelezo kuwa nauli hiyo ilikuwemo pia katika bahasha za walioripoti habari za mgombea huyo kurejesha fomu. Je, hapo kuna vita tena dhidi ya rushwa?

Ndiyo maana CCM walipobuni kauli mbiu ya “Ushindi Ni Lazima” walijua nini wanafanya. Ndiyo maana vijana walipigana vikumbo kupata nafasi ya kuwemo kwenye msafara wa mgombea huku wamevaa ‘viblauzi’ vilivyoandikwa Press-Chagua CCM kampeni zilipoanza rasmi Agosti 20, mwaka huu.

CCM ni kinyonga; hapana, vinyonga. Wakisimama jukwaani au wakiitwa kwenye makongamano ya wanahabari, hutoa ushauri mzito, “Waandishi wa habari msionyeshe ushabiki wa kisiasa wala upendeleo.”

Unafiki mkubwa! Mbona mazingira waliyojenga ni ya wao kupendelewa? Akili zao ni kwamba wakiandikwa wao ni haki, lakini habari za CUF, CHADEMA, NCCR-Mageuzi zikiripotiwa ni upendeleo. Jamaa hawa vipi?

Wanayosema si wanayotenda. Wanakuwa kama baadhi ya viongozi wa madhehebu wanaohalalisha uovu wao kwa kusema, “Usifuate ninayotenda, bali fuata ninayosema.”

Ndiyo maana katika kila mlango wa ofisi za serikali kuu, halmashauri au idara zake, kuna maandishi yasemayo, “Hatupokei wala kutoa rushwa.”

Tafsiri rahisi na sahihi ni kwamba ule mlango ndio haupokei wala kutoa rushwa; bali watu waliomo ndani wanapokea rushwa. Anayebisha anyoshe mkono hapo alipo umma umwadhibu! Hupati kiwanja bila kutoa rushwa—unapokea mlango au anapokea binadamu?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: