Ujanjaujanja huu hautaisadia CCM


editor's picture

Na editor - Imechapwa 29 September 2010

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilifanya kazi kubwa mwanzoni mwa mwaka huu, kuhamasisha wananchi, kwa mabango na vipeperushi juu ya umuhimu wa kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapigakura.

Mbali ya kuhamasisha, NEC iliandikisha wapigakura wapya kwenye daftari hilo na iliwaandikisha waliohama vituo vyao vya awali na waliopoteza vitambulisho vya kupigia kura ili waweze kushiriki katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Tume ilitumia kiasi kikubwa cha pesa kukamilisha zoezi hilo, na miongoni mwa wananchi walionufaika katika mpango huo ni maelfu ya vijana waliofikisha umri wa miaka 18 au wanaotarajiwa kufikisha umri huo ifikapo Oktoba.

Kila raia aliyejiandikisha, alishauriwa kutunza kadi yake ili aweze kuitumia siku ya kupiga kura 31 Oktoba. Wanafunzi wametunza kadi hizo, lakini kwa mshangao, serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imewapora vijana hao, haki yao ya msingi kupiga kura.

Serikali imeagiza vyuo na asasi nyingine za elimu ya juu kufunguliwa baada ya uchaguzi mkuu na kwa sababu hiyo watakosa haki ya kuchagua. Hii inatokana na sababu kwamba wanafunzi walijiandikisha walipokuwa vyuoni, hivyo hawawezi kupiga kura wakiwa likizo.

Wanafunzi wameomba vyuo vifunguliwe kabla lakini serikali imeitumia Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kusema kuwa bodi haina fedha za kulipa wanafunzi mpaka uchaguzi utakapomalizika.

Je, watu wanafunzi waelewe kuwa, fedha zilizotengwa kwa ajili ya kukopesha wanafunzi zimechukuliwa na serikali kwa ajili ya uchaguzi?

Kama fedha haziwezi kupatikana kabla ya uchaguzi, zitatoka wapi Novemba muda ambao serikali inasema ndipo wanafunzi watatakiwa kurejea vyuoni?

Jambo la kusikitisha na linaloonyesha kwamba serikali kunyonga demokrasia ni pale bodi ya mikopo inapotoa vitisho hata kwa vyuo vikuu binafsi ambavyo vilitaka kufungua kwa kufuata ratiba zake za kawaida.
Kwa namna yoyote ile huu ni ukiukwaji wa haki za msingi za binadamu na inasikitisha kuona chama tawala ndicho kinahusika kupokonya haki ya raia inaotaka kuwatumikia.

Inasikitisha kusikia pia kwamba CCM imejihusisha kununua kadi za kupigia kura na kwamba baadhi ya viwanda vinavyomilikiwa na makada wake mkoani Arusha vimekusanya kadi za kupigia kura wafanyakazi wao huku kukiwa na taarifa kama hizo Bunda, Musoma, Iringa, na Sumbawanga.

Tunaishauri serikali ya CCM iache ujanjaujanja, iwape wanafunzi na walimu wao haki ya kuchagua viongozi wanaowafaa. Vilevile iache ghiliba kwa kukusanya kadi kinyume cha sheria.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: