Ukaburu huu wa CCM ni hatari


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 27 October 2010

Printer-friendly version
Tuseme Ukweli

SERIKALI ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inaiga na kutumia sheria na sera za kibaguzi mithili ya zile za  iliyokuwa serikali ya makaburu wa Afrika Kusini.

Hii ni katika tafsiri na matumizi ya sheria inayofanya uandishi au aina ya uandishi wa habari kuwa “jinai” na hivyo, vyombo vya habari na waandishi kutuhumiwa au kushitakiwa kwa “uchochezi,” ambao hakika ni kosa la kisiasa. 

Makaburu, chini ya National Party tangu enzi za Charles Robberts Swart mwaka  1894 hadi chini ya Frederik Willem de Klerk mwaka 1994, walijipa imani kwamba Mungu aliwashushia neema ya kutawala Afrika Kusini kwa misingi ya rangi, hivyo walikuwa wanashangaa Waafrika kulalamika.

Waafrika walipokuwa wanapigania haki ya kupata elimu bora, kushiriki katika utawala, kutembea mahali popote pale nchini mwao, walionekana wachochezi au haini.

Wapigania uhuru wa Afrika Kusini, kama vile Nelson Mandela walifungwa jela na wanaharakati kama Steve Biko walikamatwa, wakateswa na kuuawa. Makaburu waliona Uafrika kuwa laana iliyoshushwa na Mungu.

Mwanaharakati wa Haki za Binadamu wa Nigeria, Ken Saro Wiwa, na wenzake wanane waliuawa na utawala wa kijeshi wa dikteta San Abacha kwa kile kilichodaiwa kufanya uchochezi.

Kisa ni Saro-Wiwa kupinga uchafuzi wa mazingira kwenye maji yanayotumiwa na wananchi wa jimbo la Niger Delta na pia kupinga makampuni ya kuchimba mafuta kutokuwa na mipango ya kuendeleza maeneo wanakoshi wananchi.

Mwanaharakati huyo alikamatwa, akafunguliwa kesi ya uchochezi chini ya serikali ya kijeshi na katika muda mfupi akanyongwa.

Lakini leo dunia nzima inalaani uchafuzi wa mazingira uleule ambao Saro-Wiwa alikufa akitetea.

Ubabe wa watawala umeelezwa vizuri katika kitabu cha “An enemy of the people” cha Henrik Ibsen wa Norway.

Katika kitabu hicho, Ibsen anaeleza mradi wa bwawa kubwa lililochimbwa kwa shughuli za binadamu lilivyogeuzwa na kuwa hatari kwa maisha yao.

Mradi huo wa Jiji la Oslo ulipoanza kufanya kazi, baadhi ya viwanda vikubwa vikawa vinamwaga uchafu ndani, hivyo waliokuwa wanaoga humo, wakiwa pamoja na watalii, wakawa wanaugua.

Uchunguzi alioufanya Dk. Thomas Stockmann, ukaonyesha tatizo ni uchafuzi wa bwawa, hivyo akawaambia watu wasiende kuoga bwawani.

Serikali ya Jiji la Oslo iliyokuwa inaongozwa na kaka yake, Peter Stockmann ililaani kitendo hicho cha kuwajuza wananchi kuwa ni cha uchochezi, kwani kilisababisha serikali kukosa mapato. Dk. Stockmann akaitwa “Adui wa Watu” – An enemy of the people.

Hivi ndivyo Serikali ya CCM ilivyojibadili taratibu na kuiga sera za makaburu au dikteta Sani Abacha au kisa katika “An enemy of the people.”

Ujumbe mwema unaotolewa na asasi za kiraia na gazeti la MwanaHALISI unaitwa uchochezi kwa sababu tu unawaelimisha watu waliolala; unawapa mwanga wa kuwafanya waone watawala wao wanavyokula na kufisadi nchi.

Wakati wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika, chama cha Tanganyika African Association (TAA) na baadaye Tanganyika African National Union (Tanu) walitumia klabu za soka na vyama vya wafanyakazi kudai uhuru.

Lakini leo serikali ya CCM inadai Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) linafanya uchochezi kwa kuwa linadai haki na maslahi ya wafanyakazi nchini.

Wabunge, ambao kimsingi ni wanasiasa, wanajifutua bila hoja kutaka Tucta ijibadili iwe chama cha siasa. Hawa ndio walichochea serikali ifungie Baraza la Wanawake Tanzania (Bawata) na asasi isiyo ya kiserikali ya HakiElimu.

Uzandiki

Serikali ya CCM huhamasisha mashirika ya dini yajenge shule, zahanati na vyuo kwa ajili ya kuhudumia watu kimwili. Mara wanapogusa siasa, wanasiasa haohao hung’aka wakidai maaskofu wavue majoho.

Hivi, mshindi wa Tuzo ya Nobel, Askofu mkuu wa Kanisa la Anglikana, Desmund Tutu alipokuwa anapambana na Makaburu alivua joho?

Hivi watumishi wa Mungu, mchungaji Dk. Getrude Lwakatare na Lackson Mwanjali wanapounga mkono na kuwa wabunge wa CCM, wamevua majoho?

Kwa nini CCM waone kile alichokuwa anapigania Tutu au wanachofanya kina Dk. Lwakatare na Mwanjali ni sahihi lakini wasione kuwa haki kwa maimam na maaskofu wa Tanzania wanaojenga shaka juu ya mfumo uliopo?

Serikali ya CCM ilidai kusikitishwa na kifo cha Saro-Wiwa, lakini katika kipindi hichohicho yenyewe ilimtia ndani mwanaharakati wa Tanzania, Tundu Lisu kwa hoja zilezile.

Maana

Kamusi ya Kiswahili inasema uchochezi ni tabia ya kuwatia watu maneno wapate kupigana au kutukanana; uchonganishi.

Aghlabu shina la neno hilo ni chochea; yaani sababisha ugomvi, tia ugomvi, chokoza, kasirisha, tia hamaki. Mtu anayechochea wengine wapate hasira na kufanya ugomvi anaitwa mchochezi.

Huo ndio msamiati wanaoutumia wanasiasa mara kwa mara wanapovijadili vyombo vya habari nchini, wengi wakitaka vibanwe kisheria ili visidadisi wakubwa wanavyotajirika kutokana na raslimali za Watanzania.

Mwaka 2001 serikali ilionywa na vyombo vya habari kuwa kiasi cha pesa kilichotumika kununua rada na ndege ya rais kilikuwa kikubwa. Uchunguzi ulionyesha ndege kama hiyo iliyonunuliwa na Saudia, bei yake ilikuwa chini kwa nusu, lakini wakakataa.

Leo serikali ya CCM imetumia mabilioni mengine ya shilingi, takriban zaidi ya zilizoibwa, kuchunguza wizi huo ambao tahadhari yake ilitolewa mapema.

Waziri wa Fedha na Uchumi wakati ule, Basil Mramba alisema, hata ikibidi “tutakula nyasi lakini lazima ndege inunuliwe;” na akavishtumu vyombo vya habari kwa kung’ang’ania suala hilo.

Leo waziri huyo ni miongoni mwa viongozi watatu waliofunguliwa kesi kortini.Yeye anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake na kusababisha hasara. Je, uko wapi uchochezi wa vyombo vya habari?

Wananchi watakuwa wanakumbuka mjadala mrefu na wa vuta nikuvute juu ya kusudio la serikali kununua mitambo ya kufua umeme wa dharura ya Dowans (Richmond). 

Rais, akionekana kutaka kuwapa unafuu walioingiza mitambo hiyo kifisadi, aliwataka viongozi wa Wizara ya Nishati na Madini waangalie upya Sheria ya Manunuzi ya Umma ili isiwe kikwazo katika uwekezaji wa miundombinu mikubwa ya umeme.

Lakini vyombo vya habari vilipoandika ‘Rais aingilia suala la umeme’, ikulu ilidai ni uchochezi.

Kwa hiyo, sheria ya uchochezi inatumiwa vibaya kwa makusudi ili kukidhi matakwa ya serikali na katika kipindi hiki matakwa ya CCM.  Huu ni ukaburu.

Uchochezi ni silaha wanayoitumia wanasiasa sasa katika njama za kuvinyamazisha vyombo vya habari ili visiibue uoza.

Kimbilio la serikali yoyote inayoendesha mambo yake kwa kificho ni kunyonga uhuru wa watu kupata habari, kuwadhalilisha waandishi kwa kuwaita “kanjanja” na kutishia au kuwafungulia kesi za uchochezi.

Kwao, kushupalia ufisadi wa Richmond, Meremeta, EPA, Deep Green Finance, Kiwira ni uchochezi. Sheria hii ina harufu, sura, umbo na maudhui ya Kikaburu. Ifutwe.

0
Your rating: None Average: 5 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: