Ukatili hujibiwa kwa sheria


editor's picture

Na editor - Imechapwa 20 April 2011

Printer-friendly version
Maoni ya Mhariri

KIJANA Lillah Hussein (24), amehujumiwa kikatili na hatimaye amefariki dunia. Ni chini ya wiki moja tangu alipotendewa unyama usiomithilika. Alikamatwa, akatishwa, akapigwa na baadaye, kama vile mateso hayo hayakutosha, akateketezwa kwa moto baada ya kuvikwa tairi la gari na kumwagiwa petroli.

Hayo yamemkuta alipokamatwa ndani ya hoteli ya South Beach Resort iliyoko Kigamboni, Dar es Salaam. Hii ni hoteli yenye historia ya uhusiano mbaya kati ya wamiliki na wenyeji wa maeneo yanayoizunguka.

Hata kama alitenda kosa lolote, Lillah hakustahili kukatiliwa kiasi hicho. Bali alipaswa kukabidhiwa vyombo vya sheria kwa hatua zinazofaa kisheria.

Sasa Lillah ni marehemu. Ungetarajia katika nchi ambayo viongozi wake wanajinasibu kwa kuendesha mambo chini ya misingi ya sheria, mtiririko wa sheria ukatumika kushughulikia watuhumiwa.

Kulingana na mazingira yaliyokwishajionesha mwanzoni tu mwa tukio, ni dhahiri tunaona jitihada za kutaka kupinda haki na ikiwezekana kuizuia isitendeke.

Nyaraka zilizotufikia zinaonesha watuhumiwa wamefunguliwa mashitaka mepesi ya “kujeruhi” na “shambulio.” Baada ya kusomewa mashitaka hayo, wamepewa dhamana na kwa sasa wako nje.

Dhamana hiyo ni kinyume na maombi ya waendesha mashitaka waliopendelea dhamana isitolewe kwa kuwa mtu aliyejeruhiwa ameshafariki dunia na majeraha aliyopata yanachukuliwa kuwa chanzo kikuu cha kifo chake.

Tunazo taarifa kuwa tangu watuhumiwa walipokamatwa, wakuu wa Polisi Temeke, wamekuwa wakipokea simu za baadhi ya viongozi waandamizi serikalini kufuatilia.

Viongozi wanaopiga simu wanaulizia na kutaraji mambo yaende harakaharaka na ikibidi wawekezaji wanaowapenda kama roho zao, wabaki nje.

Hivi ni vitendo vibaya visivyopaswa kutokea nchini. Kumfuatilia mtuhumiwa aliyehujumu raia na mfuatiliaji akawa anajitahidi kuzuia haki kutendeka, ni kukaribisha ufisadi katika jukumu muhimu kijamii la utoaji wa haki.

Tunataka kuamini harakati za viongozi hao ambao tunawafuatilia ili kuwafichua, ndizo zilizotetemesha Polisi hata kufungua mashitaka mepesi kwa watuhumiwa wakati wakijua fika kuwa waliyemkatili, ameshafariki dunia.

Viongozi wanaohusika wana haki ya kuonea huruma wawekezaji lakini lazima waheshimu sheria. Ni vema wakatambua machungu waliyonayo ndugu na jamaa za marehemu.

Hebu wangechukulia tukio hilo kama limemkumba ndugu yao, wangejisikiaje? Wangetulia, wakakaa na kufunga midomo yao?

Hapana shaka wangeonekana makatili vilevile kama wale waliomjeruhi Lillah na kumsababishia kifo angali kijana mbichi.

Tunasema huruma za viongozi kwa wawekezaji zisipitilize mipaka ya sheria za nchi. Tunahimiza watuhumiwa wafunguliwe mashitaka yanayofanana na uzito wa kile kilichotendeka na matokeo ya kitendo hicho.

0
No votes yet