Ukatili, manyanyaso hospitali ya Kahama


Ali Lityawi's picture

Na Ali Lityawi - Imechapwa 27 April 2011

Printer-friendly version

SHEBONIA Faustin (22) alikuwa na furaha isiyo na kifani katika kipindi chote cha ujauzito wake. Muda wote alikuwa anafikiria zao la ndoa yake kwa mumewe Karim Mohamed (30).

“Ujauzito wa kwanza, mtoto wa kwanza,” alikuwa akijisemea kwa furaha. Dalili za kujifungua zilipoanza kuonekana, binti huyo mkazi wa Majengo wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga, kwa msaada wa mama yake mdogo, Bahati James alichukua vifaa muhimu alivyoandaa, akaanza haraka safari kwenda hospitali ya wilaya.

Alipokewa na waauguzi, akapewa kitanda akalala, lakini aliyoyaona na hasa yaliyomkuta kuanzia Aprili 5, 2011 alipofika hadi Aprili 7, 2011 alipojifungua na kutoka, yanatisha.

Kwanza Aprili 6, alishuhudia mzazi mmoja aliyekuwa amelazwa kitanda cha jirani akilazimishwa na wauguzi wa wodi ya wazazi kubeba beseni la nguo huku mtoto akiwa tayari ameanza kutoa kichwa.

Pili, ilipofika zamu yake mama yake mdogo alilazimika ‘kuwanunulia’ chapati wauguzi ili wamhudumie mtoto wake, lakini alipotoa Sh. 2000 badala yake, walimsusa.

“Ilikuwa siku ya Jumanne ya Aprili 5, mwaka huu majira ya saa 5.00 usiku nilipofikishwa hospitalini hapo nikiwa nasumbuliwa na uchungu wa kujifungua. Lakini nilikutana na manyanyaso na hali ya kutisha kutoka kwa wauguzi.

“Alfajiri ya Aprili 6 nilishuhudia mzazi mmoja ambaye alikuwa amelazwa kitanda cha jirani akilazimishwa na wauguzi wa wodi ya wazazi kubeba beseni la nguo huku mtoto akiwa tayari ameanza kutoa kichwa hali ambayo ilinitia huzuni. Nilijiuliza itakuwaje zamu yangu ikifika?” anasema binti huyo aliyelazwa sasa zahanati ya Kwema.

Pamoja na kuwepo wito kwamba wajawazito wapewe huduma kwa upendo lakini wanakejeliwa, wanafanyiwa ukatili na uzembe huku wengine wakiombwa rushwa ya vitafunwa ili wapate huduma nzuri.

Ripoti zinaonyesha kuwa huduma zisizoridhisha na uzembe, wajawazito wengi wanaona heri kuhudumiwa na wakunga wa kienyeji kuliko hospitalini.

Takwimu za Mganga Mkuu wa wilaya, Leonard Subi zinaonyesha Idara ya Afya imepanga kukabiliana na matatizo ya vifo vya wanawake wajawazito kwa kupungua kutoka vifo 126 kwa watu laki moja hadi kufikia vifo 120 kwa watu Laki moja ifikapo mwaka 2014.

Mwaka 2008 vilitokea vifo vya wanawake 68 kutokana na matatizo ya uzazi; mwaka 2010 vilitokea vifo 40, na kuanzia Januari hadi Aprili 11, 2011 vimetokea vifo 12.

Bahati nzuzi Shebonia na mzazi mwingine aliyekuwa jirani yake wako hai, lakini wote wamepoteza watoto wao kwa sababu ya uzembe na ukatili wa wauguzi.

Kila alipojitahidi kuwapa taarifa wauguzi juu ya hali yake kuanzia saa 12.00 jioni Aprili 6, alijibiwa vibaya.

“Nesi, nesi,” aliigiza walivyomwambia huku amebana pua. “Wewe sukuma mtoto atakuja mmwenyewe au unataka na kusukuma tuje tukusaidie?” alijibiwa. “Kama ni suala la kusukuma usituite bibie!”

Muuguzi wa kiume aliyefika asubuhi aliamuru wauguzi hao wamtundikie drip ya uchungu. Alijifungua mchana akiwa amechoka, lakini walilazimika kumpeleka mtoto huyo kwenye chumba maalum chenye oksijeni.

Hata hivyo, kama ilivyotokea kwa yule jirani yake, naye alipewa taarifa na ndugu zake baadaye wodini kwamba mtoto wake wa kiume alikuwa amefariki.

Wanaopata usumbufu si kina mama wajawazito tu bali hata ndugu wanaowapeleka chakula na kutoa msaada wa hali na mali katika harakati hizo za uzazi. Hao ndio huombwa rushwa ya vitu au fedha na huhangaishwa kwa hili na lile.

Bahati, mama mdogo wa Shebonia alikabiliana uso kwa uso na waauguzi waliojenga mazingira ya rushwa na alipojipiga akatoa, akakutana na wengine waliotaka chapati.

“Ajabu ni kwamba mnamo majira ya saa nane za usiku nilimshuhudia Shebonia akirejea wodini huku akiwa amedhoofika. Nilimfuata mkunga, nikazungumza naye nikampa Sh. 2000 ndipo akamrejesha kwenye chumba cha kujifungulia,” anasimulia Bahati.

Asubuhi akakutana na mengine. Wakunga wa zamu ya usiku walipokuwa wanaondoka asubuhi walimkabidhi kwa wakunga wenzao ili kumhakikishia usaidizi mzuri.

“Saa tatu hivi asubuhi ya siku hiyo niliitwa na wakunga hao na kuulizwa, ‘unaifahamu baa moja inaitwa JVC? Nenda pale ukatununulie chapati halafu utuletee, hapa mjini si unajua tena?”

Mama huyo alitimua mbio hadi alikoelekezwa lakini hakufanikiwa. Aliporejea bila chapatti aliamua kuwapa Sh. 2000 wajinunulie lakini walikataa kwa vile muuguzi wa kiume alikuwepo na ‘aliona’.

Kwa kujihami, wakunga wakaripoti tukio la kutaka kuhongwa kwa Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo Dk. Hellen Yesaya ambaye alimwandikia barua Shebonia afike ofisini mwake ili walipatie ufumbuzi suala hilo.

Katika barua hiyo ya Aprili 12, 2011, mganga huyo alisema Shebonia Faustine anaombwa kufika Ofisi ya Mganga Mfawidhi wa Hospitali ili aweze atoe ufafanuzi juu ya malalamiko yake dhidi ya wakunga wa hospitali ya wilaya ya Kahama kusababisha kifo cha mtoto wake aliyefariki baada ya kujifungua kusudi waweze kulitafutia ufumbuzi suala hilo.

Pamoja na Dk. Hellen kuandika barua hiyo, hakuwa tayari kuongelea tuhuma hizo kwa madai wakati tukio hilo likitokea alikuwa nje ya wilaya kwa majukumu mengine. Hata hivyo aliahidi kulifuatilia akimaliza warsha ya siku mbili katika Kata ya Kagongwa ili kubaini ukweli na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wahusika.

“Unajua kwa sababu gani? Japokuwa sote tuwauguzi lakini tunatofautiana lugha katika kuwahudumia wagonjwa. Hayo yapo hata katika familia majumbani kwetu, ukweli uliopo jambo hili hatuwezi kulifumbia macho kwani linatutia dosari kwani samaki mmoja akioza basi wote wameoza hivyo, ni vyema tudhibiti hali hii isiweze kuendelea kutokea”.

Dk. Hellen ameeleza pia kwamba kuna upungufu wa wauguzi na madaktari kwa asilimia 28.86, kwani wilaya inayokadiriwa kuwa na watu wapatao 900,000 ina wauguzi na madaktari 313 huku mahitaji halisi ni 440.

Pamoja na sababu hiyo ya msingi, uchunguzi unaonyesha kuwepo kwa matukio mengi ya unyanyasaji wa wagonjwa katika hospitali hiyo jambo ambalo linawavunja moyo wakazi wa wilayani Kahama kwenda kupata huduma ya afya hospitalini hapo. Wengi wao, hasa wenye vipato huamua kwenda hospitali na zahanati za binafsi huku wasio na vipato wakikimbilia tiba mbadala.

Desemba 28, 2008 Dayness Kadikilo pia mkazi wa Majengo alijifungulia nje ya lango la kuingilia hospitalini hapo kwa sababu ya wauguzi kutomshughulikia haraka.

Pia  kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani mwaka huo, Zainabu Mustapha alijifungua kwa msaada wa wajawazito wenzake.

Februari 8, 2009 wauguzi wanadaiwa kusababisha kifo cha Halfani Salumu mkazi wa Kagongwa baada ya kupuuzia agizo la Dk. John Duttu aliyemfanyia upasuaji kwamba aongezewe damu.

Dk. Subbi kipindi hicho aliahidi kuwachukulia hatua za kinidhamu wahusika huku akisisitiza kuwa si lazima hatua atakazozichukua azitangaze kwenye vyombo vya habari.

Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa simu 0784933815, 0767933815 na 0715933815
0
No votes yet