Ukistaajabu ya Mahita utaona ya Shimbo


Mwana CCM Masalia's picture

Na Mwana CCM Masalia - Imechapwa 06 October 2010

Printer-friendly version
Tafakuri
Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo

MARA baada ya kuanzishwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, ilitungwa sheria kuzuia baadhi ya maofisa na majeshi kujiunga na vyama vya siasa. Hata wanajeshi waliokuwa na nafasi za kisiasa waliambiwa wachague siasa au warudi kambini.

Lengo lilikuwa kuvitenga mbali na ushabiki wa kisiasa, vyombo vyote vya kusimamia masuala ya ulinzi na usalama wa mipaka; amani na utulivu wa raia, ili daima viwe tiifu kwa taifa na si kwa vyama wala viongozi wa vyama.

Ni kweli viongozi wa vyama vya upinzani wanaweza kuvunja amani ya nchi, kadhalika chama tawala na viongozi wake pia, kwa vile ni wanadamu , wanaweza kuvunja amani kwa tamaa ya kupenda kubaki ikulu. Hilo likitokea, vyombo vya dola lazima viwe na ujasiri wa kukidhibiti chama tawala na kiongozi wake kwa sababu amani ya nchi si mali ya mgombea wa chama tawala wala si mali ya chama chake.

Ndiyo maana kila mpenda amani, alishangazwa na kitendo cha Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Luteni Jenerali Abdulrahman Shimbo kujitokeza kutoa matamshi makali. Tamko la Luteni Jenerali Shimbo, ambalo lilitolewa bila sababu za msingi, wiki iliyopita, limeonyesha ushabiki wa kisiasa wa ofisa huyo wa jeshi na jinsi chama tawala kinavyotaka kutumia jeshi kujihalalishia kubaki ikulu.

Lakini ushabiki wa kisiasa wa kamanda yeyote wa jeshi, kama alivyoonyesha Jenerali Shimbo, si lazima uwe ndio ushabiki wa askari anaowaongoza. Tayari, baada ya yeye kutoa tamko hilo, makamanda wengine wa vyeo vya juu wamesikika wakimpinga na kudai watamuumbua. Hiyo si afya njema kwa taifa, ni hatari na ndiyo sababu sheria ilitungwa kuwatenga kabisa na masuala ya siasa.

Katika mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM mjini Dodoma mwaka jana, walikuwa na agenda Na 14 ambayo ilisema “kupata makada katika vyombo vya dola”. Kwa kuzingatia kwamba serikali ya CCM bado inateua wanajeshi kuwa wakuu wa mikoa na wilaya kinyume cha sheria ya vyama vya siasa, Luteni Jenerali Shimbo anaweza kuwa matunda ya mjadala wa agenda Na 14.

Hii si mara ya kwanza kushuhudia majeshi yakijiingiza kutishia demokrasia. Kila unapofika uchaguzi mkuu jeshi limekuwa likitishia wananchi—Zanzibar wana uzoefu na hili.

Tanzania bara wana uzoefu na uchochezi unaofanywa na Jeshi la Polisi. Katika uchaguzi mkuu mwaka 2005, Jeshi la Polisi lilivitishia vyama vya upinzani na lilifika kudai kuwa Chama cha Wananchi (CUF) kimeingiza silaha.

Kwa kuwa kauli ile ilitolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Omari Mahita, ambaye alionyesha mabati akidai ni sialaha kutoka nje, watu waliamini wakakinyima kura. Mahita alipostaafu, alirudi kwao Morogoro akatangaza nia kuwania ubunge kupitia CCM. Alijiunga lini hadi CCM wakaona anawafaa?

Hata mkuu wa majeshi, Jenarali Robert Mboma alipostaafu alirudi Mbeya akatangaza kuwania ubunge kupitia CCM. Pia aliyekuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Alfred Tibaigana aligombea ubunge kupitia CCM. Kwa hiyo, tishio hili la Luteni Jenerali Shimbo halikuja kwa bahati mbaya ni mfululizo wa utiifu wa wanajeshi kwa chama tawala badala ya taifa.

Luteni Jenerali Shimbo, kama ilivyokuwa kwa IGP Mahita mwaka 2005, ametoa matamshi makali mbele ya vyombo vya habari, akitishia kuwa jeshi litapambana na kuhakikisha “damu” haimwagiki na matokeo ya uchaguzi yanakubalika.

Kauli hiyo inamaanisha, mshindi hatapatikana kutokana na kura zitakazopigwa 31 Oktoba 2010, bali kwa utashi wa JWTZ.

Tunafahamu kwamba Jeshi halina kawaida kuingia mahali bila kupewa amri na Amiri Jeshi. Mathalani majeshi ya Uganda yalipovamia mwaka 1978, majeshi hayakujibu mashambulizi; yalisubiri tamko la Amiri Jeshi, Rais Julius Nyerere.

Kazi ya jeshi ni kulinda amani na usalama wa mipaka na pale linapoingia ndani basi ni pale kikosi kimoja au kikundi fulani kimeasi kama ilivyotokea mwaka 1982. Kama hakuna matukio hayo jeshi hufanya shughuli nyingine za kujenga taifa kama kujenga barabara, madaraja, kushiriki uokozi na kusaidia kulinda amani katika nchi nyingine kwa ombi la Umoja wa Mataifa (UN) au Umoja wa Afrika (AU).

Nani aliyemwomba Luteni Jenerali Shimbo ahutubie wakati hakuna kikosi kilichoasi? Jeshi alipata wapi mamlaka ya kuzungumzia uchaguzi na matokeo yake? Kwa hiyo, tujue walitumwa na rais ambaye kwa sasa ni mgombea tu? Kwa nini tusiamini chama tawala kinataka kuanzisha vurugu ili kishinde kwa nguvu?

Simfahamu Luteni Jenerali Shimbo na wala sidhani kama ni muhimu kumjua yeye binafsi. Nina shida na matumizi ya nafasi yake kuwatisha Watanzania wanaojiandaa kutumia haki yao ya msingi kupiga kura ili kudumisha uongozi uliopo au kuuondoa na kuweka mwingine.

Nasisitiza, kazi ya jeshi ni kulinda mipaka ya taifa isiingiliwe na maadui wa nje. Vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi ni vya Watanzania, hakuna chama hata kimoja kilichosajiliwa nje ya nchi kiasi cha kusababisha jeshi liingilie kati ili kulinda mipaka ya taifa letu.

Kazi ya kulinda raia na kutunza amani ya ndani ya nchi ni ya polisi na vitengo vyake. Kitendo alichokifanya Luteni Jenerali Shimbo, ni kuvuruga amani na ingestahili IGP, Said Mwema (ambaye hakuwepo), amkamate kwa kuvuruga amani na kuchochea maasi ndani ya nchi.

Ikumbukwe kuwa jeshi haliko juu ya sheria. Kwa kitendo alichofanya Shimbo, sasa tumejua kwa nini askari wanapenda kujichukulia sheria mkononi na kuwapiga raia wasio na hatia.

Tamko la Shimbo limezua maswali mengi yenye utata: Kwanza, ni kwa nini tamko hili limetolewa naye na siyo Mkuu wa majeshi Jenerali Davis Mwamunyange? Kwa nini hakuwepo IGP, Mwema? Wanataka mambo yakiharibika wajitenge kwamba hawakuhusika?

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: