Ukitaka kudanganya, usimtumie Kova


Kondo Tutindaga's picture

Na Kondo Tutindaga - Imechapwa 18 July 2012

Printer-friendly version
Uchambuzi

KUNA hatua za makusudi zinazofanywa na serikali na vyombo vyake, kuzua mambo na kudanganya katika sakata la utekaji na uteswaji wa Dk. Steven Ulimboka.

Lengo la hatua hizo, ni kuhamisha mjadala na kupunguza kelele zinazosuta hatia ya yeyote aliyehusika na tukio hili la kinyama.

Kwa kuwa upotoshaji huu unafanywa na vyombo vya serikali, watazamaji hatuna njia nyingine ya kuamua ukweli juu ya jambo hili zaidi ya kuamini kuwa serikali inahusika moja kwa moja. Kama serikali haihusiki, kwa nini ipoteze muda kupotosha na kuchakachua uchunguzi huu usio huru?

Siku moja baada ya kutekwa kwa Dk. Ulimboka na baada ya yeye kupatikana akiwa katika hali mbaya, zilivuja taarifa kuwa kulikuwa na mpango wa kutoa kafara majambazi sugu kadhaa kutoka katika magereza ya mikoa ya kusini.

Habari zilieleza kuwa, majambazi hao wangeuawa maeneo fulani ya mkoa wa Pwani na kutangaza kuwa walikuwa ni majambazi waliomteka Dk. Ulimboka na kuwa wameuawa katika mapambano na polisi. Baada ya kuvuja kwa mpango huo, watekelezaji waliusitisha.

Zikafuata tetesi za makusudi kuwa ndugu wa wagonjwa waliokufa wakati wa mgomo wa madaktari ndio waliomteka Dk. Ulimboka ili kulipa kisasi kwa kufiwa na ndugu zao. Kumbe ilikuwa ni ndugu hao waliotajwa kujiapiza kulipa kisasi katika hospitali ya Muhimbili, wanafahamika lakini mpaka sasa hakuna aliyekamatwa wala kuhojiwa juu ya utekaji wa Dk. Ulimboka.

Kisha zikamiminwa tetesi na hata kuandikwa na baadhi ya vyombo vya habari, kuwa Dk. Ulimboka alitekwa na madaktari wenzake. Iliandikwa kuwa madaktari hao walimshtukia kuwa alikuwa anaelekea kuwasaliti mbele ya serikali.

Habari hizo zikaandikwa kwa kujichanganya kuwa madaktari hao – watekaji wa Dk. Ulimboka – walishtuka  kuona Dk. Ulimboka amebadilika kiuchumi kwa kumiliki gari na simu za bei ya juu.

Hawa madaktari wakaamua kumteka na kumtesa. Hakuna daktari aliyekwishakamatwa kuhusiana na tukio hili.

Ndipo mwishoni wa wiki iliyopita, akaibuka Suleiman Kova, kamanda wa polisi kanda Maalum ya Dar es Salaam. Akasema polisi wanamshikilia rais mmoja wa Kenya, aliyekiri mwenyewe kuhusika na utekaji na uteswaji wa Ulimboka.

Maelezo ya Kova, mwonekano wake mbele ya kamera za wana habari vikaacha mashaka mengi kuliko matumaini. Madai yake yakaenda mbali na kuingilia eneo la hatari kuwa jambazi huyo kutoka Kenya alitubu kanisani Kawe kuwa alimteka Dk. Ulimboka na kuwa alitumwa na watu asioweza kuwakumbuka.

Cha ajabu, Kova akasema mtuhumiwa huyo amefikishwa mahakamani!

Lakini juzi Jumapili, kiongozi wa kanisa la Kawe akaibuka na kukanusha taarifa hizo za polisi na kukemea tabia ya vyombo vya dola na serikali kuyatumia makanisa katika masuala machafu kama hilo.

Lakini, kana kwamba hata yeye alisubiri asingiziwe ndipo aibuke kusema yaliyo moyoni mwake, akawataka madaktari warudi kazini mara moja.

Kuwataka madaktari kurudi kazini kabla ya kuwasikiliza na kuisikiliza serikali ni sawa na kusema, asiyerudi kazini atatekwa kama Dk. Ulimboka.

Si mara ya kwanza kwa Kova kutumiwa kuhadaa umma juu ya masuala ya uhalifu unaofanywa na mfumo au serikali. Ameonekana mara kwa mara mbele ya vyombo vya habari akihangaika kudanganya na kutoa visingizio vingi vinavyokera.

Makundi ya wana harakati yanapotoa taarifa polisi ili kuandamana, yeye huibuka na visingizo vya kisiasa ili kuwazuia. Mara aseme hakuna polisi wa kutosha, mara kuna kundi jingine litawapinga na kusababisha ghasia, mara masuala yanayolalamikiwa yanajadilika, mara kuna wageni wanatarajiwa kuingia mkoani kwake na vingine vinavyoumbua utu wake kama kamanda wa polisi.

Tabia hii ya Kova inawakera hata wakuu wake. Mara kadhaa ameonywa na wakuu wake katika semina na mikutano yao ili aachane na jazba inayomfanya aonekane ni mkereketwa wa upande mmoja mbele ya jamii.

Jeshi la polisi ni tumaini la raia wote wanaotafuta haki. Kitendo cha Kova kuegemea upande fulani au kushabikia uhalifu wa kimfumo, unaondoa kabisa imani ya wananchi kwa jeshi hilo.

Kwa upande mwingine, serikali imeonyesha udhaifu mkubwa na wa hatari kwa kujaribu kuchezea suala hili nyeti.

Kumtumia Kova katika mchakato unaohitaji umakini katika kuwasilisha taarifa kwa umma, ni kosa linaloweza kuigharimu.

Kwa vyovyote, operesheni hii kufunika aibu ya serikali inashirikisha vyombo vingi nyeti vya dola. Serikali makini inayojaribu kufunika makosa ya serikali inahitaji kutumia maafisa wenye weredi wa hali ya juu ya kupima kila hatua inayopigwa.

Ukiachilia mbali uwongo wa wazi katika sakata zima la kujaribu kumtumia Mkenya wa bandia, hata kumtumia Kova katika kuufanikisha uwongo huo ni kosa kubwa la “Ki-operesheni funika ukweli.”

Tayari Kova alionyesha kiburi cha ajabu mbele ya wana habari siku mbili baada ya Dk. Ulimboka kutekwa, pale aliposema ni lazima polisi iongoze uchunguzi wa tukio hili kinyume na madai ya uundwaji wa tume huru.

Hii ilikuwa ni baada ya umma kumkataa Ahmed Msangi kuwa mjumbe wa tume iliyoundwa kuchunguza sakata hili.

Si kawaida mtu kukataliwa halafu wewe mwenyewe ukajitetea kwa nguvu kuwa lazima uwemo katika tume ya kuchunguza uhalifu. Hata mahakimu na majaji, wanapotiliwa mashaka na wenye kesi, hujiondoa pasipo ubishi wowote.

Kwa mara nyingine, mkono wa idara ya usalama unaonekana wazi ukiwa umejaa damu ya Dk. Ulimboka. Mkono huo uliotapakaa damu, unahangaika kuwachafua polisi na Kanisa la Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Mchungaji Gwajima.

Kwangu mimi, kutajwa kwa kanisa hilo si kwa bahati mbaya. Yawezekana kuna mengi yanayofunikwa na kwa bahati mbaya Kova amefanya kosa katika uwasilishaji wa taarifa na kuharibu mpango mzima.

Ni kanisa hili ambalo wanalitumia wanasiasa wengi kutapika nyongo zao. Nyuma ya pazia kuna tetesi kuwa wana usalama wetu wasioaminika, ama kwa kujituma au kutumwa, wanamtumia Mchungaji Gwajima kwa maslahi ya kidola au kisiasa.

Ikiwa tetesi hizi ni kweli, basi sakata la utekwaji na utesaji wa Dk. Ulimboka, kwa mara nyingine linachukua sura mpya. Kiongozi wa dini anayetumiwa na dola kufunika uhalifu wa dola, si ajabu hata yeye ana uhalifu unaofunikwa na dola hiyo hiyo.

Matamshi ya Kova katika ripoti iliyoandaliwa kiufundi hata kumshinda yeye mwenyewe kuisoma kwa usahihi yaashiria jambo kubwa nyuma ya pazia.

Ingekuwa bora, serikali iharakishe uundwaji wa tume huru ili kuepusha watu wengi zaidi kuchafuliwa na sakata hili la Dk. Ulimboka. Kujaribu kuunda masakata mengine kama njia ya kufunika mjadala huu, haitasaidia safari hii.

tutikondo@yahoo.co.uk
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)