Ukitaka meza wembe, Chenge haguswi


Mbasha Asenga's picture

Na Mbasha Asenga - Imechapwa 24 March 2010

Printer-friendly version
Tafakuri
Aliyekuwa Waziri wa  Miundombinu, Andrew Chenge

“SAFARI hii tumekuwa makini sana katika kufikia mkataba na Rites kuendesha TRL,” hii ilikuwa ni sehemu tu ya kauli ya aliyekuwa Waziri wa Miundombinu, Andrew Chenge.

Chenge alikuwa akijibu swali gumu kutoka kwa waandishi wa habari kwamba ni kwa kiwango gani serikali ilikuwa imejipanga katika kuingia mkataba na Rites. Hiyo ni kutokana na kashfa mbalimbali zilizowahi kuikuta serikali katika masuala ya mikataba.

Kampuni hiyo ya serikali ya India, ndiyo kwanza ilikuwa imepewa kazi ya kuendesha TRL, zamani likijulikana kama Shirika la Reli Tanzania (TRC). Utiwaji saini huo ulifanywa katika ofisi za PSRC, jijini Dar es Salaam kati ya Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya RAHCO, Agnes Bukuku na Mkurugenzi wa Kampuni mpya ya TRL, Sundhir Kumar Seth

Chenge aliyasema hayo kwa kuwa alikuwa anafahamu si tu ugumu wa kupatikana kwa mwendeshaji wa TRL bali pia magumu yaliopitwa.

Kwa kauli yake, mbali ya kukiri kwamba mchakato wa kuibinafsisha TRC ulipitia mlolongo mrefu pamoja na vikwazo mbalimbali, bado alikuwa anaamini kwamba Rites ndio walikuwa watu sahihi wa kukabidhiwa TRL au tuseme tu TRC.

Kwa mfano, angalia kauli hii nyingine ya Chenge siku hiyo hiyo akiwatoa Watanzania hofu kuhusu uwezo wa Rites: “Serikali inaamini kuwa kampuni mpya itaboresha huduma ya usafiri wa reli nchini na kwa nchi jirani, hasa baada ya kukamilika kwa mpango wa awali wa uwekezaji.”

Ikumbukwe kwamba Chenge alikuwa anazungumza kama waziri mwenye dhamana na shirika hilo kwa kipindi kifupi tu, kwani alikuwa amehamishiwa Miundombinu akitokea Ushirikiano wa Afrika Mashariki baada ya kufanyika kwa mabadiko ya baraza la mawaziri kutokana na kashfa ya Richmond

Hata hivyo, kuwepo kwake kwenye serikali ya awamu ya tatu kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa miaka yote 10 ya utawala wa Rais Benjamin Mkapa, kulikuwa kunampa fursa ya kujua mikataba yote ya uuzaji wa mashirika ya umma ilivyokuwa imesukwa kwa sababu si kawaida kwa serikali kujifunga kwenye mkataba wowote bila mwanasheria mkuu kuhusika kutoa ushauri wa kisheria kwa nia ya kulinda maslahi ya serikali.

Wiki iliyopita, nilizungumiza habari ya serikali kutangaza kuchukua hisa asilimia 51 za TRL kuwa ni sawa na ule msemo wa ‘wa moja havai mbili, hata akiivaa humdondoka.

Nilijitahidi kutambaa huko na huko kueleza jinsi tulivyo taifa la kuliwa, leo ninaendelea na kibarua changu kuwa kumhusisha Chenge na uchafu huu kwa sababu ni mtu ambaye kwa hakika ametajwa katika machafu mengi, lakini kwa kuwa sera za chama tawala ni za kulindana, mwanasiasa huyu anaonekana kuwa ni lulu badala ya hasara kubwa kwa taifa.

Leo ningependa Chenge huko aliko ajitokeze basi na asimamie zile kauli zake alizotoa takribani miaka miwili iliyopita juu ya TRL na umakini wa serikali katika kumpa Rites reli aivuruge kiasi cha kuicha hoi bin taaban kama si marehemu.

Yu wapi Chenge aseme vikwazo na magumu ambayo serikali ilivuka hadi kufikia maamuzi ya kumpa Rites reli ambayo leo hii hatuwezi hata kuthubutu kusema kwamba Tanzania ina miliki miundombinu ya namna hiyo? Yu wapi Chenge, amejichimbia wapi?

Juzi kaulizwa swali akiwa huko jimboni kwake Bariadi Magharibi juu ya TRL, jibu lake ni lile lile la kujificha, kwamba hayuko tena serikalini, kwa maana hiyo waulizwe walioko madarakani kwa sasa. Kweli?

Chenge leo hana la kusema juu ya madudu yaliyojaa kila kona ya nchi hii ndani ya serikali hii kutokana na mikataba ya ovyo mno ambayo waasisi wake ni watu kama yeye?

Leo ninaomba CCM itueleze Watanzania kama kuna watu waliowahi kufanya maamuzi ndani ya serikali wakitimiza wajibu wao, na sasa wanashitakiwa mahakamani kwa sababu ya maamuzi mabaya, hivi Chenge ana kinga gani? Kwa nini hashitakiwi kama wengine au ni ile ile sera iliyoua nchi, iliyoangamiza taifa mpaka kuharibu mayai na mazalia yake ya, ‘huyu ni mwenzetu’.

Sera ya huyu ni mwenzetu itatufikisha wapi, na ni nani atalipa gharama yake kama si wananchi wenye nchi yao ? Hivi Chenge anafikiri kwa sasa hivi wanaotaabika kwa kukosa usafiri nafuu ni nani kama si hao hao wapiga kura wake waliokuwa wanaitegemea Reli ya Kati?

Nani asiyejua kwamba Reli ya Kati ilikuwa mkombozi wa mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Tabora, Kigoma, Singida na Dodoma . Lakini zaidi sana mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Tabora na Kigoma!

Kwa hali hii, uwajibikaji wa Chenge akiwa pale Miundombinu si tu ulileta hasara kwa serikali juu ya TRL, bali kwa wapigakura wake wa Bariadi na ndugu zake wote wa mkoa wa Shinyanga.

Ndiyo maana ninajiuliza maswali mazito kila wakati, hivi ili uonekane umefanya makosa katika nchi hii yanayostahili kushitakiwa, kufilisiwa na kwa kweli utangazwe mtu hatari kwa ustawi wa nchi; mpaka ufanye nini?

Yaani haya yote aliyotutendea Chenge kama taifa kuanzia kwenye ununuzi wa rada ambayo sasa hakuna ubishi ni rushwa tupu, ushauri wote aliotoa kwa serikali katika mchakato wa uuzaji wa mashirika yote ya umma kuanzia mwaka 1995 – 2005, hivi huyu hana alipoikwaza serikali kiasi cha CCM kumkumbatia kiasi hili? Hii ni lulu ya wapi na ya nani?

Wiki iliyopita magazeti kadhaa yalisema kwamba Rites hawakuwahi kulipia hata senti moja hisa zake asilimia 51 za TRL, lakini isisaulike kwamba inaidia serikali mabilion ya fedha kwa kukodishwa kwa mabehewa yake ambayo hayakufanya kazi kwa sababu ya uzito wa kazi iliyokumbana nayo; lakini kwa sababu mikataba ya kukodi mabehewa haya ilikuwa imechomekwa kipengele kama kile cha mikataba ya kuzalisha umeme wa dharura wa IPTL, Songas, Richmond/Dowans yaani ‘capacity charges’ basi tusubiri chamtemakuni juu ya ulipaji wa fidia kwa Rites katika kuvunjwa kwa mkataba wa kuendesha TRL.

Mwaka baada ya mwaka, hali inazidi kuwa mbaya na ngumu katika kufunga mikataba, watu wakiwa wale wale, lakini kibaya zaidi wakiwa hawafanywi lolote; hawa ndio akina Chenge ambao CCM imejaa mfukoni mwao hata wananchi walalamike vipi, hata aonekane na mawaa gani huyo ni wao.

Ukitaka meza wembe, Chenge anaendelea kudund. Ni Mwenyekiti wao Kamati ya Maadili ya Kamati Kuu ya CCM, chombo chenye heshima kubwa! Watanzania tuendelee kulia.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: