Ukiua ufisadi utakuwa umeua CCM


Mwandishi Maalum's picture

Na Mwandishi Maalum - Imechapwa 21 September 2011

Printer-friendly version
Kisima cha Mjadala

ILIPOTANGAZWA kuwapo kwa mradi wa kujivua gamba ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baadhi yetu tulitabiri mapema kwamba hizo ni ghiliba na pengine ni sehemu ya sherehe za kuadhimisha miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM.

Ni kwa sababu, ufisadi ni sehemu muhimu ya utambulisho ndani ya chama hiki; kuuondoa ufisadi ndani ya CCM ni sawa na kusema unataka kukiua chama chenyewe.

Kwa kiwango kikubwa CCM ndiyo iliyolea na kustawisha ufisadi ndani ya nchi na kwa hiyo kuubomoa ufisadi kwa namna yeyote ile ni sawa kubomoa na kusambaratisha misingi ya nchi.

Mathalani ukisema utaondoa rushwa katika uchaguzi au kuharamisha rushwa hiyo, waweza kujikuta huna rais, wabunge wala madiwani. Lakini pia ukiharamisha mhimili huo kwa msingi kuwa ulichaguliwa kifisadi, waweza kujikuta ukiharamisha mhimili mwingine ambao unateuliwa na mhimili wa serikali kama vile mahakama na serikali.

Kwa hiyo waweza kujikuta unahoji teuzi zote za majaji wa mahakama, mawaziri, wakuu wa mikoa, wilaya, wakuu wa vyombo vya dola na wateule wote wa rais. Kuthubutu kuondoa ufisadi na rushwa katika CCM laweza kuwa janga la kitaifa.

Kwa uchache, tulipofikiria haya, tuliona Rais Jakaya Kikwete anafanya utani pale alipodai kwamba chama chake kinajiandaa kujivua gamba la ufisadi kwa kutaka kuwatosa viongozi ambao ni “mzigo kwa chama.”

Sababu ni mbili: Kwanza, tulidhani hawezi kulikashifu titi linalomnyonyesha. Unahitajika ujasiri ulio karibu na ujasiri wa kifisadi kulipiga teke titi lililokunyonyesha. Kikwete ni tunda la ufisadi kwa kutaka au kutotaka kwake.

Anajua na kukiri kuwa rafu za kifisadi zilimfikisha hapa alipo. Kwamba hata hali yake ya uchumi binafsi aliyonayo kwa sasa, si tunda la mshahara wake wa urais bali ni mchanganyiko wa mafao ya “huku na kule.” Kwa yeye kuwa kiongozi wa kupambana na ufisadi basi, linakuwa jambo gumu na lisilotegemewa.

Pili, viongozi wa vyombo vya dola kwa kiapo na matarajio ya wananchi, hawatarajiwi kuwa watamtegemea rais katika utendaji kazi wao. Yaani kama ni waadilifu hawahitaji maoni ya rais kujua kama mtu fulani ni fisadi au si fisadi.

Tumeshuhudia viongozi wote wanaoshughulikia vita dhidi ya ufisadi, kama vile Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU), Mkurugenzi wa mashitaka nchini (DPP), Mkurugenzi wa makosa ya Jinai (DCI), mkuu wa jeshi la polisi nchini (IGP) na wengineo, ni kama matarishi wasio na utashi katika kutenda kazi zao. Wanatetemeka mbele ya mafisadi na wanahitaji ruhusa kuwashughulikia.

Hivyo basi, Kikwete akiamua kukaa kimya kwa kisingizio cha kutowaingilia katika kazi zao, basi nao hukaa kimya kwa kisingizio kuwa hawapaswi kuingiliwa na yeyote; lakini kimya hicho cha rais na wateule wake kina maana ya kuwalinda mafisadi.

Vikao vya CCM  vilipokaa na kuhitimisha kwa kutangaza kuwa chama kimevunja Kamati Kuu (CC), kimesambaratisha sekretariati yake na kisha kuwapa siku 90 watuhumiwa wa ufisadi, baadhi yetu tuliona tena, kwamba huu ni mkwara wa kawaida kisiasa; wenye lengo la kujaribu kufanya wanachama waaminifu wasikate tamaa haraka.

Maamuzi hayo yalijaa kasoro nyingi na kukosa mwelekeo wa utekelezaji. Wote tumeshuhudia mathalani, sekretariati nzima ikijifungia ndani siku kadhaa kuandika barua tatu. Watu wazima na akili zao wanashindwa au wanasitasita kuandika barua na kuishia kulumbana na watu katika vyombo vya habari kuhusu barua hizo.

Mara tukasikia barua ziko mezani kwa Pius Msekwa, makamu mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, mara Wilson Mukama, katibu mkuu wa chama hicho anasita kuzisaini na kudai zipelekewe kwa mwenyekiti wa chama, Rais Kikwete.

Mara tukasikia unatafutwa ushauri mara mbili kutoka kwa viongozi wastaafu na hata baadhi yao kuwakatalia kuwa hilo suala lisimamiwe na sekretariati. Lakini tahadhari ikawa ni jinsi gani viongozi hao wastaafu hawatachonganishwa na wanaowaita CCM “mafisadi.”

Wakati hayo yanatokea, mwenyekiti wa chama alikuwa katika mashinikizo makali ya kuombwa kukutana na watuhumiwa hao wa ufisadi ambao ni maswahiba wake wa siku nyingi.

Mwenyekiti akajikuta ana sekretariati mbili – moja ikiwa ofisi ndogo ya makao makuu ya chama Lumumba na sekretariati nyingine ikiwa ni ile ya watuhumiwa ambao nao walifaulu kumyumbisha.

Kama kawaida yake, Kikwete alifanikiwa kuyatia moyo makundi yote kwa lengo la kufurahisha kila mmoja. Aliwaambia watu kuwa sekretariati ya chama inayoongozwa na Wilson Mukama (Katib u Mkuu), ina ridhaa yake ya kusema chochote bila kumung’unya maneno.

Lakini wakati huohuo akawaambia watuhumiwa wa ufisadi kuwa wasiwe na wasiwasi maana Watanzania ni mafundi wa kupiga kelele; kinachotekelezwa na Nape Nnauye, katibu mwenezi na itikadi wa CCM, ni mambo yake binafsi.

Huu ni mchezo wa hatari sana kwa wote watatu yaani – sekretariati ya chama, watuhumiwa wa ufisadi na Kikwete mwenyewe. Ni hatari kwa sekretariati ya chama kwa sababu itajidanganya sana ikidhani mwenyekiti wao anaweza kuwasimamia wao watakapobanwa na hoja za wanachama juu ya upotoshaji walioufanya katika kutekeleza hicho walichoita, “Mradi wa kujivua gamba.”

Katika masuala ya kusimamia mtu aliyewajibika vizuri katika nafasi yake, Kikwete hajawahi kuaminika. Sekretariati licha ya kuwa na maamuzi ya vikao halali vya chama – hata kama maamuzi hayo yapo – bado wanatakiwa “kuchanganya na akili zao” katika kutekeleza maagizo hayo yanayoweza kugusa maslahi binafsi ya mwenyekiti au kundi lake.

Kwa upande wa watuhumiwa wa ufisadi, nao ni hatari kumwamini Kikwete pale wanapowasiliana naye; iwe ni ana kwa ana au ujumbe wa simu. Kikwete anaamini sana katika falsafa ya mafisadi wanajimaliza wenyewe na kwa hiyo tuwaache wajimalize bila kuwapa msaada wowote wa kujimaliza.

Si mara moja wala mbili, watuhumiwa hawa wa ufisadi wamemwambia Kikwete, kwamba chama kimedandia agenda ya upinzani, husasani CHADEMA. Kwamba kung’ang’ania agenda hii kutakifikisha chama na hata Kikwete mwenyewe kubaya.

Ni Kikwete huyuhuyu anayeweza kuchelewesha kikao tangu asubuhi mpaka jioni akiruhusu watu waongee bila mwelekeo wa mapatano ili wapumue. Kwa hiyo, anaweza kuwaruhusu watuhumiwa wamwone ili kupumua hisia zao.

Kimsingi watuhumiwa mbele ya Kikwete ni kama wafungwa wa kifungo cha nje; anaweza kuwageuka kama alivyowageuka huko nyuma. Salama yao kwa sasa ni kujipanga kupambana naye.

Kwa upande mwingine, hatua yeyote ya kupambana na ufisadi kwa CCM ni sawa na kufagilia CHADEMA. Nina maana kuwa licha ya kuwa agenda hii ilianzishwa na CHADEMA na kupuuzwa na CCM kwa muda mrefu, lakini kupambana na ufisadi ndani ya CCM kutaidhoofisha zaidi CCM na kukijenga CHADEMA mbele ya umma.

Ili CCM kiweze kuaminika kinapambana na ufisadi, itabidi kifukuze watendaji wengi, jambo ambalo linaweza hata kukidhoofisha zaidi chama chenyewe.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: