Uko wapi udini anaosema Kikwete?


John Aloyce's picture

Na John Aloyce - Imechapwa 05 January 2011

Printer-friendly version
Jamvi la Weledi

UCHAGUZI mkuu wa madiwani, wabunge na rais, umekwisha. Hata hivyo, yaliyojiri wakati na baada ya uchaguzi yataendelea kukumbukwa.

Akizindua bunge la 10 mara baada ya uchaguzi, Rais Jakaya Kikwete alisema, “Uchaguzi huu umeacha majeraha mengi.” Lakini akataja udini.

Walio karibu naye wanasema kuwa hata katika maandalizi ya hotuba yake, rais alitaja hadi watu anaodai wanahusika na jeraha hili wakiwamo viongozi wa dini na wana habari.

Miongoni mwa kazi za watu walio karibu na rais, ni kueneza uvumi; na kwa kuwa hili la kutaja majina ya watuhumiwa wa udini linaangukia mrengo uleule, basi si vema kulijadili.

Lakini ni vema kujiuliza kwa nini Rais Kikwete amechagua jeraha la udini wakati kuna majeraha mengi yameachwa na uchaguzi huu?

Kwanza, kuna jeraha la wizi wa kura. Baaadhi ya vyombo vya habari, vilinukuu hatua kwa hatua kilichotendeka na njia zilizotumika. Rais hakuzungumzia jeraha hilo.

Pili, lipo jeraha la rushwa katika uchaguzi. Hili si jeraha tena. Ni dondandugu. Donda hili lilianzia ndani ya chama cha Kikwete mwenyewe.

Mchakato wa kura za maoni ulikihamisha chama kutoka kusimamia misingi ya uchaguzi, hadi gulio la ununuzi wa kura. Hili, rais halioni.

Kuna jeraha la vyombo vya dola, hasa usalama wa taifa na polisi kutisha kuwapiga na kuwajeruhi wapigakura kwa lengo la kukisadia chama tawala kushinda uchaguzi.

Wapo wanaodai kuwa, hata kujitokeza kwa wapigakura wachache kulitokana na vitisho vya dola dhidi ya wananchi.

Hakika, majeraha ni mengi. Lakini Rais Kikwete amechagua jeraha moja la udini na kuamua kufa nalo. Nami, nitajadili hilo kama lilivyojitokeza katika hotuba ya rais.

Kwanza, wakati Jakaya anagombea urais mwaka 2005, alikuwa muislamu.

Ndani ya chama chake, Kikwete aligombea na wakristo wengi, lakini akachaguliwa yeye kubeba bendera ya chama.

Katika uchaguzi mkuu wa 2005, akagombea na wakristo, miongoni mwao ni Freeman Mbowe kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

Wakristo wakamuacha mkristo mwenzao Mbowe, wakamchagua yeye.

Mwaka 2010, Kikwete aligombea urais akiwa bado na dini yake ileile. Amegombea akipambana na baadhi ya wakristo. Hakushinda kwa kishindo kama alivyotarajia.

Wapo wanaosema hata kushinda hakushinda, ingawa wapo wanaoamini kuwa alishinda, lakini si kwa kiwango ambacho kilitangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC).

Hapa ndipo anapoibuka na dai la udini. Kwa dhati naamini kuwa wapigakura walimjua kuwa ni muislamu 2005 na 2010. Kilichobadilika ama ni ufahamu wa wapigakura au uwezo wa kuongoza wa Jakaya.

Ninapata shida kuamini kuwa mabadiliko haya kama yana uhusiano na dini ya Jakaya au dini ya waliopiga kura.

Jambo la pili, nashawishika kuamini kuwa Kikwete muislamu, anapotamka neno “viongozi wa dini” ambao walitumia udini, atakuwa ana maana ya wale wasio wa madhehebu yake.

Kuna taarifa kwamba mara kadhaa amelalamika katika vikao vya ndani ya chama kuwa maaskofu hawampendi.

Siku chache kabla ya uchaguzi, kuna madai kuwa baadhi ya wakuu wa mikoa waliagizwa kuwaita “viongozi wa dini” ili kuwaeleza “masikitiko ya rais juu yao.”

Hata hivyo, walioitwa katika mikutano hiyo, walikuwa maaskofu tu. Mmoja wa mawaziri wa Kikwete Benard Membe alikwenda hadi Mwanza kukutana na viongozi wa kidini. Ujumbe aliokwenda nao na ule aliorudi nao, hakuna anayefahamu.

Sasa kwa ujumla, tathmini ya uchaguzi mkuu ndani ya CCM imegeuka zoezi la kutafuta mchawi aliyesababisha ushindi mdogo kwa CCM na Kikwete.

Rais Kikwete anaujua ukweli, lakini ameamua kuukwepa. Kwamba mwaka 2005 wakati anajitosa kwa mara ya kwanza, watu wengi walikuwa hawamfahamu kwa undani.

Miaka mitano ya utawala wake, imeonyesha nyufa za kutisha katika uwezo wake wa kufanya maamuzi na uwezo wake wa kusimamia “maisha bora” aliyoyaahidi.

Hata ndani ya chama chake, ipo migawanyiko mikubwa inayohatarisha hata uhai wa chama chenyewe. Miaka mitano imetosha kuonyesha wananchi uwezo wake katika kushughulikia mipasuko hiyo.

Kwa hiyo, wapiga kura kumkataa mwaka huu, waliona uwezo wake, wakapima kauli zake na wakaangalia matendo yake. Wengi walikataa chama chake, ingawa walikuwa hawana matatizo sana na mgombea.

Sehemu nyingi CCM hakikubaliki. Waliokikataa chama si kwa sababu ya udini, bali kwa sababu viongozi wake wamekumbatia maovu.

Liko kundi jingine japo ni dogo ambalo halina shida na Kikwete, halina shida na CCM kama taasisi, lakini lina shida na umakini wa sera za CCM.

Hawa nao hawakumchagua Kikwete kwa sababu hakuwa na sera zinazovutia, ukilinganisha na wapinzani wake. Hawa hawakuongozwa na udini. Waliongozwa na utashi binafsi.

Liko suala la ufisadi katika mjadala wa kitaifa. Chama cha Kikwete kilidhani jambo hili litapita kama yalivyowahi kupita mengi.

Jitihada za kuwafikisha baadhi ya vigogo mahakamani hazijasaidia kuzima mjadala. Uamuzi wa kupuuza suala la ufisadi katika kampeni za CCM haukusaidia kupoza mjadala.

Propoganda za makada wa CCM kuwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hakina ajenda nyingine zaidi ya ufisadi, hazikusaidia kuzima kiu ya watu kutaka kujua undani wa ufisadi.

Hii ni kwa sababu, ufisadi hauna dini wala itikadi hata kama unaweza kukumbatiwa bila shida na chama fulani.

Kwa bahati mbaya, hata ndani ya CCM wamo waliojeruhiwa na ufisadi. Wapo waliofukuzwa kazi au kunyimwa haki zao kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo.

Kwa maneno mengine, ajenda ya ufisadi iliwaunganisha wananchi wote bila kujali dini zao na inaendelea kuwaunganisha.

Uamuzi wa mgombea wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa kuufanya ufisadi kuwa moja ya ajenda kuu katika kampeni, uliwafanya wananchi wengi kumuona kuwa ndiye mkombozi.

Kutokana na kuwa CCM imekuwa madarakani kwa nusu karne, ni wazi kuwa mafisadi na wahujumu wa uchumi, watakuwa ni wale walio au waliowahi kuwa katika tabaka tawala.

Mpaka hapa, mchawi wa Kikwete haikuwa misimamo ya waamini na waumini, ni msimamo wake wa kunyamazia ufisadi.

Liko kundi kubwa la wapigakura walioamua kutoipigia kura CCM. Hawa nao walipiga kura kuukataa ufisadi, si dini ya Kikwete.

Nayasema haya kwa sababu, wagombea wa CCM walioanguka kwa ngazi za udiwani na ubunge, wamo waislamu kwa wakiristo. Hali kadhalika walioshinda ni wa kutoka madhehebu mawili.

Ni matusi kuwasingizia wapigakura dhambi ya udini eti tu kwa sababu CCM imeonekana kukataliwa katika sehemu mbalimbali. Anayepalilia fikra hizi ndiye anayepandikiza udini.

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: