Ukombozi waja… kipigo chayoyoma


Ndimara Tegambwage's picture

Na Ndimara Tegambwage - Imechapwa 08 June 2011

Printer-friendly version
Mbunge wa CHADEMA, Lucy Owenya akishambuliwa na polisi

NJIA bora ya kuharakisha mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi nchini Tanzania ni kubughudhi viongozi wa upinzani kila kukicha.

Kamata. Bambika mashitaka. Weka rumande. Peleka mahakamani… Achia kwa dhamana. Kamata. Weka rumande. Fungulia mashitaka…kama jana, kama leo, kama kesho, kila siku.

Wasimamizi wa mradi huu – wakipenyeza amri kwa watekelezaji – wanafikiri kwa njia hii, watafaulu kudhoofisha na hata kuua upinzani dhidi ya serikali chovu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Polisi hawafurahii kukamata. Polisi wanafurahia kubaki na ajira yao. Kubaki na vimshahara vyao. Kubaki ndani ya magwanda yao yanayoelekeza urefu wa kamba yao katika kujikimu.

Polisi wakamataji hawana maslahi katika kukamata viongozi wa upinzani. Wanatii amri ya wakubwa zao. Wakubwa wenye uswahiba na wakubwa siasani.

Wanaotumwa kukamata hawana maslahi katika kufyatua risasi. Katika kulipua mabomu ya machozi. Katika kumimina maji-pilipili machoni mwa wananchi. Hawana!

Ndani ya polisi nako kumejaa “Kabwela hana kitanda” – yule wa kwetu wanaita ndala omwa fulano – mtegemea fadhila!

Watawala wanatoa amri. Polisi wanatii amri. Watawala wanatoa amri kujilinda leo. Leo hii. Kufika au kutofika kesho si hoja kwao. Wanataka leo na ya leoleo.

Kwa hiyo kamata! Bambika mashitaka. Weka rumande. Peleka mahakamani… Achia kwa dhamana. Kamata. Weka rumande. Fungulia mashitaka…kama jana, kama leo, kama kesho, kila siku.

Chukua mfano wa Mbowe, Freeman wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Kijana mdogo tu mwenye mdomo mpana uliojaa ushawishi na uchochezi.

Mbowe, kama Dk. Willibrod Slaa na viongozi wengine wa CHADEMA; akilia wananchi wanaomsikiliza wanalia naye. Akicheka wanacheka naye. Akinuna wananuna naye. Watawala wanaamuru: Kamata. Bambika mashitaka.

Chukua mfano wa CHADEMA. Chama ambacho kimejidhihirisha kuwa na uwezo mkubwa wa kuwafikia wananchi; kuwaibua kutoka lindi la woga na ujinga.

Chukua mfano wa CHADEMA. Chama ambacho kimefuta umaarufu wa bandia wa CCM; kukinyang’anya wafuasi, kukibakizia wanafunzi wanaoswagwa na walimu wanaolinda ajira zao kama polisi.

Chukua mfano wa CHADEMA. Chama ambacho wengi wanasema mgombea wake wa urais alishinda na CCM inakiri nguvu yake ndani ya vikao na kwenye hadhara.

Chukua mfano wa umati wa wananchi unaojitokeza kwenye mikutano ya CHADEMA; maswali yanayoulizwa na wananchi na ahadi wanazotoa ili kung’oa CCM.

Fuatilia kashfa lukuki zilizoizonga CCM na serikali yake; kushindwa kwa chama hicho kujibu hoja kuhusu wizi ndani ya benki kuu; kuhusu matumizi hewa; kuhusu mikataba ya kihuni na ya kinyonyaji.

Kazi ya kisiasa iliyofanywa na upinzani, hasa CHADEMA, Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi, imewezesha wananchi kuelewa kuwa CCM siyo chama cha siasa; ni chama cha ukwapuaji.

Kukua na hata kuimarika kwa vyama vya upinzani, hasa CHADEMA hakutokani na ubora na umakini wa viongozi wake peke yake. Kunatokana pia na mazingira ya kutota kwa waliotawala kwa miaka 50.

CHADEMA wamepata fursa ya kuzunguka nchi na kueleza kuwa mataifa huadhimisha miaka 50 ya uhuru wake kwa kuonyesha utawala bora – kisiasa na kiuchumi.

Lakini katika Tanzania, hasa tunapokaribia
kuadhimisha miaka 50, watawala ndio huonyesha walivyo na makucha marefu ya kupora fedha na raslimali za taifa.

Viongozi wa CHADEMA wamewafafanulia haya wananchi; na wananchi wameelewa kuwa viongozi wengi wa sasa wanashindana kuiba dhahabu, almasi, tanzanite, mbao na raslimali nyingine.

Wamewafafanulia wananchi jinsi viongozi walivyoshiriki ufisadi wa kila aina; wakitoa mifano kadha wa kadha na kuioanisha na yale wanayoona na kufahamu.

Uongo na kutosema ukweli; kutotekeleza ahadi kubwa na nzito kama kununua meli kwa matumizi katika Ziwa Viktoria; kutokamata watuhumiwa wakuu wa ufisadi na tabia ya ndumila kuwili; vyote vimeelezwa kwa wananchi.

Katika mazingira ya kawaida, viongozi wa CCM wanahitaji ujasiri wa mwendawazimu kusimama mbele ya umati kueleza mafanikio, matarajio na kuomba umma kuunga mkono.

Wamewekwa uchi; wao na chama chao. Wamebakia kuanza na kumaliza mikutano yao kwa kusema “sasa tunajivua gamba.” Ndizo hotuba. Ndizo ahadi. Ndizo kinga za aibu.

Huwezi kusikia tena viongozi wa CCM wakitamba na “Ari zaidi, Nguvu zaidi na Kasi zaidi.” Wamezimika. Watani zao hutafsiri ashirio hilo kuwa na kifupi cha “ANGUKA” na huko ndiko CHADEMA inahubiri kuwa wanaelekea.

Ndani ya CCM kwenyewe, mifarakano imeota ndevu. Ni piga nikupige. Kila anayefaulu kuchomoa kizinga anamchoma mwenzake.

Katika mazingira haya ndimo tunakuta: Kamata Mbowe. Kamata Slaa. Kamata Zitto. Bambika mashitaka. Weka rumande. Peleka mahakamani…Fungulia mashitaka …kama jana, kama leo, kama kesho, kila siku.

Mazingira haya yanaibua chuki. Yanaibua hasira. Yanachochea ujasiri wa kiwango cha juu wa kusema, “Hapana. Hatukubali tena kunyanyaswa.”

Hakika hakuna wa kuwanyanyasa. Ambaye angefanya hivyo tayari amewekwa uchi. Anafahamika. Uwezo wake unajulikana. Udhaifu wake ni wazi. Nia yake imeanikwa.

Katika mazingira haya, upinzani tayari ndio tumaini la wengi; tumaini la wote isipokuwa wanaotetema na kugugumia katika “anguka” na “kujivua gamba.”

Hapa kuanguka kwa CCM ni wazi na mabadiliko yananukia.

CHADEMA wamefika kwa wakulima, wafanyakazi maofisini na viwandani.

Sauti za upinzani zimefika hata ikulu ambako baadhi ya watumishi wameeleza kutaka mabadiliko. Hawatajwi majina.

Hata hivyo, kutaka mabadiliko siyo uhaini ingawa “uasi” umewahi kuwa bora kuliko kuishi kwenye utumwa.

Polisi wanaotumwa kubughudhi, kutishia, kupiga na wakati mwingine kuua, nao wanataka mabadiliko.

Wanataka mabadiliko ili wasitumwe tena kupiga baba zao. Kubugudhi mama zao. Kumimina maji-pipili machoni mwa wadogo na wakubwa zao. Kukamata dada zao na hatimaye kuishia kuwa korokoroni kwenye maduka ya walanguzi.

Mabadiliko hayakimbiwi kwa kuwa ni mabadiliko ya kuleta faraja. Usalama wa Taifa wanataka mabadiliko. Jeshini vivyo hivyo. Mahakamani pia. Bungeni wanataka uhuru zaidi.

Kila mmoja amechoka: Kamata. Piga. Bambika mashitaka. Weka rumande. Peleka mahakamani…kama jana, kama leo, kama kesho, kila siku. Ukombozi waja.

Ni CHADEMA waliowahi kusema kuwa “tusisubiri mwisho wa miaka mitano” ndipo tuwe na uchaguzi.

Ni kweli. Serikali iliyochoka. Iliyofilisika hoja na fedha, haistahili kuendelea kuwa madarakani kwa kisingizio cha kumaliza “muda” wake.

Inahitaji kusukumwa zaidi. Kuwezeshwa kufikiri kuwa haiwezi na kwamba kuendelea kwake kuwa madarakani ni tishio kwa amani na usalama wa wananchi.

Uwezeshaji wa aina hiyo hujitokeza katika kazi za kisiasa. Hufika wakati watawala nao wakaelimika. Waweza kuitisha uchaguzi, hata sasa, kujipima kama kweli wanaweza kuendelea kutawala au wamepwelea.

Wakishindwa wakae pembeni. Wajitafiti na kujiandaa upya; huku wakiacha fursa kwa wenye uwezo kushika madaraka.

Kuendelea kutumia polisi kuzima kauli, hakuwezi kubadili mwelekeo wa wananchi au hata wa polisi wenyewe; ule wa kutaka mabadiliko. Ukombozi waja.

0
Your rating: None Average: 4.8 (4 votes)
Soma zaidi kuhusu: