Ulanguzi wa tiketi bandarini watesa wengi


Jabir Idrissa's picture

Na Jabir Idrissa - Imechapwa 28 March 2012

Printer-friendly version

UMEFIKA bandarini. Unataka kusafiri. Hata kabla ya kufikia chumba cha kukatia tiketi, tayari umekaribishwa na vijana watatu au wanne.

Hawa ni miongoni mwa wengi ambao huishi kwa kulangua tiketi za wasafiri wanaotumia boti ziendazo kwa kasi kati ya bandari ya Dar es Salaam na Zanzibar.

Mmoja wa vijana atakueleza baadaye, “…kwa siku iliyokwisha vizuri, huweza kupata hadi Sh. 80,000” kwa kuwauzia wasafiri tiketi kwa bei ya kuruka.

Utasikia kijana akikuuliza, “Mzee unataka usafiri wa Zanzibar.” Kujibu “ndio” si tatizo, isipokuwa pale unapojiingiza na kuendelea kumsikiliza na hatimaye kumtii, ndipo utajuta.

Tatizo ni kwamba unaweza kukata tiketi mikononi mwake, ukaishia kukosa safari. Vijana hawa wamewaliza wasafiri wengi kwa kuwapa tiketi zisizo halali.

Hivi ndivyo ilivyokuwa, kwa kiasi kikubwa, hadi ujio wa vyombo vya kisasa vya usafiri majini vinavyoanzia bandarini Dar es Salaam.

Bali tatizo lingalipo kwa baadhi ya vyombo ambavyo hutumiwa na watu wengi wa kipato cha kati na chini, kwa kuwa nauli zake ni za chini ikilinganishwa na boti ziendazo kwa kasi.

Chombo kinachotumia hadi saa mbili na nusu, kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, hutoza nauli ya Sh. 25,000 kwa daraja la kwanza na daraja la kawaida Sh. 20,000.

Watoto hulipa nusu nauli ya sehemu anakosafiri.

Katika vyombo vinavyotumia muda mrefu zaidi, na kubeba abiria wengi, nauli huwa chini kidogo. Katika baadhi ya meli nauli ya chini huwa Sh. 8,000 na juu Sh. 17,000.

Hivyo ni rahisi kwa walanguzi kutumia mwanya huo kurusha tiketi. Lakini uzoefu unaonyesha kuwa tiketi hizi hutolewa kwa makubaliano na wauzaji.

Kwa mfano, wauza tiketi wanapotangaza kuanza kuuza tiketi, huchukua muda mfupi kwa zoezi hilo na ghafla hutangaza, “tiketi za chini (daraja la kawaida) zimekwisha.”

Hapa msafiri hulazimika kununua tiketi ya daraja la juu ambayo ni ghali. Kwa wale wanaoona kuna tofauti kubwa kati ya tiketi ya ulanguzi na ile ya daraja la kwanza, basi hukubali “kurushwa.”

Kuna wakati hata tiketi ya daraja la pili au tatu, huuzwa kwa bei ya daraja la kwanza. Yote haya hufanywa mchana kweupe kutegemea na wingi wa abiria.

Kwenye eneo la ukataji tiketi kuna mtandao wa ulanguzi wa tiketi unaonufaisha watu wengi, wakiwemo wafanyakazi wauza tiketi.

Ni mtandao huu, unaodaiwa kuhusisha wafanyakazi ambao unachochea wingi wa abiria wasiotambuliwa.

0
No votes yet