Ulevi wa kisiasa uliyumbisha Bunge


Joster Mwangulumbi's picture

Na Joster Mwangulumbi - Imechapwa 31 August 2011

Printer-friendly version

SIKU za mwanzo za mkutano wa nne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zilijaa ulevi wa kisiasa kupita kiasi. Hakuna aliyesimama wima kutokana na ulevi; kila mmoja aliyumba kutetea sera za vyama kama vile ulikuwa wakati wa kampeni.

Spika wa Bunge, Anne Makinda na wasaidizi wake; Naibu Spika, Job Ndugai; wenyeviti Jenister Mhagama, George Simbachawene na Sylvester Mabumba wote waliegemea kwa mawaziri na wabunge ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Bungeni ikawa kukamiana kati ya wabunge wa CCM na upinzani. Wabunge walikuwa roho juu huku spika na wenyeviti wakilazimika kila mara kusimamia kuruhusu mwongozo wa kuziba suati za wapinzani.

Kwa raha zake, Naibu Spika, Job Ndugai aliwatoa nje ya lango kuu wabunge wa CHADEMA aliodai wakorofi huku Spika Makinda ama akizuia hoja nzito au akitaka wapinzani watoe uthibitisho kwa maandishi kuhusu matamshi ambayo CCM walidai ni udhalilishaji. Huo ulikuwa ulevi tu wa siasa.

Mkakati wa wabunge wa CCM kila wakitoka kwenye kikao chao, ulikuwa kuwashushua wapinzani, kukatisha maswali na kuvuruga ujengaji hoja bungeni. Walengwa wakuu walikuwa CHADEMA, CUF na NCCR-Mageuzi.

Mbaya zaidi Spika Makinda pamoja na wasaidizi wake waliruhusu wabunge wa CCM kuwazomea wapinzani na kutumia lugha chafu, lakini wapinzani walipofanya hivyo yaani kutumia lugha kali kuzomea, kuomba fursa ya kutoa mwongozo, taarifa au ufafanuzi, walinyimwa.

Sababu za kufanya hivyo zilifafanuliwa na Ndugai katika mdahalo na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lisu kwamba ni kutokana na mkakati wa upinzani wanaotaka Bunge lisitawalike. Kumbe ni ulevi wa hofu.

Huko ndiko kulisababisha Spika Makinda na wasaidizi wake kutwishwa lawama siyo tu na wabunge wa kambi ya upinzani, bali pia wananchi kwa ujumla kutokana na kutoridhishwa na uendeshaji wa Bunge.

Waliwashutumu Spika Makinda na wasaidizi wake wote kwa kufanya kazi kama makada wa CCM badala ya kusimamia Bunge bila kujali mrengo wa kisiasa.

Watu mashuhuri kama Spika wa zamani wa Bunge, Pius Msekwa; Waziri mkuu mstaafu, Joseph Warioba; Dk. Salim Ahmed Salim walitoa maoni yao kukosoa. Wapo wananchi walioshutumu na wakafika mahali wakadai Spika Makinda hana uwezo.

Uvumilivu wa wapinzani ulipofika mwisho waliamua ‘kula sahani’ moja na Spika Makinda. Wakiwa na vielelezo au ushahidi kamili, wapinzani wakiongozwa na kambi rasmi ya upinzani bungeni walimfikisha Spika Makinda mbele ya Kamati ya Kudumu ya Kanuni za Bunge.

Pamoja na mambo mengine walilalamikia hatua ya Spika Makinda kumzuia Waziri Mkuu, Mizengo Peter Kayanza Pinda kujibu maswali ya wabunge, Tundu Lissu na Esther Matiko (CHADEMA).

Mnadhimu Mkuu wa kambi ya upinzani, Tundu Lissu alisema kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge, iwapo Mbunge hataridhishwa na uamuzi wa Spika, anaweza kupeleka malalamiko yake kwenye Kamati ya Uongozi ambayo itachunguza na kutoa suluhisho.

Majibu ya ‘kesi’ hiyo inayohusu mgogoro wa kikanuni ndani ya Bunge hayakutolewa wazi lakini Watanzania wameshuhudia mabadiliko ya uendeshaji wa vikao vya Bunge ishara kwamba umemalizika ulevi wa kisiasa.

Kwanza, Spika aliwaonya mawaziri na mara kadhaa aliwanyima fursa ya kuomba mwongozo walipowasha vipazasauti bila kufuata taratibu au aliwasema wazi pale walipokiuka kanuni.

Pili, Spika na wasaidizi wake waliwazuia wabunge, hata wa CCM kuomba mwongozo kukatisha mchango wa mbunge mwenzao, na waliporuhusu, walitoa maoni yao mwishoni.

Tatu, Spika Makinda akaacha kuhudhuria vikao vya kupeana msimamo vya CCM ili visiathiri uendeshaji wa Bunge. Akafanikiwa

Mabadiliko hayo ya uendeshaji ndiyo yalichangia Bunge au wabunge kujikita katika changamoto zenye maslahi kwa taifa badala ya vyama. Hapo ndipo wabunge wa CCM wakaanza kuibana vilivyo serikali wakishirikiana na upinzani.

Heshima ya Bunge ikarejea na wakaweka rekodi kwa kuhakikisha Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini imeongezwa ili kutatua tatizo la umeme, Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi iliongezwa ili kufufua reli na usafiri wa anga na hasa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Vilevile Bunge hilo liliweka azimio la kuongeza muda wa Shirika Hodhi la CHC ili kuwezesha shughuli ya kufuatilia ubinafsishaji kuwa na ufanisi.

Rekodi nyingine ni hatua ya Spika Makinda kuunda Kamati Teule ya kuchunguza uchangishaji fedha, uliofanywa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo ili kupitisha bajeti ya wizara hiyo. Kamati hiyo ya watu watano ina wabunge watatu wa CCM, mmoja CHADEMA na mwingine CUF.

Kikubwa kilichojitokeza katika siku za mwanzo ulikuwa ulevi wa kisiasa tu, ndiyo maana kila alipopewa nafasi ya kuchangia mbunge wa CCM alilaani maandamano ya vyama vya CHADEMA na CUF, lakini baada ya kuona mambo magumu, baadhi ya wabunge wa CCM nao walisema  watahamasisha maandamano katika majimbo yao ikiwa hawatatatuliwa shida ya usafiri majini (kama Ludewa).

Baada ya ulevi huu wa kupenda zaidi chama kuwatoka, wabunge wa CCM wakagundua kumbe hata majimbo yao yana migogoro ya ardhi, kuna mapigano makali kati ya wafugaji na wakulima, kuna vita kati ya wawekezaji na wenyeji, hakuna umeme na maji, hakuna barabara nzuri na wananchi wanahofia shirikisho la kisiasa la Afrika Mashariki.

CCM na wapinzani wamemaliza mkutano, wote kilio ni kilekile. Mafuta yapo lakini hayapelekwi kwenye mitambo ya IPTL; Kwa hiyo, umeme upo lakini hauwashwi; mafisadi wapo lakini hawashtakiwi; viongozi wazembe wapo lakini hawajiuzulu; serikali inasema ina sauti lakini inapewa saa 24 na mhindi ipandishe bei na mafuta na inatii; kibopa anataka kuvunja jengo la mahakama ajenge maegesho, serikali inasema hewala; meya anasema wabunge wanafikiri kwa kutumia makalio wote wanacheka “kwakwakwakwa”. Huu wote ni ulevi.

Kwa jumla CCM kama taasisi imejingea picha ya dereva mlevi ambaye hastahili kuachwa “anywe funda moja tu la ziada” ili aendelee kuendesha (kuongoza nchi). Mafunda ya ziada waliyokunywa kwa miaka 50 iliyopita yamewaacha hoi na sasa wanatumia dawa ya kupunguza harufu chafu ya ufisadi iitwayo kujivua gamba. Wamefanikiwa?

0789 383 979, jmwangul@yahoo.com
0
Your rating: None Average: 4 (1 vote)
Soma zaidi kuhusu: