Umaarufu wa Kikwete 'feki'


Saed Kubenea's picture

Na Saed Kubenea - Imechapwa 13 October 2010

Printer-friendly version
Mwenyekiti mwenza wa REDET, Dk. Benson Bana

KILE kinachoitwa umaarufu wa Jakaya Kikwete, mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeelezwa kuwa “taarifa za kupanga” za asasi zinazoendesha kura ya maoni, MwanaHALISI limeelezwa.

Kwa mujibu wa uchunguzi, asasi zilizotoa taarifa za umaarufu wa wagombea urais nchini, zina uhusiano wa karibu na ikulu.

Wakati Mpango wa Utafiti na Elimu ya Demokrasia wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (REDET) ni taasisi iliyo chini ya chuo kikuu kinachomilikiwa na serikali, kampuni ya Synovate imekuwa na uhusiano wa kibiashara na ikulu.

Si hayo tu. Mwenyekiti wa REDET, Profesa Rwekaza Mukandala, ni mteule wa Kikwete katika nafasi yake ya sasa ya makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na rafiki yake wa karibu.

“Taarifa za asasi hizi mbili ni geresha tu,” ameeleza mwalimu mmoja wa chuo kikuu Mlimani ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini.

Hata hivyo, wasomi mbalimbali wamesema CCM haina sababu ya kufurahia matokeo hayo kwa kuwa yanaonyesha mporomoko mkubwa wa Kikwete tangu Machi mwaka huu.

“Kama asasi zingekuwa makini na kuzingatia ukweli, umaarufu wa Kikwete kwa sasa ungeonyeshwa kuwa chini ya asilimia 50,” ameeleza Dk. Sengondo Mvungi, mhadhiri katika Shule ya Sheria ya UDSM.

“Kwanza mimi sikubaliani kabisa na hizo kura za maoni zilizopigwa na REDET na Synovate. Hii ni kwa sababu zimeacha kuangalia vitu vingi muhimu kama vile usawa miongoni mwa vyama.

“CCM ina fedha zaidi kuliko vyama vingine. Ina nguvu kubwa ya kipropaganda kuliko vyama vingine na inalindwa kisheria kama chama tawala kuliko vyama vingine. Kura hizi za maoni hazikuangalia haya,” ameeleza Dk. Mvungi.

Amesema haiingii akilini, wakati kampeni zinaendelea, gazeti la serikali, Daily News, liseme Dk. Slaa hatashinda; na majeshi yaseme “watakaoshindwa wakubali matokeo, la sivyo watakiona.”

“Binafsi, ninaamini kama kura hiyo ingefanywa kisayansi zaidi, hata katika mazingira yaliyopo, Kikwete angepata pungufu ya asilimia 50. Matokeo ya sasa yamepangwa kuifurahisha serikali iliyo madarakani,” amesema.

Nazo nyaraka ambazo gazeti hili linazo zinaonyesha kuwapo kwa mahusiano ya karibu, ya kibiashara na kibinafsi, kati ya ikulu na kampuni ya Synovate.

Mahusiano hayo yameonekana katika madokezo kadhaa yaliyotoka kwa Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Salva Rweyemamu kwenda kwa katibu wa rais, mwenyekiti wa bodi ya tenda ya ikulu na mkuu wa shughuli za ikulu (Mnikulu).

Rweyemamu katika maelezo yake anasema, tayari amefanya mazungumzo na uongozi wa kampuni ya Synovate Tanzania (zamani ikiitwa Steadman Group) na kukubaliana kufanya kazi ya kitafiti.

Rweyemamu amemthibitishia katibu wa rais katika dokezo lake, kwamba kinachotakiwa na ikulu ndicho kitatekelezwa na uongozi wa Synovate, na kwamba baadhi ya huduma hizo watazipata bila kulipia chochote.

Kuvuja kwa taarifa za kuwapo kwa mawasiliamo ya kibiashara na binafsi kati ya serikali na Synovate kumekuja siku tatu tangu kampuni hiyo kutoa kile ilichoita, “Ripoti ya utafiti wa kisiasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.”

Katika ripoti yake, Synovate wanasema iwapo uchaguzi mkuu ungefanyika Jumamosi iliyopita, Kikwete angeibuka mshindi kwa asilimia 61.

Washindani wakuu wawili wa Kikwete, Dk. Willibrod Slaa anayewania urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama cha Wananchi (CUF), wangepata chini ya asilimia 22, kufuatana na taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa Synovate, kama uchaguzi ungefanyika siku hiyo, Dk. Slaa angepata asilimia 16 ya kura, huku Prof. Lipumba akiambulia asilimia tano tu.

Katika moja ya madokezo, kutoka kwa Rweyemamu kwenda kwa katibu wa rais, mapema mwaka huu, mkurugenzi huyo wa mawasiliano anaithibitishia ofisi ya rais, kuwa tayari amefanya majadiliano na watendaji wakuu wa Synovate, na kuahidi kutekeleza kile ambacho ikulu inataka.

Rweyemamu anataka Synovate iwaandalie kura ya maoni. Aidha, Rweyemamu anataka kampuni hiyo ieleze kuhusu “nguvu ya vyombo vya habari nchini kwa sasa kutokana na utafiti wao ambao unaonyesha ni chombo kipi kina nguvu ipi na katika maeneo yapi ya nchi au makundi gani ya wananchi.”

Anasema tafiti hizo ni nyenzo muhimu kwao hasa kutokana na kujiandaa na matukio yajayo. Hakuyataja matukio hayo.

Mkurugenzi huyo wa mawasiliano ya rais anasema amethibitishiwa na Synovate kwamba “presentation ya kura ya maoni tutaipata bure, lakini ile ya vyombo vya habari tutalazimika kulipia kama tunahitaji kupata ripoti kamili. Nitakujulisha gharama zao baada ya kuwa nimezungumza nao kwa kina.”

Akisisitiza kuwa hakuna mabadiliko ambayo yatatokea, Rweyemamu anasema, “Nakuomba kama unaweza kuwaarifu maofisa wengine wa OBR – ofisi binafsi ya rais – ambao wako Dar es Salaam kuja kushiriki nasi katika kuona presentations hizo kuanzia saa tisa mchana kwenye ukumbi wa mikutano wa Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais.”

Nayo ripoti ya Redet iliyotolewa Alhamisi wiki iliyopita – siku tatu kabla ya ripoti ya Synovate – inasema Kikwete angeshinda kwa asilimia 71. Wanatofautiana kwa asilimia 10. Bali ripoti ya Redet ya Machi mwaka huu inaonyesha Kikwete alikuwa mashuhuri kwa asilimia 77.2.

Hii ina maana kwamba umaarufu wa Kikwete umekuwa ukiporomoka wakati ule wa upinzani ukiongezeka.

Machi alipata asilimia 77.2 (Redet). Septemba akapata asilimia 71 (Redet) na mwezi huohuo akapata asilimia 61 (Synovate).

Kwa mporomoko wa wastani wa asilimia 10 kwa wiki, kama taarifa za Redet na Synovate zinavyoonesha, hadi kufikia wiki ya mwisho ya uchaguzi, Kikwete atakuwa ama amepanda kidogo au ameshuka hadi asilimia 30.

Profesa Mwesiga Baregu, mwenyekiti wa kampeni wa CHADEMA, alipoulizwa kuhusu uwezekano wa mporomoko wa Kikwete hadi asilimia 31 ifikapo mwishoni mwa mwezi huu alisema, “Sitashangaa hayo yakitokea.”

Alisema utafiti wa asasi hizi ulifanyika wakati wananchi hawajahamasika na wagombea hawajawafikia.

“Kimsingi kampeni za wagombea zilikuwa hazijapamba moto kati ya Machi na Julai mwaka huu wakati Redet wanafanya utafiti. Sisi hatukuwa na mgombea wa urais. Dk. Slaa alikuwa hajadhaniwa kuwa mgombea,” anaeleza Prof. Baregu.

Anasema ukitafakari yote haya, utaona kuwa sasa wananchi wameanza kutafakri na kufanya maamuzi.

Hata tafiti za Redet ambazo zinalalamikiwa, zinaonyesha kuwa Kikwete amekuwa akishuka kutoka pale walipoanza utafiti hadi walipomaliza.

Naye Dk. Azaveli Lwaitama, mhadhiri wa philosofia UDSM, amesema hakubaliani na utafiti uliofanyika kwa kuwa Redet haijataja umri wa waliohojiwa.

“Hawa hawajasema waliohojiwa ni watu wa umri gani. Je, wamehoji wazee wengi na kuacha vijana ambao Mama Salma Kikwete anasema wamepatwa wazimu na kuwataka wazazi wawatulize ili waichague CCM,” anahoji.

Anasema hakuna sababu ya kusheherekea matokeo yaliyotolewa na asasi za Redet na Synovate.

Dk. Lwaitama anasema maswali yaliyoulizwa hayakulenga kutoa majibu sahihi, “…labda kama CCM wanataka kufanya mzaha. Lakini hata CCM wanajua kuwa matokeo ya Redet si sahihi na Redet ni chombo cha serikali; hivyo hakiwezi kutenda kinyume cha watawala.”

Hadi juzi Jumatatu usiku, watu 2,375 walikuwa wamepiga kura kwenye mtandao wa MwanaHALISI, www.mwanahalisi.co.tz, uliofunguliwa kwa watu binafsi tangu 25 Agosti mwaka huu, ulikuwa na matokeo yafuatayo:

Kikwete: 8%
Dk. Slaa: 87%
Lipumba 4%
Wengine: 1%

0
No votes yet
Soma zaidi kuhusu: