Umasikini wetu unasababishwa na viongozi


Benson Msemwa's picture

Na Benson Msemwa - Imechapwa 02 June 2010

Printer-friendly version
Mtazamo

MWAKA 2003, kulikuwapo na mjadala katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu nini hasa sababu ya nchi yetu kuendelea kuwa masikini miaka zaidi ya 40 baada ya uhuru.

Tupende au tusipende huu ni wakati wa kuelezana ukweli mchungu kuwa tatizo kubwa ni kuwa na viongozi na watawala ambao ni wasaka tonge, wanaofikiri kwa kutumia matumbo yao, bila ya kushirikisha vichwa vyao.

Umaskini unaongezeka kila kukicha, mfumuko wa bei usioshikika, maisha yaliyovaa taiti (magumu). Hayo yote ni matokeo ya viongozi na watawala wetu wanaofikiri kwa kutumia matumbo yao, ndio maana wanakuja na majibu mepesi kwa maswali magumu.

Hivi juzi tumesikia huko Kilimanjaro kuwa gari la serikali lilinunuliwa kwa Sh. 155 milioni miaka michache iliyopita lakini sasa mkubwa mmoja anataka auziwe kwa bei ya chini ya milioni 10.!

Huu ni ubinafsi uliopindukia uzalendo wetu upo wapi? Ningefurahi kama ningesikia hilo gari wamelibadili kuwa gari la wagonjwa au wamelifanyia mnada na kununua matrekta ili kuimarisha utekelezaji wa sera ya Kilimo Kwanza.

Kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli na dizeli kila kukicha, jaribu kuwabana ili watoe sababu za kwa nini yote hayo?. Hata hawataumizi vichwa vyao utasikia “Soko la dunia bei imepanda kwa sasa na hatuna namna ya kukwepa hilo”.

Hapo ndipo pa kujiuliza, uwapi ubunifu, umakini, fikra mbadala na endelevu za kunusuru mfumuko wa bei ambao unawatesa watanzania? Wako wapi na wanafanya nini hao wanaotembelea VX, GX, na V8? Waliomo kwenye ofisi zenye viyoyozi? Au kwa kuwa wao magari yao hayaingii kwenye hivi vituo vyetu vya mafuta? Wanatumia vichwa kweli?

Tunauza magogo tunaagiza toka nje vijiti vya meno (toothpick), hiki kichekesho cha karne, kweli tumeshindwa hata kuwa na kiwanda cha toothpick? Hadi kwenye meza zetu nyumbani ,kwenye baa, masherehe mbalimbali kumejaa vikopo vyenye njiti za meno zilizoandikwa Made in China? Aibu tupu?

Nani wa kulaumiwa? Ni Mkuu wa Kitivo cha Uhandisi pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (USDM) au St Joseph kwa kushindwa kutoa wataalamu hata wa kutengeneza toothpick? Au kuna watu wenye asilimia kumi zao kwenye kuuza magogo nje na kuingiza toothpick?

Hapo ndio inajengeka dhana nzima ya kushirikisha matumbo na si vichwa vyetu kwenye kufikiri. Vipo wapi Mwatex, Kiltex, Mutex, Urafiki (marehemu anayetembea)? Nani ameviua? Au ndio kushirikisha matumbo na si vichwa vyetu?

Janga la njaa sasa limeshakuwa swahiba wetu mkubwa na hivi karibuni bila hata aibu na tena mbele ya vyombo vya habari mtu anathubutu kusema Japan watatoa msaada wa mchele kwa Tanzania, vyovyote utakavyokuwa iwe ni msaada, mkopo au wanakuja kufanya biashara .

Ni utaahira usiotibika hata ukienda Mirembe; tunaruhusu hilo kwa maslahi ya nani? Yanafanya nini mabonde ya Rufiji yenye uwezo wa kulisha Afrika nzima, Kilombero bonde bikra lipo wapi? Usangu kupo wapi? Hivi kweli tunashirikisha vichwa vyetu? Huu ni utani wa kuaibisha.

Mpo wapi viongozi au tuwakumbushe ule wimbo wa Tazama ramani utaiona nchi nzuri, yenye mito na mabonde mengi ya nafaka? Hii ni nchi ya Tanzani, nchi ya neema iliyogeuka kuwa ya karaha kutokana na uvivu wa viongozi wake kufikiria.

Tumeshuhudia vijana waliokuwa masomoni Ukraine wakirudishwa nchi eti serikali haiwezi kuwakopesha kusoma huko; hizi ni fikra potofu,ni mawazo mpauko ya watawala na viongozi wetu; Taifa gani duniani lililoendelea bila kuwekeza kwenye rasilimali watu?

0
No votes yet