Umbali shuleni bado kero


Nicoline John's picture

Na Nicoline John - Imechapwa 30 June 2009

Printer-friendly version

SHULE za sekondari za kata zimejengwa nyingi mijini na vijijini baada ya wananchi kutekeleza agizo la serikali ya awamu ya nne.

Ilipoleta mpango wake huo mwaka 2006, wa kutaka wazazi kuchangia ili kufanikisha ujenzi wa shule hizo, serikali ilisema zitakuwa suluhisho la tatizo la uhaba wa nafasi kwa watoto wanaomaliza elimu ya msingi.

Idadi kubwa ya watoto wanashindwa kuendelea na elimu ya sekondari kwa sababu serikali hufanya uchaguzi wa wanafunzi wa kidato cha kwanza kwa kuzingatia nafasi katika shule zake.

Lakini, serikali pia ilisema ujenzi wa shule za sekondari za kata utapunguzia wanafunzi usumbufu wa kufuata elimu maeneo yaliyo mbali na wanapoishi.

Kwamba pale itakapojengwa shule ya sekondari katika kata husika, watakaochaguliwa kujiunga na shule hiyo watakuwa watoto wa familia zinazoishi ndani ya kata hiyo.

Sasa hali ni tofauti. Wakati wananchi wamejitahidi na kufanikiwa kujenga shule kwenye kata zao, tayari malalamiko yameenea hasa maeneo ya miji na majiji, kwamba pamoja na matatizo ya miundombinu mibaya, wapo watoto wamepangiwa shule za mbali na kwao.

Hii inawawia vigumu wanafunzi kwa sababu wengine wanakaa mbali na shule walizopangiwa. Kuna wanaosafiri kilometa 10 hadi 20 kutoka nyumbani kwenda shuleni.

Usafiri ni tatizo kubwa linalowapata wanafunzi wa shule za maeneo ya majiji na miji. Tatizo hilo limekithiri katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha na Mbeya.

Ni vigumu kupita siku bila ya kusikia migogoro kati ya wanafunzi na makondakta wa magari binafsi ya abiria (daladala). Wakati wanafunzi huwa wanagombania kupanda basi kwa nauli halali iliyotangazwa na serikali kwa ajili yao, makondakta huwakatalia.

Katika tatizo hilo, wanafunzi wasichana ndio wanaoathirika zaidi kwa vile ni wachache wenye uwezo wa kupambana na makondakta jeuri.

Kutokana na tatizo hilo, ni dhahiri mazingira ya kusoma yanakuwa magumu kwa wanafunzi wanaokaa mbali na shule wanazosoma kuliko wale wanaoishi karibu na shule zao.

Mwanafunzi mmoja analalamika kuwa inamchukua saa nne kufika shule ingawa anawahi kuamka alfajiri hata kabla ya wanaokwenda kusali.

“Nikifika shule huwa nimechoka sana; inakuwa vigumu kusoma. Kwa kuwa ninaamka usiku, mara nyingi najikuta nikisinzia darasani,” anasema.

Hutokea wakati wanafunzi wanaochelewa kufika shule wakazuiwa kuingia darasani. Kwa kutarajia huenda ikafika muda wakaitwa ili waungane na wenzao, wanabaki nje ya majengo na kusubiri. Ni tatizo kwa watoto na wazazi.

Familia zinalazimika kutumia fedha nyingi kwa ajili ya nauli. Mzazi anahitaji angalau Sh. 2,000 kila siku ambazo kwa mwezi ni sawa na Sh. 48,000. Hapa ndipo mzazi huyu anapotoa kilio.

Sasa wazazi wana mawazo hasi kuhusu mfumo wa sekondari kwa shule za kata. Ni mfumo usio na nafuu kwao kifedha. Lakini pia kutokana na watoto wao kusoma mbali na wanapoishi, wanahofia usalama wao.

Tatizo la watoto kupelekwa shule za mbali na wanapoishi ni moja tu ya matatizo mengi yanayohusu mfumo wa shule za kata.

Shule nyingi hizi zina upungufu wa walimu. Walimu wengi hawataki kufundisha katika shule zilizoko maeneo ya vijijini kutokana na ugumu wa maisha.

Walimu wanapofika kwenye shule hizo vijijini na kukuta hakuna uhakika au urahisi wa mahitaji muhimu kimaisha, wanavunjika moyo na hatimaye kuondoka.

Wengi wanahama na ikibidi, hata kuacha kazi, ili kuondokana na maisha ya shida vijijini.

Hakuna nyumba za walimu; hakuna maji wala umeme. Kwa zile shule za masomo ya sayansi, hakuna maabara na vifaa. Pia baadhi ya shule zipo maeneo ya makazi ya watu na shughuli nyingi za biashara.

Mazingira haya si mazuri kwa kusoma na hayaleti matumaini ya maendeleo katika shule za kata.

0
No votes yet